The House of Favourite Newspapers

Simba Wabishi Aisee

0

LICHA ya kupoteza kwa kufungwa mabao 2-1 wakiwa ugenini mbele ya Red Arrows, wawakilishi wa Simba kwenye mashindano ya kimataifa wameweza kutinga hatua ya makundi katika Kombe la Shirikisho Afrika kwa jumla ya mabao 4-2.

Ni mabao ya Erick Banda dakika ya 44 kwa shuti kali akiwa ndani ya 18 baada ya mabeki wa Simba waliokuwa wakiongozwa na Pascal Wawa kufanya uzembe katika kuokoa mpira huo uliomshinda kipa namba moja Aishi Manula.

Mpaka dakika 45 zinakamilika Uwanja wa Heroes nchini Zambia, Red Arrows walikuwa mbele kwa bao moja ambalo liliwafanya Simba kucheza wakiwa na presha kubwa kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili tena safu ya ulinzi ya Simba haikuwa makini kwenye mipira ya juu ambapo bao la pili lilipatikana dakika ya 46 na kuongeza mzigo kwa Simba katika kujilinda huku wakifanya mashambulizi ya kushtukiza.

Ni Hassan Dilunga kiungo mzawa ambaye alikuwa msumbufu kwenye mchezo huo aliweza kufunga bao la kuongeza nguvu kwa Simba dakika ya 67 baada ya kutumia makosa ya beki wa Red Arrows ambaye alifanya makosa kwenye kuokoa mpira mrefu uliopigwa na Rally Bwalya.

Kiungo wa Simba, Bernard Morrison ambaye alifunga mabao mawili kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa ambapo alifunga mabao mawili na kutoa pasi moja ya bao kwa Meddie Kagere alibanwa mbavu na wachezaji wa Red Arrows ambao walikuwa wanakula naye sahani moja kila hatua jambo lililofanya ashindwe kuonyesha makeke yake.

Hata hivyo, aliweza kupiga kona moja ambayo ililenga lango lakini uzembe wa wachezaji wa Simba walishindwa kuizamisha nyavuni kwa kuwa kipa wa Red Arrows alitema mpira huo.

Nguvu kubwa ilitumika kwa Simba hasa kipindi cha pili kwenye kujilinda ambapo Pablo Franco aliweza kuingiza mabeki wake wawili waliokuwa benchi ikiwa ni pamoja na Shomari Kapombe na Joash Onyango ambao walikwenda kuungana na Henock Inonga, Pascal Wawa, Mohamed Hussein pamoja na Israel Patrick.

Pongezi kwa Manula ambaye hakuwa na chaguo la kufanya pale ambapo wachezaji wake wanafanya makosa kwa kuweza kuokoa michomo yote iliyokuwa ni moto mwanzo mwisho.

Aliweza kuokoa jumla ya mashuti 16 ambayo yalipigwa kuelekea kwenye lango lake kipindi cha kwanza ilikuwa ni mashuti nane na kipindi cha pili ilikuwa ni mashuti nane.

Hii imekuwa timu ya tatu kwa Tanzania kufuzu kwa hatua ya makundi baada ya Yanga na Namungo FC ya mkoani Lindi.

MWANDISHI WETU, Dar es Salaam

Leave A Reply