The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya AY: Ashinda medali za kuigiza na tenisi akiwa shuleni

0

AY (2)MPENDWA msomaji wa simulizi hii tamu, wiki iliyopita tuliishia pale AY alipoamua kufyeka uwanja wa mpira nyuma ya nyumba yao na kuanzisha timu aliyoiita Barcelona kwa mapenzi aliyonayo kwa timu hiyo ya Hispania tangu mwaka 1993 hadi sasa ambapo bado ni shabiki mkubwa.

ENDELEA NAYE…

Ni safari nyingine mwanana naianza ya kwenda kuonana na AY baada ya kutoka nchini Afrika Kusini ‘Sauz’ hivi karibuni, nafika eneo la Mikocheni kulipo na ofisi yao ya Mkasi TV. Namkuta akiwa na waandaaji wa kipindi hicho. Namsogelea na kuwapa salamu kisha namuelezea kidogo tulipoishia kwenye simulizi hii.

AY (1)Ananielewa, kwanza ananipa michapo kidogo ya Sauz kisha anaendelea na simulizi yetu.

“Nakumbuka kipindi nipo na wenzangu wa Kundi la East Coast ni Buff G pekee alikuwa shabiki wa Barcelona na kitambo hicho nilikuwa nikicheza naye sana mpira wa mitaani,” anasema AY na kusita kuendelea, anakaa kimya kwa muda kama vile anakumbuka kitu kingine kisha anaendeleza simulizi…

“Wengi hawajui kama nilikuwa nikiishi na kuiwakilisha Dodoma kama walivyo marehemu Albert Mangwea (Ngwear), Dark Master pamoja na Noorah waliokuwa wakiunda Kundi la Chemba Squard).

“Kuna kipindi maisha yangu yalibadilika, yakawa ya kuhamahama kutokana na kazi za mare-hemu baba yangu, ambaye alikuwa akifanya kazi serikalini. Baba alinifanya niendelee kupenda sana michezo, na kwa upande wa shule (msingi) nilikuwa nafanya vizuri sana kiasi cha kushinda medali kibao (za uigizaji na uchezaji wa mpira wa tenisi) na kufanikiwa kuiwakilisha shule yangu kwa ngazi mbalimbali ikiwemo ya kata.

“Pia katika kipindi cha utoto, wako watu wengi ninaokumbuka niliwahi kucheza nao kama vile mtoto wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba, Mwamvita na January Makamba (sasa waziri) ingawa January alikuwa mkubwa kwetu, wakati huo tulikuwa mkoani Morogoro sehemu f’lani inaitwa Barabara ya Boma.

“Basi baada ya kumaliza shule ya msingi (2005) nilifanikiwa kuendelea na elimu ya sekondari katika Shule ya Dodoma, nilisoma hapo kwa miezi sita kisha nikahamia Sekondari ya Ifunda, Iringa ambapo nilisoma hadi kidato cha nne (1999).”

Anashusha pumzi na kukaa kimya kwa muda, kisha namuuliza kulikoni, anaonekana kama yuko mbali hivi kimawazo, nadhani kuna kitu anafikiria kama aniambie au la! Baada ya muda anaamua kufunguka.

“Kiukweli wakati niko sekondari, somo la Technical Drawing lilikuwa likinisumbua sana na wengi waliosoma shule za ufundi wanafahamu ugumu wa somo hilo, somo lililokuwa kwangu ni mteremeko ni Electrical Installation. Ingawa kiukweli napenda sana somo la Jiografia na mambo ya anga kwa sababu ya mikakati yangu ya baadaye kama Mungu akipenda.

Usikose sehemu inayofuatia ya simulizi hii katika gazeti hilihili.

Leave A Reply