The House of Favourite Newspapers

SHOO YA JIDE, BASTOLA YAZUA TAHARUKI MBELE YA WAZIRI!

MWANAUME mmoja ambaye jina halikuweza kupatikana mara moja, ameibua taharuki ya aina yake baada ya kuonekana akiwa na bastola kwenye shoo ya mwanamuziki Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ au ‘Jide’, Ijumaa Wikienda lilikuwepo.  

 

Shoo hiyo ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza na vigogo wengine wa kada mbalimbali.

NI MLIMANI CITY

Tukio hilo lilijiri usiku wa Jumamosi iliyopita katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar wakati jamaa huyo alipokuwa akigombana na mwanaume mwingine (jina halipatikana pia), jirani kabisa na eneo alilokuwa amekaa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

 

WAZICHAPA KAVUKAVU

Wakati onesho hilo likiwa linaendelea ndipo ghafla likazuka timbwili ambapo jamaa mmoja aliyevalia shati jeupe alionekana akizichapa kavukavu na jamaa mwingine aliyevalia ‘kiboditaiti’ cha rangi ya kijivu. Kabla hayajatokea madhara makubwa watu wa usalama waliingilia kati na kutuliza ‘vurumai’, lakini tayari taharuki ilishazuka ukumbini hapo, meza kadhaa zilipinduliwa kibabe na mazagazaga yote yaliyokuwemo kusambaratika.

BASTOLA YAONEKANA

Taharuki zaidi ilizuka baada ya jamaa aliyevalia kiboditaiti kuonekana akiwa na bastola kiunoni huku akipambana ambapo baadhi ya mashabiki waliokuwa jirani na eneo la tukio walipoiona walianza kutawanyika huku wakioneshana silaha hiyo wakimuhofia jamaa huyo huenda angeitumia endapo angezidiwa nguvu. “Mh sasa pale si hatari, jamaa akizidiwa si anaitoa halafu itakuwa balaa hapa tuondoke fasta,” alisikika mmoja wa mashabiki huku akitoweka eneo hilo na kusababisha kimbikimbia ya watu.

 

Wakati varangati hilo likiendelea, Waziri Shonza aliyekuwa mbali kidogo na eneo hilo alionekana kutulia kwenye kiti kama vile mtu aliyekuwa hana mpango na timbwili hilo, lakini Makonda ambaye alikuwa karibu na timbwili hilo alionekana kuwaangalia jamaa hao kisha kuwapotezea na kuendelea na maongezi yake na wanamuziki wa Kizazi Kipya, Ambwene Yessayah ‘AY’, Hamisi Mwinjuma ‘MwanaFA’ na Meneja wa Wasafi classic Baby (WCB), Hamis Taletale ‘Babu Tale’.

 

CHANZO CHA TIMBWILI

Chanzo cha timbwili ilidaiwa kuwa ni mmoja kati ya jamaa hao waliokuwa wakizichapa kumfanyia bughudha mwanamke wa mwenzake ambapo mwanamke huyo baada ya kuona jamaa hao wakizichapa, alianza kupiga mayowe kuomba msaada. Hata hivyo, vurumai hiyo ilitulizwa na walinzi maalum wa shoo hiyo na burudani ziliendelea hadi pale Jide alipomaliza kutumbuiza.

Jitihada za kuzungumza na jamaa hao hazikuzaa matunda kufuatia mwanahabari wetu kushindwa kuwafikia wawili hao waliotokomea kusikojulikana baada ya tukio hilo. Shoo hiyo ilihudhuriwa na watu mbalimbali mashuhuri ambapo mbali na Waziri Shonza na Makonda, pia alikuwepo mwanasiasa mkongwe, John Cheyo na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza.

 

JIDE AMERUDI?

Kama kawaida yake, Jide huwa anapotea na kurudi hivyo shoo hiyo ilikuwa ya makusudi kwa ajili ya kumrejesha machoni na masikioni mwa mashabiki wake

STORI: Richard Bukos, DAR

Mama Mzazi wa Isaac Gamba: Sitomsahau Mwanangu

Comments are closed.