The House of Favourite Newspapers

Simbachawene Azindua GGM Kili Challenge 2022, Aahidi Ushirikiano

0
Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti – GGML anayesimamia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo akizungumza katika uzinduzi wa harambee hiyo.

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi- Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) George Simbachawene amezindua harambee ya uchangiaji wa Kampeni ya GGM Kili Challenge 2022 na kuahidi Serikali itaendelea kuthamini na kuwezesha jitihada za aina hiyo katika mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi.

 

Kampeni hiyo ya GGM Kili Challenge ilianzishwa mwaka 2002 na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa lengo la kuchangia fedha kwa ajili ya shughuli za udhibiti wa ukimwi, ikiwa na lengo la kukusanya fedha ili kuisaidia serikali ya Tanzania katika jitihada zake kufikia malengo ya sifuri tatu.

 

Malengo ya sifuri tatu yanamaanisha kupunguza kabisa kwa kufikia asilimia sifuri ya maambukizi mapya, sifuri ya unyanyapaa pamoja na sifuri katika vifo vitokanavyo na UKIMWI.

 

GGM Kili Challenge 2022 ina lengo la kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini na kushirikisha wadau kuchangia mwitikio wa  taifa dhidi ya virusi vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI.

 

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika juzi Weruweru wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, Simbachawene ameipongeza GGML ambao ni waanzilishi wa Programu ya ufadhili wa masuala ya VVU na UKIMWI kwa kupanda Mlima Kilimanjaro ambayo inatimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake.

 

Amesema umuhimu wa afya bora kwa wananchi wa Tanzania ni moja ya vipaumbele vya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

 

Amesema kutokana na jitihada hizo za GGML na wadau wengine kiwango cha upimaji wa VVU kimeongezeka kutoka asilimia 61 (ya makadirio ya watu wanaoishi na VVU – WAVIU) mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 81 mwaka 2020;

 

“Hivyo basi, ili kufikia malengo ya sifuri tatu pamoja na mengine katika kuishida vita hii dhidi ya VVU na UKIMWI, kunahitaji nguvu ya pamoja kati ya Serikali na Wadau Wengine, hususan Sekta Binafsi ili kupata rasilimali fedha ya kutosha,” amesema.

 

Aliyekuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo, Waziri wa Nchi- Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) George Simbachawene (kushoto) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai.

Aidha, Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti – GGML anayesimamia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo amesema mwaka huu wameendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, hivyo GGML kwa kushirikiana na TACAIDS zoezi la kupanda mlima limeanza Julai 15 hadi Julai 21 mwaka huu.

 

“Tunawakaribisha sana wadau na makampuni mbalimbali kuchangia na kushiriki katika kampeni hii,” alisema Bw. Shayo.

 

Mmoja wa watoto wanaohudumiwa na Kituo cha Rainbow Center – Moshi, Hosea Patrick ambaye amehitimu kidato cha sita na Waziri Simbachawene kumuahidi kuhakikisha anapata mkopo asilimia 100 kuendelea na masomo ya elimu ya juu. Kituo hicho ni mojawapo ya Asasi zinazofaidika na fedha za mfuko wa GGM Kili challenge.

 

Aidha, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa msaada wake na ushirikiano wa TACAIDS katika kampeni ya Kili Challenge tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002.

 

Takwimu za kitaifa za watu wanaoishi na VVU hujuimuisha hata wale wanaoishi Mkoani Geita, ndio maana tunafanya jitihada za pamoja kutokomeza maambukizi mapya nchi nzima,” aliongeza Bw Shayo.

 

GGM Kili Challenge imepiga hatua kubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002 hadi kufikia kuwa mfuko wa kimataifa, wenye kushirikisha wapanda mlima na waendesha baiskeli zaidi ya 700 kutoka mabara 6 na zaidi ya nchi 20.

 

Mkurugenzi Mkuu TACAIDS, Dk. Leonard Maboko amesema licha ya mafanikio yaliyofikiwa, UKIMWI bado ni tatizo nchini.

 

Amesema takwimu zinaonesha kuwapo kwa ongezeko la maambukizi mapya ya VVU hususan kwa makundi maalum yaliyo katika hatari kubwa ya maambukizi. Hadi kufikia mwaka 2020 idadi ya Watanzania wanaoshi na virusi vya UKIMWI nchini imefikia watu 1,700,000 na Maambukizo mapya kwa mwaka ni watu 68,000.

 

“Makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya VVU ni vijana, wanaotumia madawa ya kulevya, wanaofanya biashara ya ngono, madereva wa malori yaendayo masafa marefu, wafanyakazi wa kwenye mashamba makubwa na jamii za wavuvi na wafanyakazi wa migodini. Makundi haya hatarishi yanahitaji mikakati maalumu ya kuzuia maambukizo mapya ya VVU kwao na kwa jamii kwa ujumla,” alisema Dk. Maboko.

 

Kupitia kampeni ya GGM Kilimanjaro Challenge, taasisi mbalimbali zimenufaika kwa kupata fedha za kutekeleza shughuli za mwitikio wa VVU na UKIMWI nchini. Kwa mfano, mwaka 2020 Mfuko wa Kilimanjaro Challenge ulitoa fedha taslim Milioni 800 za Tanzania kwa taasisi 20 zisizo za kiserikali.

 

Asasi hizo zimetekeleza miradi mbalimbali iliyowalenga vijana, watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, watoto yatima na waliopo kwenye mazingira magumu, na jamii kwa ujumla. Zaidi ya watu 1,000 wamenufaika kutokana na fedha hizo.

 

Wakati Meneja Mwandamizi wa masuala ya ubia kutoka GGML, Manace Ndoroma amesema shughuli za Kili Challenge ziliahirishwa kwa miaka miwili kutokana na ujio wa janga la UVIKO 19, mpaka pale ziliporuhusiwa tena na mamlaka husika mwezi April mwaka huu.

Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti – GGML anayesimamia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo (kulia) akiwa na Meneja Mwandamizi wa masuala ya ubia kutoka GGML, Manace Ndoroma (kushoto) katika uzinduzi wa harambee ya Kampeni ya GGM Kili Challenge kwa mwaka 2022.

 

“Kwa sababu hiyo, maandalizi rasmi yalianza mwezi huo wa Aprili na ninayo furaha kukujulisha kwamba mbele yako kuna jumla ya washiriki 52, ikijumuisha wapanda mlima 24 na waendesha baiskeli 28. Ukilinganisha na jumla ya washiriki 55 kwa mwaka 2019, kuna upungufu wa watu 3 tu. Wote wametimiza vigezo vya ushiriki vinavyojumuisha vipimo vya afya na maandalizi ya kimwili (mazoezi),” amesema.

Leave A Reply