The House of Favourite Newspapers

Sinema Nzima Mzee Kilomoni Alivyochotwa na Polisi Dar

JESHI la Polisi jijini Dar jana lilimkamata aliyekuwa mdhamini wa Klabu ya Simba, Hamis Kilomoni, ambaye alihojiwa kwa muda katika kituo cha Oysterbay kwa kosa la kuitisha mkutano na waandishi wa habari nyumbani kwake bila kuwa na kibali.


Mzee Kilomoni aliitisha kikao na waandishi wa habari jana, nyumbani kwake Kinondoni Biafra kwa lengo la kufafanua juu ya kauli ya uongozi wa Klabu ya Simba chini ya Mtendaji Mkuu, Crescentius Magori ambaye aliweka wazi hivi karibuni kuwa Kilomoni siyo Mdhamini wa Simba.

 

Sakata zima la kukamatwa kwa mzee Kilomoni lilianzia baada ya Katibu wa Baraza la Wazee wa Simba, Shaweji Macho ya Mzungu kuanza kuzungumza katika mkutano huo.

Macho ya Mzungu alieleza: “Sisi kama wazee tunamtambua Hamisi kama mdhamini ambaye ni miongoni mwa waasisi na mdhamini wa klabu, waasisi rasmi wa Simba walianza tangu mwaka 1929 wakati huo ilikuwa ikiitwa Old Boys, kazi ya kwanza ya waasisi ilikuwa kulinda jina, nembo ya klabu na kazi ya pili kulinda mali zinazohamishika na zisizohamishika.

 

“Taasisi rasmi iliundwa mwaka 1968, baada ya kupata ruhusa kutoka wa wadhamini na kuamua kuitisha kikao kwa makundi manne ambayo ni wanachama, viongozi, wachezaji na wazee wa klabu. Baada ya kupata hati ya viwanja, waliamua kuanzisha ujenzi wa jengo la Simba.

“Katika makundi hayo, Kilomoni alikuwa mmojawapo katika kundi la wachezaji na alipewa ukatibu katika mchakato wa ujenzi wa jengo la Simba, walitambuliwa kipindi hicho na mpaka leo ni wanachama wa kudumu wa Simba, hakuna atakayewaondoa wala atakayeondoka na ndiyo waanzilishi wa mali za Simba.

“Walitambulika kwa mujibu wa katiba ya kipindi kile ambayo haikuguswa hadi mwaka 1988, hati ya majengo ya Simba ni mali ya waasisi na si ya viongozi wala mtu mwingine, waasisi wanarithiwa na wanakuwa karibu, wazee na wadhamini wanapewa haki ya kumiliki hati, maamuzi ya kutoa hati ni ya sisi ambao tuliojenga na si viongozi wa klabu ambao wanaingia na kutoka, sijawahi kuona mtu anamkodisha nyumba mtu mwingine kisha anampatia
hati, hii ni mpya kwetu.

 

“Tangu mwaka 1929 ilipoanzishwa klabu hakukujengwa jengo lolote hadi ilipofika mwaka 1968 ndipo mchakato wa ujenzi ulivyoanza baada ya makundi manne kukubaliana.

 

Wadhamini waliokuwemo huko nyuma mzee Abdullahabi Maziwa ndiye aliyekuwa wa kwanza kuwa mdhamini wa klabu ya Simba, ni maajabu kuona hati apewe mwekezaji.

 

“Ilipofika mwaka 1975, Ramadhani Kilundu aliamua kuweka utarajibu wa kuwasainisha wadhamini rasmi kwa dhumuni la kulinda na kutunza mali za Simba ambao hawakubadilishwa hadi ilipofikia mwaka 2011, Machi 24 ndipo Kilomoni na Rameshi Katel walipokabidhiwa baada ya baraza la wazee kupitisha.

 

Kwa mujibu wa katiba yetu, mdhamini hawezi kuondolewa hadi kuwepo kwa sababu maalumu ambazo ni awe amechanganyikiwa, anaumwa hawezi kufanya kazi au awe amefariki,” alimaliza.

 

Kabla ya Mzee Kilomoni kuanza kuzungumza, difenda la polisi lilifika nyumbani kwa mzee huyo wakimtaka aende katika Kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar, jambo ambalo alilitekeleza ambapo aliondoka majira ya saa 6:10 mchana na kurejea saa 7: 02 mchana na kuwaeleza wanahabari juu ya kile kilochotokea.

 

Akizungumzia juu ya kukamatwa kwake na polisi, Mzee Kilomoni alisema: “Nashangaa kwa nini leo wamekuja kunikamata, kwa kuwa nimefanya mkutano hapa, bila tatizo lolote.

 

“Nitafuata taratibu zote kama polisi walivyonielekeza, wamenitaka niandike barua ya kuomba kuitisha mkutano na waandishi, nitafanya hivyo ndani ya muda mfupi nitaeleza kile nilichokikusudia.”

 

Kabla ya kumaliza kutoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari juu ya kile alichokwenda kuhojiwa, polisi walifika tena eneo hilo majira ya saa 7:14 ili kuhakikisha kama ametekeleza agizo lake.

Comments are closed.