visa

Shinyanga: Mbaroni kwa Kukutwa na Dhahabu Bandia

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linawashikilia watuhumiwa watatu kwa kukutwa na vipande 10 vya madini bandia aina ya dhahabu wakiwa kwenye harakati za kuyauza wilayani Kahama.

 

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Richard Abwao, alisema watuhumiwa hao walikuwa na mtambo wa kufyatua madini hayo bandia ya dhahabu ambayo huyauza wilayani Kahama, Geita  na Mwanza.

 

Alisema katika msako ya uhalifu ambao waliufanya mwezi uliopita mkoani humo, walifanikiwa kukamata watuhumiwa 73 wa matukio mbalimbali ya uhalifu, wakiwamo wezi, wauaji,  na watu watatu kwa utengenezaji wa madini bandia ya dhahabu.

 

“Watuhumiwa hawa tuliwakamata wakiwa na vipande 10 vya madini bandia aina ya dhahabu na walikuwa kwenye harakati ya kuyauza wilayani Kahama, na wamekuwa wakiyauza pia Geita,  na Mwanza,” alisema Abwao.

 

“Katika msako huo pia tulifanikiwa kukamata watuhumiwa 48 wakihusika na uuzaji madawa ya kulevya aina ya bangi kilo 229, mirungi kilo 117, cocaine kilo 117, heroine gramu 189, pikipiki tatu, televisheni sita, Laptop mbili, Subwoofer moja, pamoja na mitambo ya gongo 27,” aliongeza.

 

Alisema pia walifanikiwa kukamata watuhumiwa wanne waliohusika na matukio ya mauaji ya Kalekwa Shiku (50) mkazi wa kijiji cha Mishepo, Shinyanga Vijijini, ambaye aliuawa kwa kufunikwa mfuko usoni, kufungwa mawe miguuni, na kisha kuzamishwa kwenye bwawa la maji na kufariki dunia.

 

Alisema watuhumiwa hao walitekeleza mauaji hayo Juni 6, mwaka huu, kwa madai ya tamaa ya kutaka kujipatia ng’ombe tisa kwa mwanamke huyo na baada ya kugoma ndipo wakatekeleza mauaji hayo.

 

Alisema watuhumiwa wote waliohusika na matukio hayo ya uhalifu na mauaji mkoani humo, wanawashikilia na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani ili sheria ifuate mkondo wake.
Toa comment