The House of Favourite Newspapers

SIKU MOJA BAADA YA KUOLEWA… BIBI HARUSI AIKIMBIA NDOA!

 

Siku moja tu baada ya kuolewa kisha kwenda kuishi kwa mumewe kwa siku moja, bibi harusi, Shani Saidi ‘15’, Mkazi wa Manyuki-Kihonda mkoani hapa ameikimbia ndoa yake kisha kurejea kwao, mtandao wa Global Publishers ina mkasa kamili.

Uchunguzi wa mtandao wa Global Publishers ulibaini kwamba, wakati Serikali ya Awamu ya Tano ikisisitiza maadili kwenye jamii na haki za watoto kuzingatiwa, mama mzazi wa Shani, Sophia Ally anadaiwa kumuozesha binti yake huyo kwa mwanaume aliyetajwa kwa jina la Hassani Ally, naye mkazi wa maeneo hayo ambaye alikataa katakata kutaja umri wake.

Tukio hilo la ndoa na harusi lilijiri Februari Mosi, mwaka huu nyumbani kwa mama huyo, Manyuki-Kihonda kabla ya siku moja baadaye, Shani kumtoroka mumewe huyo na kurejea nyumbani.

 

JPM ATAJWA

Taarifa zilizopatikana kijijini hapo zilieleza kuwa, mama Shani alidaiwa kumficha bintiye huyo baada ya kutonywa kuwa, kitendo alichokifanya cha kumuoza bintiye akiwa chini ya umri wa miaka 18 ni kinyume cha sheria na kwamba serikali ya Rais John Pombe Magufuli ‘JPM’ atamtia ndani.

Habari zilieleza kwamba, baada ya kukimbiwa, jamaa huyo alifanya uchunguzi kujua alipokwenda mkewe huyo ambapo alielezwa kuwa yupo kwa mama yake, ndipo akafika nyumbani kwa mama Shani akiwa na hasira kisha kuanzisha timbwili zito.

TIMBWILI UKWENI

Wakati akiangusha timbwili hilo ukweni, jamaa huyo alikuwa akitaka apewe mkewe au gharama zake za kifunga uchumba, mahari, matunzo ya mwezi mmoja aliyotoa na pesa za gauni la harusi alilomnunulia Shani.

Baada ya kutokea kwa mtafaruku huo, gazeti hili lilifika kijijini hapo ambapo ni zaidi ya kilomita nane kutoka Morogoro mjini.

Bi Harusi, Shani Saidi.

BIBI HARUSI

Mwandishi wa mtandao wa Global Publishers alipofika, alikuta mzozo ukiendelea ambapo alipata nafasi ya kufanya mahojiano na wahusika wote akianza na bibi harusi mwenyewe ambaye alifunguka juu ya sakata hilo:

“Baada ya kumaliza darasa la saba, kwa bahati mbaya sikubahatika kufaulu hivyo nilikuwa ninafanya kazi kwa mamantilie hapa Manyuki.

 

“Wakati nikiendelea na kazi hiyo ndipo alipofika kijana huyu (akimuoneshea kidole Hassani), akaongea na mama yangu (Sophia) ambapo mama alinifuata na kuniambia niolewe, nikamwambia mbona mimi ni mdogo? Maana ndiyo kwanza nina umri wa miaka 15!

“Mama aliniambia, kwa kuwa nilifeli shule, basi bora niolewe. Kiukweli nilitamani sana kuendelea na shule, lakini ndiyo hivyo sina baba wa kunisomesha.

 

“Baada ya mama kunilazimisha sana, sikuwa na namna hivyo nilikubali niolewe kama unavyoniona (akionesha mikononi, miguuni na kifuani) nina rangi (piko) baada ya kufungishwa ndoa na Hassani iliyofanyika Februari Mosi.

“Baada ya ndoa, kweli nilikwenda kwa mume wangu kule Mawenzi (kijiji kingine). Nilipofika kwake nilikuta chumba cheupe, akiwa hana kitu isipokuwa godoro tu la sufi na kitanda cha futi nne.

“Jambo lingine ni kwamba simjui mwanaume maana tangu nizaliwe sijawahi kushiriki tendo la ndoa na nilishajiwekea nadhiri kuwa, atakayenioa ndiye atakayeniingiza kwenye ulimwengu wa mapenzi.

 

“Sasa baada ya kukuta hali hiyo (maisha magumu) kwa mume wangu ndipo nikawasiliana na mama yangu ambaye alinikubalia kuondoka kwa Hassani kwa maelezo kuwa alikuwa hajajipanga kuoa na kwamba kulikuwa na maneno mengi juu ya mimi kuolewa naye alihofia kukamatwa na Rais Magufuli kutokana na umri wangu.

“Usiku alipotaka nimpe penzi, nilimdanganya ninaumwa na kwamba nipo kwenye siku zangu. Kulipokucha nilimvizia amekwenda kazini, nami nikabeba vitu vyangu nilivyotunzwa kwenye harusi nikarudi kwa mama yangu.

 

b

 

“Nilishangaa kumuona Hassani hapa akidai nirudi nyumbani kwake au arudishiwe gharama zake shilingi laki tisa na mimi sina hizo pesa. Nimemwambia kama akiendelea kuning’ang’ania nitakwenda polisi kwani umri wangu ni mdogo na nilikubali kuolewa kwa sababu ya mama yangu, lakini na yeye (mama) anahofia.”

Alipoulizwa alipo baba yake, Shani alisema kuwa, mama yake hakuwahi kumuonesha baba yake isipokuwa anasikia ni Mpemba aliyeko jijini Dar ambaye ni dereva wa magari makubwa.

 

 BWANA HARUSI

Muoaji alipohojiwa juu ya tukio hilo alisema: “Hapa siondoki hadi nipewe mke wangu au gharama zangu shilingi laki tisa, mke amenitoroka hata hajamaliza siku saba, amekaa kwenye ndoa kwa saa sita tu.”

Alipoulizwa kwa nini alimuoa mtoto wa umri wa miaka 15 wakati ni kinyume cha sheria za nchi alisema:

“Mimi sijui, lakini dini yangu (Uislam) inaruhusu kuoa mwanamke mwenye umri wa miaka 14 na kuendelea.”

 

MAMA SHANI SASA

Naye Sophia (Mama Shani) alipobanwa na gazeti hili juu ya kitendo chake cha kumuozesha mwanaye akiwa na umri mdogo alijitetea: “Mwanangu nimemzaa mwaka 2,000, ninachojua kwa sasa ametimiza umri wa miaka 18…”

Kufuatia mvutano huo, mwandishi wetu alitaka kujua hatma ya jambo hilo, lakini aliona hakuna mwelekeo hivyo akageuka msuluhishi, jambo ambalo lilitaka kushindikana.

Bi. Sophia (Mama Shani).

 

MWENYEKITI WA MTAA

Hata hivyo, binti huyo alilipeleka suala hilo kwa mwenyekiti wa mtaa ambako huko mwandishi wetu aliacha likishughulikiwa.

 

SHERIA INASEMAJE?

Kufuatia utata huo wa umri wa binti kuolewa, gazeti hili lilizungumza na Mwanafunzi wa Shule Kuu ya Sheria jijini Dar, Innocent Simon juu ya sheria ya ndoa ambapo alikuwa na haya ya kusema:

“Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inatoa ruhusa kwa mwanamke kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 ila ni kwa ruhusa ya mahakama.

“Kisheria siyo sawa, Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inasema ni ruksa kuanzia miaka 14, lakini wadau na wanaharakati wa haki za wanawake wanapigania ibadilishwe,” alisema mwanasheria huyo na kuongeza:

 

“Vipengele vinavyopingwa katika sheria hiyo ni kifungu cha 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa (CAP 29 R.E 2002), sheria inayotoa mwanya kwa mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 14 kwa kibali cha mahakama na miaka 15 kwa ridhaa ya wazazi ambayo ni kinyume na Ibara ya 13, 12 na 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

STORI: Dustan Shekidele, Global Publishers | MOROGORO

 

LIVE: RC MAKONDA AKISIKILIZA KERO ZA WANANCHI WA DAR

Comments are closed.