The House of Favourite Newspapers

Simba Nini Kinakwamisha Bunju Complex?

0

KUNA wakati mchakato wa ujenzi wa uwanja wa Klabu ya Simba uliopo Bunju ujulikanao kama Bunju Complex ulipamba moto na tukaambiwa mpaka nyasi bandia kwa ajili ya uwanja huo zimewasili, lakini ghafla hatusikii kinachoendelea.

 

Viongozi wa klabu hiyo kongwe hata ukiwauliza nini kinaendelea kuhusu uwanja huo wanaonekana kurushiana mpira kiasi cha kukosa maelezo ya moja kwa moja.

Ujenzi wa uwanja huo ilikuwa ni sehemu ya ukombozi ya klabu hiyo ambayo tangu ianzishwe kwake haina uwanja wake wa ku­fanyia mazoezi kitu ambacho ni aibu kabisa.

 

Mtu anaweza asiamini kuona klabu kubwa kama Simba au hata watani wao wa jadi Yanga kuwa kwa miaka yao yote na mashabiki lukuki ilionao pamoja na wana­chama wao lakini havina viwanja vyao hata mazoezi.

 

Bunju Complex ilikuwa ni ukom­bozi mkubwa kwa Simba na ndiyo maana wanachama na mashabiki walipokea kwa shangwe taarifa kuwa wanaanza ujenzi.

 

Ndiyo maana wanachama wa Simba walijitolea wakaenda ku­fyeka wengine wakasema watatoa saruji kwa ajili ya ujenzi, yote ni kuona wanafanikisha ujenzi huo.

Lakini matokeo yake kumeanza danadana na hakuna kinachoe­lezwa chochote kuhusu uwanja huo.

Pamoja na Klabu ya Simba kuele­kea hivi sasa katika mchakato wa kumsaka yule atakayeendesha klabu hiyo katika mfumo wa kisasa, suala la Bunju Complex lilipaswa kuangaliwa kwa kina.

 

Suala la viwanja vya klabu hizi lili­paswa kuwa histo­ria kama mchakato huu wangeufanya siku nyingi. Leo hii klabu ndogo kama Azam ambayo hai­na hata miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, inamiliki uwanja wake tena wa kisasa kabisa.

Klabu hizi leo zingekuwa zina­zungumzia kuwa na vitu vya kitega uchumi na sio viwanja, lakini kuto­kana na ubabaishaji wa viongozi wake, bado zimebaki kuwa maskini wa kutupwa.

 

Leo tembelea katika majengo yao hutoamini kabisa, kama majengo tu ya klabu za hawa jamaa wanashindwa kuyatunza sembuse wataweza kuwa na viwanja?

Wana Simba mnapaswa kuuliza Bunju Complex imefikia wapi? Nini kinakwamisha? Au ilikuwa ni siasa tu wakati ule kusema tunajenga uwanja Bunju?

Nafikiri umefika muda sasa wa wa­nachama wa Simba kuanza kuhoji kuhusu mambo haya am­bayo hayaleti sura nzuri kwenye klabu yao.

 

Siyo kweli kwamba klabu hizi zinashindwa kumiliki viwanja kwa sasa, bali hii inatokea kwa kuwa wana­chama wamekuwa hawa­hoji kuhusu maendeleo ya uwanja huo wa Bunju.

Ufike muda sasa klabu hizo zipambane na vitu vingine na kuachana na suala la uwanja ambalo naamini kuwa lipo ndani ya uwezo wao na kama wanachama watakubali kuwaunga mkono na kupambana pamoja.

 

 

Leave A Reply