The House of Favourite Newspapers

Simba Haikamatiki Yaipiga Yanga, African Lyon na Lipuli

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba, wameendelea na kasi yao ya ushindi baada ya jana kuwafunga Lipuli FC ya mkoani Iringa mabao 3-1.

Kikosi cha Yanga.

Huo ni ushindi wa tano mfululizo wa ligi walioupata Simba tangu waanze kucheza mechi zao za viporo. Ilianza kwa kuifunga Mwadui mabao 3-0, ikaichapa Yanga bao 1-0, African Lyon ikafungwa 3-0, Azam FC nayo ikaambulia kichapo cha mabao 3-0, kabla ya jana Lipuli nayo kufungwa.

 

Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi 48 katika msimamo wa ligi wakibakiwa na mechi sita kuwa michezo sawa na Yanga.

Kikosi cha timu ya Simba SC

Hii ni mara ya kwanza kwa Simba kuifunga Lipuli kwani kabla ya mchezo wa jana, timu hizo zilikutana mara tatu kwenye ligi na kutoka sare zote.

 

Katika mchezo huo wa jana uliochezwa kwenye Uwanja wa Samora mkoani Iringa, Simba ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya tano kupitia kwa Mzambia, Clatous Chama aliyepokea pasi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

 

Simba baada ya kupata bao hilo, Lipuli waliongeza kasi ya ushambuliaji na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 18 kupitia kwa Paul Nonga.

 

Dakika ya 43, Chama aliifungia Simba bao la pili kwa faulo ya moja kwa moja nje kidogo ya eneo la 18. Timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa mabao 2-1.

 

Baadaye dakika ya 58, Mnyarwanda, Meddie Kagere aliifungia Simba bao la tatu baada ya kumchambua kipa wa Lipuli, Mohammed Yusuph.

 

Wakati pambano hilo likiendelea, beki wa Lipuli, Paul Ngalema alipewa kadi nyekundu baada ya kumpiga kiwiko, John Bocco.

 

Bao alilofunga Kagere jana lilimfanya afikishe 12 sawa na Heritier Makambo wa Yanga na Salim Aiyee wa Mwadui, huku Simba ikiwa imefunga jumla ya mabao tisa katika mechi tatu mfululizo.

 

Comments are closed.