The House of Favourite Newspapers

SIMANZI! MUME AMUUA MKEWE GESTI

SIMANZI! Mfanyabiasha wa matairi eneo la Temeke Chang’ombe jijini Dar, Mussa Kalavya anashikiliwa na jeshi la polisi akiwa hoi Hospitali ya Temeke, baada ya kudaiwa kumuua mkewe, Claudia Mengere (pichani) kwa kumchoma na bisibisi kichwani na mbavuni kisha naye kujijeruhi kwa kifaa hicho, Risasi Jumamosi lina habari nzima ya kusikitisha.  

 

Kichocheo cha mauaji kinatajwa kuwa ni wivu wa mapenzi ambao katika siku za hivi karibuni umegeuka kuwa janga kwa wapenzi wengi.

Chanzo cha habari kilidai kuwa awali wawili hao waliishi raha mustarehe, lakini mambo ya kimaisha yalipoyumba viashiria vya kutoelewana vilianza kujitokeza.

“Machi mwaka huu mume alimshauri mkewe waende Tunduma mkoani Songwe alikozaliwa ili wakajipange upya kimaisha,” chanzo kilisema.

 

MWAKA WA HASARA HASARA

Mwaka wa hasara ni hasara wakiwa Tunduma inadaiwa mambo yalizidi kuwa mabaya zaidi baada ya mwanaume huyo kufungua duka ambalo baadaye wezi walilivunja usiku na kuiba kila kitu jambo linalodaiwa kumpotezea mwanaume huyo mwelekeo.

Kutokana na balaa hilo mwanamke alimshauri mumewe arejee Dar akiamini kuwa angepata lau kazi ndogondogo za kumpatia kipato cha kuweza kujikimu kimaisha na watoto wakati mumewe akiendelea kutafakari maisha huko Tunduma.

Mungu alikuwa nyuma ya Claudia ombi lake mumewe alilikubali; alipofika Dar alitafuta kibarua kwenye kampuni moja (jina kapuni) akapata na kuanza kuendesha maisha yake huku mume naye akichakarika kivyake huko Tunduma.

 

MTU CHAKE

Maisha yakiwa yanaendelea hivyo imedaiwa mume alianza kufanya ‘upekepeke’ kuhusu mwenendo wa mkewe, pengine kuna jambo alisikia au alikuwa akitumikia hofu yake mwenyewe kutokana na kuishi mbali na mkewe.

Siku zilivyozidi kukatika Mussa akaingiwa na wazo la kuja Dar kumjulia hali mkewe ambapo alimpigia simu mwandani wake na kumwambia nia yake hiyo. “Mwishoni mwa wiki iliyopita alimpigia simu mkewe na kumwambia kuwa atakuja Dar Jumanne, lakini cha ajabu akafika Jumatatu,” chanzo kilisema.

AMUITIA GESTI

Baada ya kutua Dar alimshtukiza mkewe na kumpigia simu na kumwambia alikuwa amefika na hivyo alimtaka aende kwenye Gesti iitwayo West London iliyopo Yombo Buza jijini Dar wakalale.

Kwa kuwa huyo alikuwa ni mumewe hivyo Claudia hakuwa na cha kupinga; alikwenda na kuwa na mumewe usiku mzima huku madai ya mume kumtuhumu mkewe kuwa msaliti yakitajwa.

Mhudumu mmoja wa gesti hiyo aliliambia Risasi Jumamosi kwa siri kuwa Jumanne majira ya saa 5 asubuhi walisikia vurugu chumbani alikokuwa amelala Claudia na mumewe; walipojaribu kuingia ndani walishindwa kutokana na mlango kuwa umefungwa.

 

“Tulipoona hali inatisha ikabidi tupige simu polisi, walipofika wakavunja mlango walipoingia wakamkuta Claudia ameshapoteza fahamu na mumewe akitapatapa pembeni yake huku akiwa amejichoma bisibisi tumboni na pembeni yake kukiwa na nyundo na kisu.

 

MDOGO WA MAREHEMU ASIMULIA

Akiongea na mwandishi wetu mdogo wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Jackline David, alisema; “Dada alipotoka Tunduma na kuja Dar kujaribu tena maisha kwa kuwa hakuwa na chumba hivyo nilikuwa nikiishi naye kwangu mpaka siku aliyoitwa na mumewe kumbe alikuwa akienda kuuawa.

“Mumewe alinipigia simu na kuniambia shemeji nitakuja Dar, Jumanne lakini ghafla alitushtukiza Jumatatu. “Dada alipopigiwa simu na kuitwa alisita sana kwenda na kuniambia hataki kwenda kwa kuwa mumewe amebadilika, amekuwa na tabia za kumpiga mara kwa mara kutokana masuala ya wivu.

 

“Alienda kwa shemeji akiwa shingo upande lakini alipofika niliongea naye kwenye simu na kisha tukachati lakini yaliyotokea asubuhi yake ndiyo hayo yaliyotokea sasa sijui kilitokea nini wakiwa hapo gesti,” alimaliza kusema Jackline.

STORI: Richard Bukos, Risasi Jumamosi

Comments are closed.