The House of Favourite Newspapers

SIMULIZI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS(SAA ZA GIZA TOTORO)-25

0

MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)

0719401968

ILIPOISHIA:

Kwa mara ya kwanza nilielewa maana ya mapenzi! Ile hofu niliyokuwa nayo ndani ya moyo wangu iliyeyuka na nikajikuta nikitamani kurudia tena na tena sanaa ile ya kikubwa, naye akawa ananipa ushirikiano wa kutosha na kunielekeza nini cha kufanya.

Mpaka tunakuja kulala, ilikuwa ni karibu saa nane za usiku, nikapitiwa na usingizi mzito kiasi kwamba sikuelewa tena kilichoendelea mpaka nilipokuja kuzinduka kukiwa kumeshapambazuka.

SASA ENDELEA…

Harakaharaka aliamka na kwenda bafuni, akaoga na aliporudi, alijiandaa tayari kwa kuondoka. Nikachukua noti tatu za shilingi elfu kumikumi na kumpa.

 

“Hizi za nini?”

 

“Utanunulia mahitaji yako madogomadogo.”

 

“Aliyekwambia mimi nina shida na fedha zako ni nani? Au unafikiri najiuza?” aliniambia huku akikataa kuzipokea zile fedha. Akachukua mkoba wake mdogo na kuanza kutembea harakaharaka kuelekea kwenye mlango wa kutokea.

 

Nilibaki namsindikiza kwa macho huku moyo wangu ukiwa na furaha ya ajabu. Alipoondoka, nilienda kufunga vizuri milango, na mimi nikaenda kuoga kisha nikarudi sebuleni na kuwasha runinga, nikawa nachezeachezea simu yangu.

 

Kilichonishtua ilikuwa ni taarifa ya habari iliyokuwa inaoneshwa kwenye TV kuhusu tukio baya la ujambazi lililotokea Tandika kwenye tawi dogo la benki. Niliacha kila nilichokuwa nakifanya na kuikodolea macho runinga.

 

Mapigo ya moyo yalianza kunienda mbio baada ya kugundua kwamba kilichokuwa kinatangazwa lilikuwa ni lile tukio tulilolifanya jana yake. Mtangazaji aliendelea kueleza kwamba katika tukio hilo, watu kumi na moja wamefariki dunia, watano kati yao wakiwa ni askari wa jeshi la polisi, wanne walinzi wa kampuni binafsi waliokuwa wakilinda benki hiyo na wawili kati yao ni majambazi.

 

Nilishtuka sana kugundua kwamba kumbe watu wengi walikuwa wamepoteza maisha kiasi hicho, mwili mzima ukawa unatetemeka, habari zikaendelea kueleza kwamba katika tukio hilo, watu wengine sita wamejeruhiwa vibaya wakiwemo askari na walinzi ambao wote walikimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu.

 

Pia ilielezwa kwamba majambazi hao waliovamia gari la kubebea fedha kwa kushtukiza na kuanza kupiga risasi hovyo, walikuwa wamefanikiwa kupora jumla ya shilingi milioni mia moja na sitini za Kitanzania na kutokomea kusikojulikana.

 

“Ni tukio baya sana kuwahi kutokea katika siku za hivi karibuni, tulifanikiwa kuwaua wawili eneo la tukio na msako mkali unaendelea kuhakikisha wahusika wote wanapatikana na kurejesha kiwango hicho cha fedha zilizoibwa.

 

“Nawaomba wananchi watulie, nawahakikishia kwamba tunaendelea na uchunguzi na tutahakikisha wote waliohusika wanapatikana na kushughulikiwa ipasavyo,” kamanda wa polisi wa kanda maalum ya Dar es Salaam, alisikika akizungumza kutoka eneo la tukio, huku picha za video za eneo la tukio zikipita. Ilikuwa ni habari ya kutisha sana.

 

Habari hiyo ilifika mwisho na mtangazaji akawa anaendelea na habari nyingine lakini bado akili zangu zilikuwa zimeganda kwenye tukio hilo. Mwili wote ulikuwa umeishiwa nguvu, nilisimama na kuchungulia nje nikihisi pengine naweza kuona hata gari la polisi likiwasili.

 

Hofu ilinizidi kuliko kawaida, nikaenda chumbani lakini nako nilihisi kama kuna mtu ananitazama, nikarudi tena sebuleni na kukaa lakini bado akili yangu ilikuwa imevurugika. Nilijikuta natamani tena kulewa, niliamini nikipiga ‘vyombo’, ile hofu niliyonayo inaweza kuyeyuka kama ilivyokuwa jana yake.

 

Swali likawa je, nitatokaje? Niliamua kujilipua kwamba liwalo na liwe. Nilivaa nguo harakaharaka na kichwani nikavaa kofia ambayo niliishusha na kuziba sehemu kubwa ya uso wangu.

 

Unajua wakati mwingine ni rahisi sana kumtambua mtu mwovu unapokutana naye barabarani na pengine hata vyombo vyetu vya ulinzi vinatakiwa kuelekeza nguvu zaidi katika kufundisha watalaamu wa masuala ya saikolojia.

 

Nimesema hivyo kwa sababu kwa hali niliyokuwa nayo, kama ningekutana na mtu yeyote anayeweza kusoma sura ya mtu, ingekuwa rahisi sana kunigundua kwamba sikuwa sawa na pengine huo ungeweza kuwa mwanzo mzuri wa kupata ukweli wa kilichokuwa kimejificha nyuma ya pazia.

 

Nilitoka nikiwa na ‘mawenge’ mpaka mtaa wa pili, nikaingia kwenye kiduka kidogo kilichokuwa kinauza bidhaa mbalimbali za nyumbani, yaani kilijengwa kama ‘supermarket’ flani hivi kwa sababu mle ndani kulikuwa na kila kitu.

 

Sikuwa nazijua pombe vizuri, kwa hiyo nilichofanya ilikuwa ni kuonesha tu kwa kidole, ‘nataka ile na ile’, mhudumu akanishushia chupa kama nne hivi za pombe tofautitofauti, nikamuuliza bei ambapo aliponitajia tu, nilizama mfukoni na kutoa noti nne nyekundu na kumkabidhi, sikusubiri hata chenji, nikaondoka harakaharaka kurudi kwangu.

 

Niligundua pia kwamba sikuwa nimekula na nilishasisitizwa na Bonta kwamba ninapotaka kulewa, ni lazima nihakikishe nimekula na kushiba.

 

Nilipita kwenye kimgahawa kilichokuwa pale jirani, nikamuita mhudumu mmoja wa kike na kumuuliza naweza kupata kitu gani cha kula asubuhi hiyo. Alinitajia orodha ya vilivyokuwepo, nikamwambia nataka supu na chapati nne lakini sina kitu cha kubebea.

 

“Kwani unaishi mbali?”

 

“Hapana! Pale kwenye ile nyumba yenye geti jeusi,” nilimwelekeza, akaniambia basi nitangulie ataniletea na vyombo vyake. Nilimshukuru kwa sababu sikuwa nataka kuendelea kuonekana nje, nikatoa noti ya shilingi elfu kumi na kumpa, nikaondoka zangu huku mara kwa mara nikigeuka kutazama kama hakuna mtu anayenifuatilia.

 

Niliingia ndani na kwa sababu yule dada aliniambia kwamba atakuja muda si mrefu, sikufunga mlango. Nilizibwaga zile chupa za pombe pale chini, nikabadilisha runinga kutoka kwenye ile chaneli ya habari na kuweka muziki, nikaongeza sauti na kukaa pale kwenye kochi, nikafungua chupa moja na kuanza kuigida.

 

Muda mfupi tu baadaye, tayari nilishaanza kuchangamka, ile hofu niliyokuwa nayo ikaanza kuyeyuka na nikawa najikuta tu nachezesha mwili wangu kufuata midundo ya muziki. Kumbe yule dada alishafika na kugonga mlango lakini kutokana na sauti kubwa ya muziki, wala sikumsikia, ikabidi aingie.

 

Nilipogeuka, nilishtuka kumuona msichana huyo akiwa amesimama mlangoni, tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.

 

“Kumbe unajua kucheza,” aliniambia huku akicheka, na mimi nikacheka sana na kukaa. Tayari pombe zilishaanza kukolea ndani ya kichwa changu kwa hiyo nilikuwa na uchangamfu usio wa kawaida.

 

“Una furaha sana mwenzetu, asubuhi yote hii unacheza muziki,” alisema huku akiinama na kuweka ‘hotpot’ lililokuwa na supu pale mezani, macho yangu yakatua kwenye eneo lake la nyuma.

 

Sijui nini kilitokea lakini nilijikuta nikivutiwa naye na hapohapo nikatamani nilale naye.

 

“Kumbe we mzuri kiasi hicho,” nilisema huku nikimsogelea mwilini na katika hali ambayo hakuitegemea, alishtukia nikipitisha mikono yake kwenye kiuno chake. Mshtuko alioupata nusura amwage ile supu, akanigeukia na kunitazama.

 

“Kwani unaishi na nani humu?”

 

“Naishi na braza’angu lakini kasafiri kaenda Nairobi, niko peke yangu,” nilimjibu huku nikimvutia kwangu.

 

“Mh! Mbona kama umelewa?”

 

“Kwani kuna tatizo lolote mrembo? Fedha siyo tatizo kwangu, kwa hiyo nakula, nakunywa, nalewa muda wowote ninaotaka,” nilisema huku nikiingiza mkono mfukoni na kutoa noti nyingi za shilingi elfu kumikumi.

 

“Hata wewe ukitaka naweza kukupa,” nilisema, nikamuona ananitazama kwa kunirembulia macho! Nilikuwa na uchawi wa Kizungu.

 

“Mi nakupenda mwenzio, hivi unaitwa nani?” nilisema huku nikijaribu kumbusu, cha ajabu wala hakuleta ubishi wowote, akaniruhusu nimbusu kwenye shavu lake, akaniambia jina lake anaitwa Neema.

 

“Njoo basi huku mara moja,” nilisema huku nikimshika mkono na kuanza kumvuta kuelekea chumbani, mwanzo alileta ule ubishi wa kawaida wa kikekike lakini nilipozidi kumng’ang’aniza, alikubali, nikamkokota mpaka chumbani.

 

Hata sijui nini kilitokea lakini nafikiri kwa sababu ya pombe, ukichanganya na ukweli kwamba tayari nilishajua ladha ya mapenzi, nilijikuta nikipandwa na mzuka wa hatari wa kufanya mapenzi na Neema.

 

Ilikuwa kazi ngumu kidogo kumshawishi lakini baada ya kumpa noti nyekundu mbili, mwenyewe alikubali lakini akanitaka nisimwambie mtu yeyote kwa sababu bosi wake akijua anaweza kumfukuza kazi.

 

Harakaharaka nilivua shati langu, nikamsaidia na yeye kuvua zake, nikamvutia kifuani kwangu huku nikiwa na papara zisizoelezeka. Mara nilishtuka kusikia mlango ukigongwa kwa nguvu, kibaya zaidi ni kwamba sikuwa nimeufunga, nikashtuka kuliko kawaida.

 

Kabla hata sijajua nini cha kufanya, nilishtukia mlango wa chumbani ukisukumwa kwa nguvu. Alikuwa ni Bonta na kwa jinsi ilivyoonesha, kulikuwa na tatizo kubwa lililotokea.

 

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia: www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com ,  Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online. Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

 

 

 

Leave A Reply