The House of Favourite Newspapers

Simulizi Ya Kusisimua: The Darkest Hours (Saa Za Giza Totoro)- 22

0

 

MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)

0719401968

ILIPOISHIA:

Dakika chache baadaye, tuliona yale magari yanayotumika kubebea fedha na kuzisambaza kwenye benki mbalimbali, likipita kwenye barabara ya lami huku nyuma likiwa linasindikizwa na gari la polisi. Kwa wanaoyajua magari ya kubebea pesa watakuwa wanaelewa vizuri, lilikuwa ni kama Hiace ndogo lakini likiwa limezibwa pande zote.

SASA ENDELEA…

Safari yetu iliishia kwenye mtaa mmoja wenye pilikapilika nyingi, eneo ambalo baadaye nilikuja kulitambua kwamba ni Tandika. Tulisimama kwenye barabara ya vumbi ya mtaa huo, mita chache kutoka kwenye barabara ya lami.

 

Dakika chache baadaye, tuliona yale magari yanayotumika kubebea fedha na kuzisambaza kwenye benki mbalimbali, likipita kwenye barabara ya lami huku nyuma likiwa linasindikizwa na gari la polisi. Kwa wanaoyajua magari ya kubebea pesa watakuwa wanaelewa vizuri, lilikuwa ni kama Hiace ndogo lakini likiwa limezibwa pande zote.

 

Harakaharaka madereva walipeana ‘signal’, lile gari la mbele ambalo ndiyo nililokuwa nimepanda mimi, likaondoka kwa kasi na kuingia kwenye barabara ya lami, tukawa tunalifuata lile gari lililobeba fedha na lile gari jingine, liligeuza na kupita mtaa wa pili, sikuelewa linaelekea wapi.

 

Kulikuwa na magari mengine kadhaa katikati yetu, dereva akawa anajaribu kuyapita kwa fujo, mwisho likabakia gari moja mbele yetu, kisha gari la polisi halafu ndiyo lile gari lililobeba fedha.

 

Jombi ambaye tulikuwa naye kwenye gari moja, alitoa ishara kwamba kila mmoja ajiandae kwa kazi, huku nikitetemeka, niliitoa bunduki yangu niliyokuwa nimeivaa shingoni na kuificha ndani ya koti refu, nikaishika vizuri na kutoa ‘safety lock’, tayari kwa chochote.

 

“Gari litakaposimama tu, tunawaangusha kwanza hawa waliopo kwenye gari la polisi, wewe na wewe mtabaki kutoa back-up, hakikisha yeyote anayesogea mnamuangusha,” aisema Jombi huku akinioneshea mimi na yule mwenzangu, tukatazamana huku kijasho chembamba kikiwa kinatutoka.

 

Lile gari la lilikatiza na kuingia upande wa kulia, gari la polisi nalo likafuatia. Dereva wetu alipunguza mwendo kidogo, akalitoa gari barabarani, tukashuhudia yote mawili yakienda na kusimama nje ya tawi dogo la benki. Askari waliwahi kushuka, wakawatawanya watu wote waliokuwa nje ya ile benki.

 

Kulikuwa na skari kama sita hivi, wote wakiwa na silaha lakini pia kulikuwa na askari wengine kwenye lile gari lenye fedha ambao wao walivaa nguo za tofauti, tukawaona pia walinzi wa ile benki wakiungana nao kuhakikisha hakuna kinachoharibika.

 

Hata kabla ya tukio lenyewe, nilishajua kwamba hatuwezi kufanikisha tunachoenda kukifanya kwa sababu kwa hesabu za harakaharaka, wao walikuwa wengi kuliko sisi.

 

Kumbe dereva alikuwa anasubiri tu maelekezo, Jombi alipotoa ishara tu, dereva alikanyaga mafuta kwa nguvu kisha akakata kona na kuelekea pale wale askari walipokuwa wametanda.

 

Wakati wale askari wakishtuka na kuelekezea mitutu yao kwenye gari letu, lile gari jingine lilitokea upande wa pili, kwa kasi ileile, kwa hiyo wakawa ni kama wamepatwa na kiwewe, ndani ya sekunde chache tu, wote tulikuwa tumeshashuka kwenye magari yote mawili kwa staili ya kikomando kama tulivyofundishwa kule porini, tukawa tumewazunguka wale polisi na walinzi.

 

Jombi ndiye aliyekuwa wa kwanza kufyatua risasi, na ya kwanza ilimlenga mmoja kati ya wale askari, tena kichwani! Akadondoka chini kama mzigo, kilichofuata baada ya hapo ilikuwa ni kama uwanja wa vita.

 

Tuliwafyatulia mvua ya risasi kutoka pande mbili, nao wakawa wanajibu mapigo lakini kwa kuwa tulikuwa tumewazunguka, tuliwazidi ujanja. Ndani ya sekunde chache tu, watu wote walikuwa chini, si polisi, si walinzi, watu waliokuwa jirani wakawa wanakimbia huku wakipiga kelele, kila mmoja akiokoa maisha yake.

 

Kama tulivyoelekezwa, mimi na yule mwenzangu tulibaki kama ‘back-up’ kuhakikisha hakuna mtu anayesogea kwenye eneo la tukio, Jombi, Bonta na wengine kutoka kwenye lile gari, wakakimbilia mpaka kwenye lile gari huku wakiendelea kufyatua risasi.

 

Kwa kuwa tayari gari lilishakuwa limefunguliwa na sanduku la fedha kutolewa, hawakupata shida, wakaanza kusaidiana kuliburuza huku risasi zikiendelea kurindima.

 

Dereva wa lile gari letu alilisogeza mpaka pale karibu na lile sanduku kwa kasi mithili ya magari ya mashindano, Akina Jombi wakalibeba lile sanduku lililoonekana kuwa zito kwelikweli na kuliingiza ndani ya gari. Waliingia ndani ya gari na dereva akaondoka kwa kasi kubwa, sekunde chache tu baadaye tayari walishaingia barabarani.

 

Kimbembe kikabakia kwetu sisi wawili tuliobaki kutoa ‘back-up’ kama tulivyoelekezwa, lile gari la pili lilikuwa limepaki kama mita hamsini hivi kutoka pale tulipokuwepo, kwa hiyo ilikuwa ni lazima tulikimbilie haraka iwezekanavyo na kuungana na wale wenzetu wawili ambao nao walibaki kama ‘back-up’, kibaya ni kwamba wote tulikuwa ni kutoka Kikosi B.

 

Tukiwa tunalikimbilia kwa tahadhari kubwa huku tukifyatua ovyo risasi, tulishtukia magari mengine mawili ya polisi yakiingia kwa kasi ya kimbunga, askari wengi wakaruka kabla hata hayajasimama na kuanza kutufyatulia risasi kama mvua.

 

Kilichotokea siku hiyo, kilikuja kubadilisha kabisa maisha yangu na naweza kusema kwamba hata ile roho ya ukatili na unyama niliyokuja kuwa nayo, ilisababishwa kwa kiasi kikubwa na kitu kilichotokea siku hiyo.

 

Hali ilichafuka, risasi zikawa zinamiminwa kama mvua, zote zikielekezwa kwetu. Kumbuka mpaka wakati huo, kundi la kwanza ambalo ndiyo lenye watu wazoefu, akiwemo Bonta, Jombi na wengine, lilishaondoka na tuliobakia, naweza kusema wote tulikuwa wanafunzi.

 

Tulijaribu kupambana, ikawa na sisi tunafyatua risasi kwa kasi lakini kwa sababu wale askari walikuwa wengi na walikuwa na mafunzo kuliko sisi, walituelemea. Nilijitahidi kadiri ya uwezo wangu kutumia mafunzo yote tuliyopewa na Mamba, ikiwemo staili ya kukimbia kwa kubingirika huku nikiendelea kufyatua risasi.

 

Pale chini palikuwa pamepigwa ‘pavings’,vile vigae vidogo vinavyowekwa kwenye barabara za nje kwa hiyo kujirusha hakukuwa jambo jepesi lakini ilikuwa ni bora kuvumilia maumivu ya kujirusha kuliko kupigwa risasi.

 

Sijisifii lakini naweza kusema kwamba kati ya wale tuliobaki, mimi ndiyo nilikuwa shapu kidogo na nilikuwa najua kinachotakiwa kufanyika ni nini.

 

Mamba aliwahi kutufundisha kule porini kwamba inapotokea mnashambulia, mnatakiwa kusonga mbele lakini mkiwa mnashambuliwa, mnatakiwa kurudi nyuma kwa kasi na alikuwa anatumia zaidi neno la Kiingereza la ‘retreat’, yaani kurudi nyuma kwa lengo la kukimbia au kujipanga upya.

 

Mimi nilishaona kwamba hali imechafuka na badala ya sisi kuwa washambuliaji, sasa tulikuwa tukishambuliwa, kwa hiyo nikaitumia vizuri ile dhana ya ‘retreat’ lakini wenzangu walionesha kwamba hawajaiva.

 

Nasema hivyo kwa sababu yule mmoja tuliyekuwa naye kwenye lile gari lililotuacha, yeye alikuwa akikimbia kwa staili ya kuwapa mgongo wale askari, yaani akili zake zilikuwa ni kuwahi kufika kwenye gari tu bila kujua hatari iliyopo.

 

Wala hakukumbuka hata kutumia ile mbinu niliyokuwa naitumia mimi, ya kujirusha  kama unapiga ‘samasoti’, ukitua chini unageuka na kushambulia kisha unaruka tena! Yeye alikuwa anakimbia mzimamzima bila kujua kwamba kitendo cha kugeuka na kuwapa mgongo watu wenye silaha, kinatosha kumaliza kazi kwa sababu watakulenga bila kizuizi chochote.

 

Nikiwa namshuhudia kwa macho yangu, alishonwa risasi kibao mgongoni, akapiga yowe moja tu, akadondoka kama mzigo huku damu zikianza kuvuja mithili ya bomba lililopasuka. Sijawahi kushuhudia mtu akikata roho kwa kupigwa risasi, hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza.

 

Moyo wangu ulikufa ganzi, nikajua anayefuatia ni mimi na kamwe hakuna atakayeweza kutoka salama!

 

Nilimtazama pale chini alipodondoka, nikaingiwa na ujasiri wa ajabu, niliinuka na kuikamata vizuri bunduki, nikaanza kufyatua risasi kwa staili ambayo Mamba alituambia kwamba inaitwa ‘sweeping’, yaani unafagia kutoka kushoto kwenda kulia kisha unarudi tena kushoto.

 

Kitendo kile kilisaidia kuwapunguza kasi wale askari kwani niliona wengine wakianguka na wengine wakijirusha kukwepa risasi, nikatumia mwanya huo kujirusha mpaka kwenye gari.

 

Japokuwa mimi ndiye niliyekuwa mbali, niliwatangulia wale wenzangu kuingia kwenye gari, dereva naye alishakanyaga mafuta na gari likawa linatoa moshi, yule mwingine alifanikiwa kupanda lakini mwenzake alipojaribu kuingia kwenye gari, naye alishonwa risasi kibao za mgongoni, akadondoka kama mzigo huku damu zikivuja mithili ya bomba.

 

Dereva aliondoa gari kwa kasi kubwa, tukajua tumesalimika! Kufumba na kufumbua tukashtukia vioo vya lile gari vikimwagika kuonesha kwamba wale askari bado walikuwa wakiendelea kutufyatulia risasi.

 

Akili ya haraka ilinituka kulala chini kabisa ya siti, tukamuachia derava afanye kazi yake ambapo alikuwa akiendesha gari kama kichaa, honi kali, breki za ghafla, kona za ajabuajabu na kelele za watu waliokuwa wakikoswakoswa na gari letu zilishereheshwa na milio ya risasi zilizokuwa zikiendelea kufyatuliwa kuelekezwa kwenye lile gari.

 

Nilijikausha pale chini huku nikishikilia vyuma vinavyoziunganisha siti za gari na ‘chasis’, dereva akaendelea kufanya yake na kiukweli nikiri kwamba maisha yetu kwa wakati huo, yalikuwa yakimtegemea yeye.

 

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Kwa shilingi 6,000 tu unaweza kupata simulizi yote kwa mfumo wa softcopy, piga 0719401968. Pia ukitaka kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia:

 

www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com, Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online.

Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

Leave A Reply