The House of Favourite Newspapers

Simba Yapangua Fitina, Yagoma Kulala Angola Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika

0
Kikosi cha timu ya Simba.

UONGOZI wa Simba umeendelea kutengua fitina zote walizoandaliwa na wapinzani wao Primeiro De Agosto ya Angola kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo sasa wataondoka nchini Angola mara baada tu ya mchezo wao kumalizika ili kuwahi maandalizi nchini.

 

Kesho Jumamosi Simba wataondoka nchini kwa ndege ya kukodi tayari kwa mchezo huo utakaopigwa Oktoba 9, mwaka huu, katika Uwanja wa De November 11, majira ya saa 10:00 kwa saa za Angola, huku ukitarajiwa kurudiwa Oktoba 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

 

Chanzo chetu kutoka Simba kimelihakikishia Championi Ijumaa kwamba, pamoja na uwepo wa usalama katika msafara wao, bado wamejadiliana kuona timu inarejea muda mfupi tu baada ya mchezo huo, ili wachezaji wapate muda wa kupumzika na kuanza maandalizi kwa ajili ya mchezo wa marudiano.

“Kuna njama za fitina tumezigundua kwa wapinzani wetu hivyo kuepuka hilo ni bora turudi mara tu baada ya mchezo kumalizika, maana jamaa wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanatuvuruga ili tusiweze kusonga mbele, jambo ambalo tayari tumepata taarifa za kina kutoka kwa watu wetu muhimu.

 

“Kwenda na ndege pekee hakukufanyi kuondoa fursa kwa wapinzani wako kukufanyia madhara nje ya uwanja, maana ikumbukwe ile ni nchi yao na jamaa wanatokea jeshini, hivyo kama tukisema tuzubae kule baada ya mchezo itatugharimu kulingana na taarifa za siri tulizopata hivyo tutavunja kila nia yao ovu ili kulinda mipango yetu,” kilisema chanzo hicho.

 

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amethibitisha kuwa: “Ni kweli kwa kuwa tutaondoka na usafiri binafsi ni wazi kabisa kwamba hatutakuwa na muda tena wa kulala kule, japo bado tunaangalia nini kitafaa zaidi.”

KOCHA NABI ANAZUNGUMZA MUDA HUU KUELEKEA MECHI DHIDI YA AL HILAL…

Leave A Reply