The House of Favourite Newspapers

SIMULIZI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS(SAA ZA GIZA TOTORO)-26

0

MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)

0719401968

ILIPOISHIA:

Harakaharaka nilivua shati langu, nikamsaidia na yeye kuvua zake, nikamvutia kifuani kwangu huku nikiwa na papara zisizoelezeka. Mara nilishtuka kusikia mlango ukigongwa kwa nguvu, kibaya zaidi ni kwamba sikuwa nimeufunga, nikashtuka kuliko kawaida.

SASA ENDELEA…

Kabla hata sijajua nini cha kufanya, nilishtukia mlango wa chumbani ukisukumwa kwa nguvu. Alikuwa ni Bonta na kwa jinsi ilivyoonesha, kulikuwa na tatizo kubwa lililotokea.

 

“Hebu achana na chochote unachokifanya, binti vaa nguo zako ondoka haraka!” alisema Bonta huku akinitazama, akionesha kutokuwa na hata chembe ya masihara. Harakaharaka nilivaa nguo zangu lakini moyoni nikawa nahisi kama Bonta ameniingilai sana uhuru wangu.

 

Hata hivyo, nilikiuwa najua kwamba Bonta siku zote ni mtu anayenipenda na kuniheshimu, kwa hiyo lazima kuna sababu iliyomfanya akanifanyia kitendo hicho. Yule msichana alivaa nguo zake harakaharaka akionesha kufadhaika sana, akatoka sebuleni an kuchukua vyombo vyake alivyoniletea supu, akatoka huku akikimbia.

 

“Kuna tatizo! Hakikisha umefunga nyumba vizuri, tunaondoka,” alisema Bonta huku akizunguka huku na kule, kweli nilifanya kama alivyoniambia, nikafunga chumbani, nikazima kila kitu na wakati natoka, aliona ule mfuko uliokuwa na chupa za pombe.

 

Akauvuta na kuchungulia ndani kisha akanitazama, hakusema kitu zaidi ya kuuchukua. Tukatoka mpaka nje, awali nilidhani kwamba Bonta atakuwa amekuja peke yake lakini kumbe alikuwa amekuja na watu wengine kadhaa.

 

“Ingia nyuma!” aliniambia huku akinipa ishara ya kuingia kwenye siti ya nyuma ya gari dogo lililokuwa limepaki pale nje, mle ndani niliwakuta Jombi, yule jamaa mwingine tuliyeenda naye kwenye tukio Tandika na mwanamke mmoja ambaye sikumjua, yeye alikaa siti ya pembeni na dereva, Bonta ndiye aliyekuwa nyuma ya usukani.

 

“Bosi Mute ameagiza tuondoke mjini, hali siyo shwari kwa sasa, polisi wanatusaka kwa udi na uvumba,” alisema Bonta wakati akiondoa gari kwa kasi, sasa nikawa nimepata picha ya nini kilichokuwa kinaendelea.

 

Ilikuwa ni lazima hali hiyo itokee, hamuwezi kusababisha mauaji makubwa kama tuliyoyasababisha sisi, tukamwaga damu za askrai na watu wasio na hatia kisha mambo yaishe hivihivi! Lilikuwa ni jambo lisilowezekana.

 

Basi tulitoka na kupita Barabara ya Bagamoyo, hii inayopita Mwenge, tukaenda mpaka Njia panda ya Goba na kuchanja kuelekea kule ndanindani, mwisho tukatokezea Mbezi na kuingia Morogoro Road, safari ikaendelea kwa muda mrefu na mwisho tukafika Kibaha.

 

Japokuwa tulikuwa tukisafiri mchana, hakuna mtu yeyote aliyetutilia wasiwasi na nakumbuka njiani tulipita kwenye vizuizi vingi vya barabarani lakini hatukusimamishwa hata mara moja. Unajua wakati mwingine, polisi huwa wanakosea sana kuamini kwamba wahalifu wote huwa wanatembea usiku tu.

 

Kwa ushuhuda wa mimi mwenyewe, naweza kukiri kwamba matukio mengi tulikuwa tukiyafanya usiku wa giza totoro lakini pia yalikuwepo matukio mengine mengi ambayo tulikuwa tukiyafanya mchana wa jua kali.

 

Kuna wakati kwa mfano, tulikuwa tukisakwa na polisi kwa udi na uvumba na wakati huohuo tukawa tunajichanganya mitaani lakini kwa namna ambayo ni vigumu mtu yeyote kukutilia mashaka.

 

Basi tulipofika Kibaha, tuliiacha barabara ya lami na kuingia mkono wa kulia, safari ikaendelea kwa muda mrefu na mwisho tuliishia kwenye geti kubwa ambalo lilifunguliwa na walinzi wenye silaha.

 

Tukaingia mpaka ndani nikiwa nashangaashangaa. Kwa wenzangu, ilionesha kwamba walikuwa wanayajua mazingira kwa sababu gari liliposimama tu, wote waliteremka na kila mtu akaendelea na hamsini zake.

 

Yaani mle ndani jinsi mlivyokuwa, japokuwa kwa nje ungeweza kudhani labda kumezungushiwa ukuta tu halafu ndani hakuna shughuli yoyote inayoendelea ziaidi ya kilimo lakini ndani kulikuwana ulimwengu mwingine tofauti kabisa. Labda niseme hivi, lile halikuwa shamba kama ambavyo mtu angeweza kuamini baada ya kuona kibao kikubwa pale nje, ilikuwa ni kama kambi ambayo ndani yake kuna shughuli kibao zinazoendelea kimyakimya. Kulikuwa na majengo mengi yakiwa yamejengwa kwa mpangilio maalum.

 

“Hujawahi kufika huku?”

 

“Sijawahi kabisa!”

“Hii ni ngome yetu ya siri! Mambo yakiharibika kule mjini huwa tunakuja huku kupumzika na kujipanga upya,” alisema Bonta huku akinitembeza. Ni hapo ndipo tulipopata nafasi ya kuzungumza naye vizuri kwa sababu tangu lile tukio la ujambazi litokee, mimi na yeye hatukupata nafasi ya kuzungumza.

 

“Unaionaje kazi?”

 

“Ngumu sana! Daah, braza hii kazi ni hatari sijawahi kudhania.”

 

“Sisi hatujasoma mdogo wangu, tunakula kutokana na nguvu zetu. Wenzetu waliosoma wameajiriwa huku wanakula maisha, kwa hiyo lazima uipende kazi yako ndipo utakapoiona rahisi.”

 

“Braza, nitaipendaje kazi ya kuua au kuuawa!”

 

“Kuua au kuuawa huwa inatokea kama bahati mbaya, hakuna kazi ambayo haina ubaya, cha msingi ni umakini tu. Mbona matukio kibao huwa tunafanya na hafi mtu hata mmoja? Ile ilikuwa bahati mbaya,” alisema Bonta, akaanza kunitolea mifano ya watu kibao ambao walifanikiwa kabisa kubadili maisha yao kwa sababu ya kazi ya kushika mashine.

 

Alinitolea mfano wa Jombi, yule rafiki yao akasema ni tajiri mkubwa sana mjini, anamiliki baa kubwa nne, hoteli mbili na nyumba kibao kwa sababu ya kazi hiyohiyo!

 

“Cha msingi ni kuipenda kazi yako tu, halafu pia kuna jambo jingine muhimu sasa sijui wewe imani yako ikoje,” alisema Bonta tukiwa tumeshakaribia kufika kwenye jengo moja lililoonekana kuwa zuri kuliko mengine ndani ya eneo hilo.

Aliniambia kwamba kazi za kushika bunduki, ni lazima mtu uzindikwe na kutoa kafara, vinginevyo uwezekano wa kupigwa risasi na kufa ni mkubwa sana.

 

Yalikuwa ni mambo mageni kabisa kwangu, aliendelea kunisimulia jinsi yeye na wenzake wanavyopelekwa kwa mganga na Bosi Mute karibu kila mwezi.

 

“Si unaona hii,” alisema Bonta huku akitoa kitu kwenye waleti yake na kunionyesha! Ilikuwa ni hirizi kubwa nyekundu, akaniambia kwamba kila anapokwenda kwenye kazi ni lazima aichukue na huwa inamkinga sana kwenye matatizo.

 

Kiukweli mimi sikuwa naamini katika mambo ya ushirikina kwa hiyo nikawa namuitikia tu, yakiingilia kwenye sikio la kushoto na kutokea kwenye sikio la kulia. Tuliendelea na stori, mwisho tukafika pale kwenye lile jengo ambapo palikuwa kama na ofisi fulani hivi.

 

Tukaingia ndani ambapo kulikuwa na msichana mmoja aliyekaa mapokezi, akamsalimia Bonta kiheshima na kunitazama.

 

“Huyu ni mgeni eeh!”

“Ndiyo, ni mgeni kiasi lakini ni mwenzetu,” alisema Bonta, nikasalimiana na yule dada.

 

“Mdogo! Una miaka mingapi?” aliniuliza, nikamgeukia Bonta na kumtazama, nadhani hiyo ilitosha kumfanya aelewe kwamba sijapendezewa na swali lake.

 

“Siyo kwamba nakudharau, nimekuuliza kwa nia njema tu, mbona hata mimi ni mdogo, tena zaidi yako?” alisema yule msichana huku akijaribu sana kujenga mazoea.

“Mdogo wangu, wewe hujaoa na huyu naye hajaolewa! Muda wote anashinda amekaa tu hapo, kama vipi fahamianeni mi nakuja! Malizia kile nilichokukatisha kule Sinza,” alisema Bonta na kuingia kwenye vyumba vya ndani vilivyoonesha kuwa na watu.

 

“Unaitwa nani!”

“Kwani we unaitwa nani?”

“Mh! Mbona umekaa kisharishari hivyo jamani, Mungu amekuumba bonge la ‘hendsamu’ halafu unajiharibu, hata hupendezi,” alisema yule msichana baada ya kuona namkazia.

 

“Do you smoke?” aliniuliza msichana huyo huku akitoa sigara kwenye pakti, akaiweka mdomoni na kuiwasha. Kiukweli nilibaki nimepigwa na butwaa, kwa mwonekano wake sikudhani kama anaweza kuvuta sigara hadharani, nikatingisha kichwa kuonesha kwamba sivuti.

 

Akahama kule alikokuwa amekaa na kusogea pale nilipokuwa, nadhani alifanya makusudi ili anioneshe shepu yake ambayo ilikuwa imejengeka vizuri kwelikweli, akawa anaendelea kutoa moshi kwa fujo.

 

“Unajua namna ya kuitumia hii,” alisema huku akitoa bastola yake kiunoni na kuninyooshea. Unajua bado nilikuwa nazidi kujiuliza maswali mengi yasiyo na majibu, nimamtazama usoni kwa lengo la kutaka kujua nia yake maana tulishafundishwa kwamba mtu akishika bunduki, unatakiwa kuwa makini sana kumsoma machoni.

 

Nilichokifanya, niliipokea ile bastola, nikaiinua juu, nikaikoki na kuchomoa ‘magazini’, risasi zikamiminika chini, nikawa nazidaka na kuziweka vizuri. Niliamua kutumia mbinu hiyo kumuonesha yule msichana kwamba mimi siyo wa mchezomchezo maana alishaanza kama kuniletea dharau.

Nilizirudisha risasi na kuikoki, kisha nikamrudishia, akawa ananitazama machoni huku akitabasamu.

 

“Nini kilichokufanya ukaingia kwenye hii kazi!” aliniuliza swali ambalo sikulitegemea, nikamtazama, naye akanitazama, tukawa tunatazamana.

 

“Kwani wewe ni nini kilichokufanya ukaingiakwenye hii kazi?”

 

“Kazi gani? Mimi hapa ni receptionist, mtu wa mapokezi. Kwani kuna ubaya wowote mtu kufanya kazi hii?”

“Receptionist? Wewe ni receptionist?” nilimuuliza huku nikiwa namtazama machoni. Dawa ya mtu anayedanganya ni kumtazama machoni, kwa hiyo kitendo cha mimi kumkazia macho, kilimfanya apoteze pozi, akakwepesha macho yake na kuanza kucheka.

Alikuwa akitaka kuniletea uongo wa waziwazi, bila shaka sote tunawafahamu wale watu wanaofanya kazi mapokezi au kwa kiingereza receptionist. Eti alitaka kuniaminisha kwamba yeye ni mtu wa mapokezi tu, wakati muda mfupi uliopita alinitolea bastola na kuniuliza kama najua kuitumia.

 

Inawezekanaje mtu wa mapokezi akawa na bastola kiunoni?

 

“Anyway tuachane na hayo, mi naitwa Kezia, wengi wamezoea kuniita Lady Keys, nafurahi kufahamiana na wewe,” alisema huku akinipa mkono, na mimi nikanyoosha mkono wangu na kumpa.

 

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia: www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com ,  Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online. Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

 

 

Leave A Reply