The House of Favourite Newspapers

SIMULIZI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 9

0

 

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower)

0719401968

ILIPOISHIA:

“Mimi pia nataka afe, na nitahakikisha namuua kwa mikono yangu.”

 

“Sikia Snox, usifanye maamuzi kwa hasira. Kwa hali uliyonayo hivi sasa, unatakiwa kwanza kukaa na kuuguza jeraha lako huku ukipanga mipango ya namna ya kurudi, utakapokuwa tayari mimi nipo tayari kukusaidia.”

 

SASA ENDELEA…

“Nashukuru kwa msaada wako, ahsante sana Siza,” nilimwambia huku nikimpa mkono, naye akanipa wake, nikautumia kama ‘sapoti’ ya kusimama kutoka pale kitandani. Tukakamatana mikono kikakamavu kama kawaida yetu. Ghafla nilisikia maumivu makali pale kwenye lile jeraha la mkono, Siza akanituliza na kunitaka nikae, nikafanya hivyo.

 

“Huwezi kupambana ukiwa na hali kama hiyo, kaa utulie! Hapa ni sehemu salama, nitakulinda!” alisema Siza, nikamtazama usoni, na yeye akanitazama, macho yetu yakagongana na kweli alionesha kumaanisha alichokuwa anakisema.

 

Nilitikisa kichwa kuonesha kumkubalia, akaniambia nimsubiri anatoka kidogo lakini akanionya kutotoka nje. Alitoka na kuniacha mle ndani huku nuru ya mshumaa ikinisaidia kutazama vizuri mazingira.

 

Lilikuwa ni jengo kubwa kama ghala fulani hivi ambalo halitumiki, na kulikuwa na vifaa vingi vya kilimo vikiwa vimehifadhiwa.

 

Niliendelea kuchunguza vizuri na katika utafiti wangu, nilibaini kwamba kuna uwezekano mkubwa ghala hilo likawa ni miongoni mwa maghala nisiyoyajua ya Bosi Mute kwa sababu alikuwa amejitanua sana maeneo ya kibaha, akijifanya anajishughulisha na kilimo cha kisasa.

 

Moyoni nilikuwa na wasiwasi kuhusu usalama wangu, hasa kutokana na Siza kuniambia kwamba Bosi Mute alikuwa ameagiza niuawe baada ya tukio lile la kuwashambulia vijana wake na kujaribu kumtorosha Saima.

 

Hata hivyo, kauli alizoniambia Siza kwamba nisiwe na wasiwasi atanilinda, zilinifanya kidogo niwe na amani.

 

Kilichonipa ujasiri zaidi, ni uwepo wa silaha yangu, nikaichukua pale nilipokuwa nimeiweka baada ya kuridhikana maelezo ya Siza, nikaikumbatia na kuibusu, nikawa naitazama huku mawazo mengi yakiendelea kupita ndani ya kichwa changu.

 

“Lazima nitakuokoa Saima, tena haraka kuliko unavyotegemea,” nilisema, nikaibusu tena bunduki yangu na kuiweka pale kitandani, upande wa kichwani kisha nikajilaza, mawazo mengi yakiendelea kupita ndani ya kichwa changu.

 

Nilikuwa nasikiamaumivu makali pale kwenye jeraha la mkononi lakini kwa kuwa haikuwa mara yangu ya kwanza kupata majeraha makubwa mwilini mwangu, tena ya risasi, nilijikuta nikipata nguvu za kuendelea kuvumilia maumivu hayo.

 

Kumbukumbu zangu zilinirudisha nyuma mpaka siku ya kwanza nilipokutana na Bosi Mute ambaye kama nilivyosema, ndiye aliyenifanya nikaingia kwenye kazi hiyo ya hatari kwelikweli.

 

Nakumbuka ilikuwa ni tarehe za mwishomwisho za mwezi Desemba, wakati maandalizi ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya yakiwa yamepamba moto.

 

Tofauti na familia zote ambazo zilikuwa zikiendelea na maandalizi ya sikukuu, kwetu sisi hali ilikuwa tofauti.

 

Nyumba yote ilikuwa imegubikwa na huzuni kubwa kutokana na hali ya kiafya ya baba ambaye alikuwa anaumwa sana, akiwa amefikia hatua ya kukata kauli.

 

Tulishafanya kila kitu kama wanafamilia kuokoa maisha ya baba, alishatibiwa sana Hospitali ya Taifa ya Muhimbili bila mafanikio, tulishauza karibu mashamba na viwanja vyetu vyote kuokoa maisha ya baba, lakini yote ilikuwa ni kazi bure.

 

Hali ya kiafya ya baba ilikuwa ikizidi kuwa mbaya kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele na ikafika mahali, hata hospitali kwenyewe tukaambiwa tujaribu kutafuta mbinu nyingine kwani ilionesha matibabu ya hospitalini hayawezi tena kumsaidia baba.

 

Kwa waliowahi kuuguza, watakuwa wanaelewa hali mnayokuwa nayo ndugu pale mnapoambiwa na madaktari kwamba jaribuni kuhangaika kwa njia nyingine kwani matibabu ya hospitalini yameshindikana.

 

Kama hujawahi kufikwa na hali kama hiyo, maana yake huwa ni kama mnaambiwa mchukueni ndugu yenu akafie nyumbani.

 

Hivyo ndivyo ilivyotokea kwetu, hatukuwa na cha kufanya zaidi ya kumchukua baba hospitalini akiwa na hali mbaya na kurudi naye nyumbani, Msanga, Kisarawe Mkoa wa Pwani.

 

Kiasili sisi ni wenyeji wa Kanda ya Ziwa, Mkoa wa Mara kwenye eneo liitwalo Kiabakari na huko ndiko tulikozaliwa ingawa baadaye katika pilika za maisha, baba alipata kazi kwenye mashamba ya korosho ya Mhindi mmoja kwa sababu kitaalamu baba alisomea mambo ya kilimo, tukahama kutoka Mara na kwenda Msanga na kujenga makazi yetu ya kudumu hapo.

 

Baba ndiye aliyekuwa kiongozi wa familia na maisha yetu yote tulikuwa tukimtegemea kwa hiyo kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja alipokuwa anaumwa, maisha yetu yalikuwa ya tabu sana.

 

Basi tukiwa hapo nyumbani, baadhi ya ndugu kutoka Mara walikuja, tukawa tunashirikiana kumsindikiza baba katika siku za mwisho za uhai wake, kwa hiyo pale nyumbani palikuwa ni kama pana msiba.

 

Majirani na jamaa zetu nao walikuwa nasi bega kwa bega, wanaoishi jirani wakawa wanakuja na kuondoka huku wengine wakihamia hapohapo nyumbani kwa sababu sote tulikuwa tunajua lolote linaweza kutokea wakati wowote.

 

Hali ilipozidi kuwa ngumu pale nyumbani, wakati mwingine tukishinda njaa au kutegemea misaada ya ndugu, jamaa na marafiki, niliamua kuchukua uamuzi mgumu.

 

“Utaondokaje mwanangu wakati hali ya baba yako unaiona?”

 

“Sasa mama, unafikiri tutaendelea na maisha haya mpaka lini? Kuna dawa baba aliandikiwa aendelee kutumia akiwa nyumbani, zote zimeisha na hakuna fedha za kuzinunua tena, ndugu ndiyo kama hao unavyowaona, hakuna mwenye msaada zaidi ya kututegemea sisi, sina namna mama ngoja nikajaribu kutafuta hata kibarua mjini.”

 

“Kibarua gani mwanangu wakati hata elimu huna, umeishia form two kwa sababu ya kukosa ada, ingekuwa baba yako ameanza kuumwa ukiwa umemaliza form four angalau ningekuruhusu, utaenda kufanya kazi gani mjini?”

 

“Mama mimi ni mwanaume.”

 

“Sawa lakini wewe bado ni mdogo sana Kenny, mimi siwezi kukuruhusu mwanangu, kaa tu hapahapa nyumbani tutajua cha kufanya,” alisema mama akiwa na uso wa huzuni, macho yake yakiwa yamebadilika rangi na kuwa mekundu.

 

Kiukweli japokuwa alinisihi sana, mimi nilishakuwa na uamuzi wangu na miongoni mwa tabia ambazo wazazi wangu walikuwa hawazipendi kabisa, ni suala langu la kuwa na misimamo yangu.

 

Tangu nikiwa mdogo, nilikuwa na hulka moja kwamba nikishaamua kung’ang’ania kitu, lazima nikifanye hata kama nikikatazwa kiasi gani.

 

Basi japokuwa kwa nje nilionekana kama nimemuelewa mama, moyoni nilishaapa kwamba lazima niende Dar es Salaam. Uzuri ni kwamba kutoka Msanga mpaka Dar es Salaam siyo mbali sana, nikazugazuga pale nyumbani na nilipopata upenyo tu, niliondoka kimyakimya bila kumuaga mtu yeyote.

 

Nilienda moja kwa moja mpaka stendi ya Msanga, huku mfukoni nikiwa sina hata senti tano.

 

Nilipofika, nilijichanganya na abiria wengine waliokuwa wakisubiri usafiri na moyoni nikawa najisemea liwalo na liwe!

 

Mara lilikuja gari, likateremsha abiria waliokuwa wakitoka mjini na kugeuza, abiria wote wakalikimbilia, na mimi nikajichanganya.

 

Muda mfupi baadaye, tayari nilikuwa nimepanda, tena nilifanikiwa kupata na siti, nikakaa huku nikiwa sijui nitamjibu nini kondakta atakapoanza kudai nauli.

 

Basi muda mfupi baadaye, safari ilianza.

 

Mbele kidogo, kondakta alianza kukusanya nauli na alianza na abiria waliokuwa mbele, taratibu akawa anasogea kule nyuma nilikokuwa nimekaa, mapigo ya moyo yakaanza kunienda mbio.

 

Aliendelea kukusanya nauli mpaka aliponifikia, akagongagonga safaru alizokuwa amezishika mkononi, kama wanavyofanya makonda wa daladala wanapodai nauli.

 

“Nitakupa mbele!” nilijibu kwa kujiamini, akanitazama usoni, na mimi nikawa ‘siriasi’ kisha akaendelea kuchukua nauli kwa abiria wa upande wa pili. Mbele kidogo, kuna abiria walikuwa wanashuka, basi akaacha kupokea nauli na kwenda kuwafungulia mlango.

 

Waliposhuka safari iliendelea, akarudi tena kuendelea kukusanya nauli na alipomaliza, alinigeukia tena.

 

“Hapoo!”

 

“Si nimekwambia nitakupa mbele?” nilijibu kijeuri, akanitazama tena kisha akarudi mlangoni.

 

Safari iliendelea abiria wakawa wanashuka na kupanda na hatimaye tukawa tumekaribia Gongo la Mboto ambapo kimsingi ndiyo mwisho wa magari yanayotoka Pwani, akanifuata tena na safari hii, alikuwa amekuja kisharishari kabisa.

 

“Nitakupa wakati wa kushuka,” nilimwambia, akaona kama namletea masihara kwenye kazi. Akanikomalia nimlipe, na mimi nikawa nakomaa kwamba nitakupa wakati wa kushuka, zogo kubwa likaibuka kiasi cha kufanya abiria wengine waingilie.

 

Wengine walikuwa wananipigia kelele mimi kwamba nini kinachonizuia kumpa nauli yake? Wengine wakawa wanampigia kelele konda kwamba kwa nini asisubiri mpaka nitakapokuwa nashuka.

 

“Mimi hapa sina nauli lakini kuna ndugu yangu ananisubiri stendi, yeye ndiye atakayelipa,” nilisema katikati ya lile zogo, konda akazidi kuwa mbogo kiasi cha kufikia hatua ya kunikunja, tukaanza kuvutana.

 

Yeye alikuwa na mwili mkubwa na kimsingi ndiye aliyekuwa na haki, kwa hiyo alinidhibiti kisawasawa, abiria wengine wakawa wanamsihi aniachie lakini akakomalia kwamba hawezi kuniachia mpaka nilipe, ndani ya gari ikawa ni vurugu mtindo mmoja.

 

Tayari tulishawasili Gongo la Mboto, basi akanivuta kutoka pale kwenye siti na kuanza kunitoa nje huku akifoka kwamba nikamuoneshe huyo atakayenilipia nauli, vinginevyo atanikomesha.

 

Niliogopa sana, nikawa hata sijui mwisho wangu utakuwa nini. Alinishusha huku akiwa bado amenikwida kwa nguvu, watu wakajaa, abiria wengine waliteremka kwenye gari na kuja kujaribu kutuamulia.

 

“Kwani unamdai shilingi ngapi jamani? Basi mimi namlipia,” alisema mama mmoja wa makamo huku akitoa noti ya shilingi elfu kumi, kwa hasira konda alinitingishatingisha, akanizibua kofi la nguvu na kunisukuma, nikapepesuka na kwenda kudondokea kwenye mtaro, wahuni wa stendi wakawa wanacheka huku abiria wengine wakianza kumjia juu konda kwamba kwa nini amenipiga wakati tayari msamaria mwema alishatoa fedha.

 

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia:

 

www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com ,  Facebook:

 

Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online.

 

Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

Leave A Reply