The House of Favourite Newspapers

Simba Queens Kutangaza Ubingwa na Mechi Mkononi

0

KLABU ya Simba Queens huenda ikatangazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu endapo itaibuka na ushindi mbele ya Baobab Queens, mchezo utakaochezwa keshokutwa Jumatano katika dimba la Uhuru, Dar.

 

Simba Queens wana pointi 50 kileleni na wamewaacha JKT Queens kwa pointi saba, wao wakiwa nafasi ya pili na pointi zao 43.

 

Simba Queens walio chini ya straika wa zamani wa Simba, Mussa Hassan Mgosi, wamebakiza mchezo mmoja wa nyumbani, kisha baada ya hapo watapaa hadi Kanda ya Ziwa pale jijini Mwanza kucheza michezo miwili dhidi ya Alliance Girls na TSC Queens na hiyo ndiyo itakuwa michezo yao ya mwisho kwa msimu huu.

 

Wikiendi iliyopita, Simba walivuna ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Tanzanite. Matokeo mengine ilikuwa ni Yanga Princess 4-1 TSC Queens, bingwa mtetezi JKT Queens alimchapa Alliance Girls 3-2, Ruvuma Queens 2-0 Kigoma Sisterz, Marsh Queens 1-0 Panama Girls na Mlandizi Queens waliwachapa Baobab Queens kwa mabao 2-1.

 

Msimamo wa ligi hiyo yenye timu 12 unaongozwa na Simba Queens kwa pointi 50, JKT Queens pointi 43 sawa na Alliance Girls waliopo nafasi ya tatu na ya nne wapo Ruvuma Queens na pointi 42, nafasi ya tano ni Yanga Princess wenye alama 33.

 

Wakifuatiwa na Mlandizi Queens pointi 29, Kigoma Sisterz alama 24. Baobab Queens pointi 22, Marsh Queens pointi 15, Tanzanite Queens alama 13.

 

Huku walio kwenye janga la kushuka daraja ni TSC Queens wenye pointi 12 nafasi ya 11 na Panama Girls nafasi ya 12 na pointi zao nne tu na timu zote zimecheza michezo 19.

Issa Liponda, Dar es Salaam

Leave A Reply