The House of Favourite Newspapers

Simba yampandisha ndege… Kamusoko

0

Wilbert Molandi,
Dar es Salaam
IMEELEZWA kuwa kama siyo mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga, basi kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko asingepanda ndege kwenda nchini Mauritius.
Mzimbabwe huyo, yupo nje ya uwanja kwa muda wa wiki akiuguza jeraha la kifundo cha mguu ‘enka’ aliyoyapata mara baada ya mechi ya Coastal Union iliyochezwa Mkwakwani, Tanga, hivi karibuni.
Kiungo huyo kutokana na majeraha hayo ya enka, amelazimika akose michezo miwili ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons na JKT Ruvu.
Kamusoko anatarajiwa kukosekana kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius wikiendi hii kutokana na jeraha hilo lakini kwa mujibu wa uongozi wa Yanga, atalazimika kwenda na timu ili aungane nayo kwenye kambi ya kujiandaa na pambano la watani, Februari 20.
Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alithibitisha kuwa: “Kamusoko yupo kwenye msafara wa wachezaji 21 watakaokwenda Mauritius kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa sambamba na kambi ya nchini humo tukijiandaa na mechi na Simba.”
Hata hivyo, akizungumza na Championi Jumatano, mara baada ya kumalizika kwa mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika Boko Beach Veterani jana asubuhi, kocha wa timu hiyo, Hans Pluijm, alisema hatima ya Kamusoko kwenda au kutokwenda ilitegemea majibu ya vipimo vya mashine ya CT Scan aliyoifanya kwenye enka ya mguu wake wa kulia jana jioni.
Mholanzi huyo alisema ripoti ya daktari wa timu hiyo ndiyo itatoa majibu kutokana na majeraha yake yaliyomsababishia ashindwe kufanya mazoezi kwa muda wa wiki moja.
“Timu yetu inatarajiwa kuelekea nchini Mauritius kesho (leo) asubuhi, msafara huo unatarajiwa kuwa na wachezaji 21 pekee akiwemo Cannavaro (Nadir Haroub).
“Wakati Cannavaro akiwemo kwenye msafara huo, Kamusoko bado haijajulikana hatima yake ya kwenda au kutokwenda hadi pale tutakapopata majibu ya vipimo vyake atakavyovifanya kwenye mashine ya CT Scan.
“Leo (jana) asubuhi alipelekwa hospitali kwa ajili ya vipimo hivyo kwa ajili ya kujua tatizo zaidi ambalo ninaamini leo (jana) litajulikana baada ya kupimwa na mashine hiyo maalumu,” alisema Pluijm.

Leave A Reply