The House of Favourite Newspapers

Simba Yawaacha Mastaa Dar

0

IMEFAHAMIKA kuwa kiwango kibovu ndiyo sababu ya mastaa wa Simba kuachwa kwenye msafara wa timu hiyo ulioelekea Pemba, kucheza michuano ya Kombe la Mapinduzi.

 

Viongozi wa Simba wikiendi iliyopita walionekana kukerwa na viwango vya wachezaji wao walivyovionyesha wakati wa mchezo dhidi ya watani wao Yanga.

 

Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, Simba imewaacha Dar wachezaji wote waliocheza katika kikosi cha kwanza, baada ya kikao cha viongozi wa timu hiyo kilichokaa na kufikia maamuzi hayo huku ikiwapeleka wale wa akiba na waliokaa jukwaani kwenye michuano ya Mapinduzi.

 

Mtoa taarifa huyo, alisema kuwa lengo ni kuwaonyesha bila ya wao timu yao ina uwezo wa kupata matokeo mazuri baada ya kukerwa na kiwango kibovu.

Aliongeza kuwa, uongozi wao umepanga pia kufuta ufalme wa baadhi ya wachezaji wanaojiona muhimu katika timu hiyo kwa lengo la kurudisha nidhamu.

 

“Kama unakumbuka baada ya mchezo na Yanga viongozi walikaa kikao vyumbani kwa zaidi ya dakika 30 ni baada ya kukerwa na matokeo ya sare ya mabao 2-2.

“Katika mchezo huo, viongozi walitarajia kuona timu yao ikipata ushindi wa mabao mengi, lakini haikuwa hivyo baada ya kuongoza kwa mabao mawili waliamini wataongeza mengine kabla ya yote mawili kusawazishwa.

 

“Viongozi waliujadili mchezo na kuonekana baadhi ya wachezaji walishindwa kuitumikia timu yao kwa asilimia mia moja, hivyo wakaamua wabaki Dar na kuendelea na mazoezi,”alisema mtoa taarifa huyo.

Simba bado ipo kileleni kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 35 zikiwa ni tisa mbele ya timu inayoshika nafasi ya pili.

Leave A Reply