The House of Favourite Newspapers

Simba Waenda Stars, Warudi Kucheza Mechi

IMEBAINIKA kuwa baada ya kikosi cha Taifa Stars kuingia kambini juzi Jumatatu, wachezaji ambao wana mechi za ligi kuu, wataruhusiwa kwenda kucheza mechi kisha kurejea tena kwenye kambi hiyo.

 

Stars ipo kambini kwa sasa kwa ajili ya maandalizi ya mch­ezo wao dhidi ya Cape Verde ambao unatarajiwa kupigwa Oktoba 12, mwaka huu nchini humo.

 

Stars itacheza mchezo huo kisha ule wa marudiano ambao utapigwa Oktoba 16, mwaka huu hapa nchini.

Kambi hiyo ilianza rasmi siku ya Jumatatu ambapo mpaka jana Jumanne mchana wachezaji ambao walikuwa kambini ni 12 kati ya 30 ambao waliitwa na kocha Em­manuel Amunike.

 

Akizungumza na Cham­pioni Jumatano, Meneja wa Stars, Danny Msangi, alisema kuwa wachezaji ambao watakuwa na mechi, wataruhusiwa kutoka kam­bini kisha kurejea baada ya majukumu hayo.

 

“Wachezaji wapo kambini hapa lakini wale ambao wana michezo kama Simba, Yanga na Azam tutawaruhusu kwenda kwenye mechi zao za ligi siku moja kabla kisha watarejea tena kuendelea na kambi kama kawaida.

 

“Pia kuna wachezaji wale wa nje ambao hawatakuja hapa Tanzania kama Simon Msuva, Himid Mao, Mbwana Samatta, Shaban Chilunda na Farid Mussa, hao wengine tutatoa taarifa yao.

 

“Na kwa sasa maandalizi yanaendelea kama kawaida, mazoezi yanafanyika kwa ajili ya kuandaa timu kwa wale ambao tayari wameripoti kambini,” alisema Msangi.

Comments are closed.