The House of Favourite Newspapers

Simba wasepa zao Mwanza, Kichuya, Mavugo Wabaki Dar

Sweetbert Lukonge na Said Ally |CHAMPIONI| Dar es Salaam

ILE safari ya kikosi cha Simba ya Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kusaka pointi tisa katika mechi zake tatu za Ligi Kuu Bara itakazocheza huko dhidi ya Kagera Sugar, Toto Africans na Mbao FC hatimaye imetimia na jana alfajiri kikosi kimeondoka jijini Dar es Salaam.

Kikosi hicho kimeondoka kwa basi na kwenda mkoani Kagera ambako Jumapili ijayo ya Aprili 2 kitapambana na Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kabla ya kusafiri tena mpaka jijini Mwanza kucheza na Mbao FC na baadaye Toto Africans.

Hata hivyo, kikosi hicho kimeondoka bila ya kuwa na baadhi ya nyota wake wa kutumainiwa kutokana na kukabiliwa na majukumu ya kitaifa ambapo wamebakia jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaoikutanisha Taifa Stars na Burundi kesho Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa.

Wachezaji hao ni nahodha wa timu hiyo, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin, Said Ndemla, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda na Ibrahim Ajibu ambao wapo na kikosi cha Taifa Stars lakini pia Laudit Mavugo ambaye uongozi wa Shirikisho la Soka Burundi, limemtaka asiondoke Dar ili aweze kuitumikia timu yake ya taifa katika mechi hiyo ya kirafiki.

Akizungumza ba Championi Jumatatu, Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema kuwa wachezaji hao watajiunga na timu hiyo haraka iwezekanavyo mara tu watakapomaliza majukumu yao ya kitaifa.

“Hata hivyo, ukiachana na hilo pia napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza beki wetu Juuko Murshid kwani amerejea nchini jana (juzi) baada ya kumaliza jukumu lake la kuitumikia Uganda katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa na leo hii (jana) tupo naye safarini.

“Kutokana na hali hiyo ni matumaini yetu kuwa kikosi chetu kitakuwa sawa na tutafanya vizuri katika mechi zetu hizo kwani mpaka sasa majeruhi ni mmoja tu ambaye ni Method Mwanjale na tumemuacha Dar es Salaam,” alisema Mayanja.

Mayanja aliongeza: “Hakuna wa kutuzuia kupata pointi katika mechi hizo kwanza hilo wanatakiwa walitambue hata wajiandae kwa namna gani kwa sababu tunataka kumaliza ligi kama ambavyo tulivyoanza mwanzoni.

“Lakini kingine ambacho kinatupa jeuri ya kuona tuna kila sababu ya kutamba huko ni uimara wa kikosi tulichonacho tofauti kabisa na wao na sasa amebaki mchezaji mmoja pekee Method Mwanjale ambaye ndiye mgonjwa hivyo tukienda huko tunaenda tukiwa kamili.”

Comments are closed.