The House of Favourite Newspapers

Bodi Mpya ya ATCL Yatakiwa Kuusuka Upya Uongozi wa Sasa

atcl-1
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati) akitoa maelekezo kwa bodi mpya ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) wakati alipoitambulisha jijini Dar es Salaam. Waziri huyo alitoa miezi mitatu kwa bodi hiyo juusuka upya uongozi wa shirika hilo ili kuleta ufanisi.  Kulia ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Eng. Edwin Ngonyani na kushoto kwake ni Katibu Mkuu Eng. Leonard Chamriho.
atcl-2Profesa Makame Mbarawa akisisitiza jambo katika hotuba yake.

Akizungumza jijini Dar es Salaam mara baada ya kuitambulisha bodi mpya ya Shirika la Ndege Tanzania (ACTL), Waziri Mbarawa amesema kuwa uteuzi wa bodi hiyo utasimamia kuleta tija na ufanisi wa shirika hilo ambalo kwa kipindi kirefu lilikuwa na changamoto nyingi.

“Nataka kuona mabadiliko makubwa kuanzia kwenye menejimenti hadi uongozi wa chini, hakikisheni mnaweka uongozi ambao utafuata maadili, utakuwa na ufanisi, ubunifu na kasi katika utendaji kazi,” amesema Profesa Mbarawa.

Aidha, ameitaka bodi hiyo kusimamia na kuboresha mpango wa kibiashara wa usafirishaji (Business Plan) katika shirika hilo ili  kumudu soko la ushindani na  kuongeza mapato ya shirika hilo.

“Kama mnavyojua usafiri wa anga una ushindani mkubwa, hivyo ili serikali iweze kupata faida katika biashara hii ni lazima tuboreshe mpango wa kibiashara unaoendana na wakati,”amesisistiza  Mbarawa.

Pia ameitaka bodi hiyo kuipa ATCL mifumo imara, makini na mahiri ili  kutatua changamoto zinazoikabili shirika hilo ikiwemo wizi wa mafuta ya ndege na upotevu wa mapato.

Ili kupima ufanisi wa utendaji wa shirika hilo, ameitaka bodi hiyo kuandaa mkataba kwa kila mfanyakazi kuanzia ngazi ya juu hadi chini.

Katika hatua nyingine waziri huyo amesema kuwa serikali ina mpango wa kununua ndege mbili mpya aina ya Jet ifikapo mwaka 2017 kwa lengo la kuboresha sekta ya usafirishaji wa anga nchini.

Naye Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani, ameitaka Bodi hiyo kutumia fursa walioipata katika kufanya kazi vizuri ili kufufua shirika hilo na kuwapatia watanzania huduma sahihi na bora za usafirishaji.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Emmanuel Korosso, ameahidi kushirikiana na wajumbe wa bodi yake katika kutekeleza maelekezo ya Waziri haraka iwezekanavyo ikiwemo kubadilisha menejimenti ya shirika hilo.

Imetolewa na Kitengo
cha Habari na Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Comments are closed.