The House of Favourite Newspapers

Simba: Tumefuata Ushindi Congo

SIMBA imesema inafahamu ugumu wa mechi ya leo dhidi ya AS Vita ya nchini hapa lakini wao wameweka wazi mapema kwamba wamefuata ushindi na siyo sare. Kauli hiyo imetolewa na Mtendaji Mkuu wa Simba (C.E.O), Crescensius Magori pamoja na Kocha Patrick Aussem, muda mfupi baada ya kutua jijini hapa kwa ajili ya mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mchezo utakaopigwa leo kwenye Uwanja wa Martyrs de la Pentecôte uliopo Kinshasa, DRC Congo.

 

Simba ilitua juzi mchana ikiwa na msafara wa wachezaji 19 na kufikia kwenye hoteli ya kifahari kabla ya jioni kufanya mazoezi ya mwisho katika kujiandaa na mchezo huo unaotarajiwa kuwa mgumu baada ya AS Vita kupoteza mchezo uliopita kwa kufungwa mabao 2-0 na Al Ahly ya Misri.

 

Magori ameliambia Championi Jumamosi kuwa: “Hatujaja hapa Kinshasa kujilinda kwa ajili ya kutafuta sare, tumekuja kutafuta ushindi wa aina yoyote ili kuhakikisha tunajiwekea mazingira mazuri ya kufuzu hatua inayofuata ya michuano hii. “Lakini nipongeze pia mapokezi mazuri hapa tangu tuliposhuka kwenye ndege na kupokelewa na balozi wa Tanzania wa hapa Congo pamoja na Watanzania waishio hapa.

 

“Kidogo tulipata matatizo ya mizigo yetu katika ndege lakini tunashukuru tumeipata, maandalizi yanakwenda vizuri kabisa kwa ajili ya mchezo wetu huo ambao tunahitaji ushindi pekee.” Naye aussems alisema: “Itakuwa mechi ngumu lakini hatujaja hapa kuzuia, tumekuja hapa kujaribu kutengeneza nafasi kama ilivyo kwa michezo yetu mingine na kujaribu kufunga.”

WAWA ATEMA CHECHE

Wakati mashabiki wengi wa Tanzania ambao wataungana kushabikia Simba leo kuonekana kuwa na hofu, beki kisiki Pascal Wawa raia wa Ivory Coast ameweka wazi kwamba hakuna cha kuogopa kwani kila kitu kipo sawa. “Nimewasoma na kujua mbinu zao kupitia video, mimi kama beki nahitaji kufanya kazi yangu ipasavyo katika mechi hiyo ili niweze kufanikiwa kufanya vizuri katika mchezo
huo ambao naamini utakuwa mgumu, tunakwenda kupambana ili tushinde,” alisema Wawa.

 

NIYONZIMA AANDALIWA

Baada ya kutua jijini hapa, Kocha wa Simba, Patrick Aussems alionekana akizungumza mara kwa mara na kiungo Haruna Niyonzima akimuelekeza vitu kadhaa jambo ambalo inaaminika anaweza kucheza kwa mara ya kwanza mechi za kimataifa na kikosi hicho.

 

Niyonzima ambaye alijiunga na Simba uliopita akitokea Yanga alijikuta akiwa kwenye wakati mgumu kwa muda mrefu kutokana na matatizo yake na uongozi pamoja na majeraha hivyo kukaa nje kwa muda mrefu. Hata hivyo, hivi karibuni alionekana kurejea tena kwenye kiwango chake baada ya kuonyesha uwezo mzuri kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyomalizika wiki iliyopita.

 

“Kwa jinsi hali ya mambo inavyoonekana kuna uwezekano mkubwa Niyonzima akacheza kwa mara ya kwanza mechi hiyo, bado sijajua kama ataanza au ataingia kipindi cha pili lakini ana nafasi kubwa ya kucheza.

 

“Kocha amekuwa akifanya naye mazungumzo mara kwa mara kabla na baada ya mazoezi tangu tulipokuwa Dar es Salamu na hata tulipofika huku wakipeana maelekezo kwa Lugha ya Kifaransa na kuna wakati kocha amekuwa akimsifia sana kuhusiana na kiwango chake kuongezeka,” alisema mmoja wa watu wa benchi la ufundi.

 

 

Alipofuatwa Niyonzima alisema: “Nashukuru Mungu kila kitu kinakwenda sawa, lakini suala la kucheza ni kocha ndiye anayeamua kutokana kiwango anachoonyesha mchezaji pale mazoezini.”

Comments are closed.