The House of Favourite Newspapers

Sibomana Aimaliza Township

IKIWA imesalia saa chache kabla ya Yanga kushuka uwanjani kukipiga mechi ya kimataifa, kuna habari njema kwa mashabiki wa timu hiyo. Benchi la ufundi la kikosi cha Yanga, likiongozwa na kocha wake mkuu, Mwinyi Zahera, raia wa DR Congo, limefunguka kuwa limeshapata dawa ya kuwakabili wapinzani wao, Township Rollers ambao watapambana nao katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kesho Jumamosi.

 

Yanga imepata matumaini hayo kutokana na kucheza mechi mbili za kirafiki ambazo ni sawa na dakika
180, huku mshambuliaji wa timu hiyo, Mnyarwanda, Patrick Sibomana akiwa na rekodi nzuri ndani ya kikosi hicho licha ya muda mfupi tangu aanze kuitumikia timu hiyo. Yanga watakuwa wenyeji wa Rollers katika pambano la Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.

Kabla ya mchezo huo Yanga walijichimbia visiwani Zanzibar ambapo walicheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Mlandege na jana dhidi ya Malindi. Sibomana ambaye anatumia zaidi mguu wa kushoto anaongoza kwa kufunga katika kikosi cha Yanga kuliko wachezaji wengine wote. Katika mechi nane za kirafiki hadi jana jioni, alikuwa amefunga saba akifuatiwa na Mganga, Juma Balinya ambaye amezifumania nyavu mara tano. Mechi hizo ni sita ambazo Yanga ilicheza ilipokuwa kambini Morogoro, nyingine ni dhidi ya Kariobangi Sharks ya Kenya na Mlandege ya Zanzibar.

 

“Nashukuru Mungu kwa hilo lakini mipango yangu ni kuhakikisha nafanya vizuri zaidi ili niweze kuisadia timu yangu,” alisema Sibomana alipoulizwa juu ya kasi yake ya mabao. Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, ameliambia Championi Ijumaa kuwa katika mechi hizo mbili, kocha Zahera amekuwa akizitumia kwa ajili kurekebisha makosa ambayo yalijitokeza katika mechi yao na Kariobangi Sharks ya wiki iliyopita lakini ametumia kwa ajili ya kusaka kikosi cha kwanza kitakachopambana na Rollers.

 

“Kocha Zahera ndiye ambaye aliomba timu ipate mechi mbili ili asawazishe makosa ya wachezaji hasa baada ya ile mechi yetu na Kariobangi.

 

Anachokifanya katika mechi hizi mbili ni kuyafuta makosa ambayo yalifanywa na wachezaji katika mchezo wetu huo uliopita. “Lakini pia anatumia kwa ajili ya kusaka kikosi cha kwanza ambacho atakitumia katika mchezo wetu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers. Baada ya mechi hizi mbili kukamilika basi kila kitu kitakuwa sawa na tunaamini tutafanya vizuri katika mechi hiyo huku tukiwataka mashabiki wetu waje kwa wingi kwa ajili ya kutushangilia,” alisema Hafidh.

 

MBINU ZA MBELGIJI KUTUMIKA Wakati huohuo, mabosi wa Yanga wameweka mikakati thabiti ya kuhakikisha wanafika mbali kwenye michuano hiyo ambapo Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela amesema kuna mikakati mikubwa ya kuhakikisha wanashinda michezo yao yote ya nyumbani.

 

Ikumbukwe kuwa msimu uliopita mkakati kama huo ulitumiwa na Simba inayofundishwa na Mbelgiji, Patrick Aussems katika michuano ya kimataifa.

 

“Tunafahamu ugumu wa mashindano haya kutokana uzoefu tulionao, tunafahamu ugumu unakuwepo ugenini zikiwemo fitna za wenyeji, hivyo kamati yetu husika ilikutana kuweka mikakati ya ushindi kwa kuanzia mchezo wetu wa Jumamosi.

 

“Kikubwa mashabiki niwatake wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kuisapoti timu yao watakapokuwa uwanjani kama ilivyokuwa siku ya kilele cha Wiki ya Mwananchi,” alisema Mwakalebela.

 

Ameongeza kuwa kikosi chao kitarejea Dar es Salaam, leo usiku kwa ajili ya mchezo huo wakitokea Zanzibar walipoweka kambi ya siku tano kujiandaa na mchezo huo wa kimataifa.

Waandishi: Said Ally, Wilbert Molandi na Sweetbert Lukonge

Comments are closed.