The House of Favourite Newspapers

SHKUBA, WENZAKE WAHENYA KORTINI ‘KWA TRUMP’

Shkuba na wenzake kortini.

 

DAR ES SALAAM: Wakati vita ya kupambana na madawa ya kulevya ikionekana kufanikiwa kwa kiasi flani hapa nchini, taarifa mpya iliyotua kwenye dawati la gazeti hili ni kwamba, hivi karibuni Watanzania watatu wamepandishwa kizimbani Texas, California nchini Marekani kwa tuhuma za kujihusisha na biashara hiyo haramu.

 

Akizungumza na UWAZI kwa njia ya simu, Kamishna wa Sheria wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini, Edwin Kakolaki amewataja Watanzania hao kuwa ni Ally Haji ‘Shikuba’, Iddy Mfuru na Tiko Adam ‘Tikotiko’ ambao kesi yao imeshaanza kusikilizwa nchini humo.

“Katika uendeshwaji wa kesi hiyo tumekuwa tukishirikiana na Marekani kwa kupeana taarifa mbalimbali kwa kila kinachoendelea.

 

 

“Taarifa walizotuletea hivi karibuni ni kwamba wameshawapandisha kizimbani na kuwasomea mashitaka yao ya kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya,” alisema Kakolaki. Alisema watu hao wanashitakiwa kwa makosa ya kusambaza na kujihusisha na biashara hiyo haramu nchini Marekani.

 

Wakati watuhumiwa hao wakihenyeshwa kortini, hapa nchini mambo yanazidi kuwa moto kufuatia mamlaka ya kuzuia na kupambana na madawa ya kulevya kuonesha kujizatiti kuhakikisha wafanyabiashara wanaotumia njia za panja kuingiza madawa hayo hawafui dafu.

 

Akizungumzia hilo, Kamishna wa Intelijensia wa Mamlaka hiyo ya kuzuia madawa ya kulevya nchini, Frederick Kibuta alisema cocaine na heroine hazizalishwi hapa nchini, zinatoka nje ya nchi na kuingizwa kwa njia mbalimbali.

 

“Kwa upande wetu tunapambana kuhakikisha madawa hayo hayaingii nchini kwa namna yoyote, iwe kupitia mipakani au viwanja vya ndege, tumejizatiti vilivyo,” alisema.

 

Tiko.

TUJIKUMBUSHE YA AKINA SHKUBA

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, chini ya Hakimu Mkazi, Cyprian Mkehe Aprili 12, 2017 ilikubali ombi la Wizara ya Sheria na Katiba la kuruhusu mtuhumiwa wa kusafirisha madawa ya kulevya, Shkuba na wenzake wawili, Mfuru na Tikotiko, wasafirishwe kwenda Marekani kujibu mashtaka ya kusafirisha madawa ya kulevya.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers William Sianga.

 

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mkehe alisema anakubaliana na maombi ya serikali kama yalivyowasilishwa na vielelezo ikiwemo barua kutoka Serikali ya Marekani ikiomba watuhumiwa hao kusafirishwa kwenda nchini humo kwani serikali ya Marekani ilikuwa inamsaka Shkuba kwa muda mrefu.

Mwaka jana Marekani ilimtangaza Shkuba kuwa ni kinara wa usafirishaji wa madawa ya kulevya kwenye nchi za Afrika, Asia, Marekani ya Kaskazini kupitia Afrika Mashariki ambako ndiko kwenye ngome yake. Shkuba alikamatwa Februari 2014 akijiandaa kupanda ndege kwenda Afrika Kusini akiwa na kilo 210 za heroin.

STORI: RICHARD BUKOS, UWAZI

Comments are closed.