The House of Favourite Newspapers

Simba Ikishinda, Yanga Ndiyo Basi Tena

STORI: Said Ally na Omary Mdose | CHAMPIONI | DAR ES SALAAM

SIRIASI! Simba imesema ikishinda mechi yao ya leo Jumamosi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Prisons na kufikisha pointi 51, Yanga ndiyo basi tena iandike imeumia katika mbio zao za kutwaa ubingwa.

Benchi la Ufundi la Simba linaloongozwa na Kocha Joseph Omog raia wa Cameroon, limetamba kuwa, wakiifunga Prisons pia watahakikisha wanaifunga Yanga, Februari 25, mwaka huu na kumaliza mchezo.

Wakati leo Jumamosi Simba inacheza na Prisons kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Yanga inayoongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 49 yenyewe imeenda Comoro na kesho inacheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Ngaya Club de Mbe.

Omog ameliambia Championi Jumamosi kuwa, ni lazima wapate pointi tatu kwenye mechi ya leo dhidi ya Prisons, kisha wamalizane na Yanga katika kujihakikishia nafasi ya kuchukua ubingwa wa ligi msimu huu.

“Ni lazima tupate ushindi dhidi ya Prisons na Yanga kwa ajili ya kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa kwa sababu mechi hizi mbili zina umuhimu mkubwa kwetu na kama tukipoteza tunaweza kujiweka katika eneo baya.

“Hatutakiwi kukosa hata pointi moja kwa sababu kama tukiwafunga Prisons basi tutarejea kileleni na tukija kuwafunga Yanga ndiyo tutazidi kujikita kileleni zaidi hata kama wao wakishinda mchezo mechi zao.

“Ingawa malengo yetu ni kupata pointi kila mechi lakini kwa sasa tumezitolea macho pointi za mechi hizi zilizo karibu na tukifanikiwa kuzipata basi ndiyo itakuwa safari ya ubingwa imeiva,” alisema Omog.

Naye Kocha wa Prisons, Mohammed Abdallah, akiuzungumzia mchezo huo wa leo alisema: “Tumejipanga vizuri kukabiliana na Simba, matokeo mazuri ya mchezo wa awali yanatufanya tujiamini zaidi.

“Licha ya wao kuwa juu yetu, lakini hilo halizuii sisi kuwafunga, tulivyowafanya kwenye mchezo wa kwanza ndivyo hivyohivyo tutakavyowafanya kwenye mchezo huu wa pili.”

Siimba ina pointi 48 katika nafasi ya pili lakini Prisons ipo nafasi ya sita na 29. Katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Prisons ilishinda mabao 2-1.

Save

Save

Comments are closed.