The House of Favourite Newspapers

Simba Vs Azam, Sura Mpya Kibao leo Uwanja wa Taifa

Mchezo huo namba 67 wa Ligi Kuu Bara, ndiyo utakuwa mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana katika ligi msimu huu. Awali timu hizo zilikutana kwenye Ngao ya Jamii wakati wa ufunguzi wa msimu huu, mchezo uliochezwa Agosti 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 4-2.

 

Kuelekea mchezo huo, kuna wachezaji wapya ambao walisajiliwa na timu hizo msimu huu na watakutana kwa mara ya kwanza kwenye mchezo wa ligi.

 

Licha ya kwamba walikutana kwenye Ngao ya Jamii, lakini katika ligi hii ni mara ya kwanza. SIMBA Simba msimu huu walifanya usajili wa wachezaji wengi ambao tayari takribani wote wameshawatumia kwenye michezo mbalimbali ya kirafiki, Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Wachezaji hao, wapo ambao ni mara yao ya kwanza kabisa kucheza Ligi Kuu Bara na wengine wapo kitambo ligi kuu wakizitumikia timu zingine ambao ni:

MIRAJI ATHUMAN

Amesajiliwa kutoka Lipuli FC na tayari usajili wake ndani ya Simba umeleta matunda makubwa hasa katika michezo ya ligi kuu. Katika mechi nne za Simba, amefunga mabao matatu. Amekuwa akitumika zaidi kama mchezaji wa akiba ambaye huingia baadaye, akiingia analeta changamoto kwa wapinzani. Uwezo wake umemfanya kwa mwezi Septemba kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi wa Ligi Kuu Bara.

 

 

SHARAF SHIBOUB Kabla ya ligi kuanza, kiungo huyo Msudan alionyesha uwezo kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam na kufunga mabao mawili. Azam wanamtambua vizuri sana kutokana na siku hiyo kuwa mwiba kwao. Hii ni mara ya kwanza anacheza na Azam katika ligi kuu, tusubiri tuone kama moto wake ule atauendeleza.

 

IBRAHIM AJIBU Huyu siyo mgeni wa Ligi ya Bongo, lakini msimu huu atakutana na Azam kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na Simba akitokea Yanga.

GERSON FRAGA Ni raia wa Brazil aliyejiunga na Simba msimu huu akitokea nchini India. Katika mechi nne ambazo Simba imecheza, amefanikiwa kucheza zote.

 

FRANCIS KAHATA Hakuna asiyemjua uwezo wake japo Azam nao wanamjua kwa kazi aliyoionyesha kwenye Ngao ya Jamii. Sasa wanaenda kukutana kwa mara ya kwanza kwenye ligi, je ataweza kuifunga tena kama alivyofanya kwenye Ngao ya Jamii?

 

GADIEL MICHAEL Misimu mitatu nyuma, aliachana na Azam na kutimkia Yanga. Msimu huu ametua Simba na kwa mara ya kwanza anakwenda kukutana na waajiri wake wa zamani. Wachezaji wengine wapya wa Simba ni Kennedy Juma, Tairone Santos, Wilker da Silver, Haruna Shamte na Deo Kanda.

 

AZAM FC Wao hawakufanya usajili wa wachezaji wengi kama ilivyo kwa Simba. Wachezaji wao wapya ni:

RICHARD DJODI Ni raia wa Ivory Coast ambaye tayari ameonyesha uwezo mkubwa kwa baadhi ya michezo ya ligi pamoja na ile ya kimataifa ambayo Azam ilishiriki Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya kutolewa. Kwenye ligi kuu, itakuwa ni mara ya kwanza anakutana na Simba.

 

IDD SELEMAN Anafahamika kama Nado na uwezo wake siyo wa kuubeza jambo ambalo Simba wanatakiwa kulifahamu wanapokwenda kukabiliana naye. Msimu uliopita alikuwa Mbeya City na tangu atue Azam FC, amekuwa msaada mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

 

KASSIM KHAMISI Msimu uliopita akiwa Kagera Sugar aliifanyia Simba kitu mbaya, safari hii anaenda kukutana na Simba kwa mara ya kwanza kwenye ligi akiwa na jezi za Azam.
Tusubiri tuuone moto wake.

 

SELEMAN NDIKUMANA Amesajiliwa msimu huu, lakini uwanjani amekuwa haonekani mara kwa mara, huenda akapangwa kwenye mechi dhidi ya Simba. Si mgeni na Ligi ya Tanzania kwani miaka ya nyuma aliwahi kucheza hapa nchini akiitumikia Simba kabla ya kutimka na sasa yupo Azam FC.

Stori na Martha Mboma

Comments are closed.