The House of Favourite Newspapers

SIRI CORONA KUTESA WANAWAKE WACHACHE YAFICHUKA

0

TANGU ugonjwa wa COVID -19 ubishe hodi nchini China Desemba 31 mwaka jana, idadi ya wanaume wanaofariki kwa ugonjwa huo unaosababishwa na Virusi vya Corona ni mara mbili zaidi ya wanawake waliofariki dunia hadi sasa.  Hadi kufikia Machi 29 mwaka huu, watu 680,746 waliokuwa wameambukizwa ugonjwa huo, ambapo kati yao watu 31,920 walifariki na watu 146,396 walipona kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani.

Hata hivyo, ripoti mbalimbali zimeonesha kuwa, wanaume waliofariki ni asilimia 4.7 ikilinganishwa na asilimia 2.8 ya wanawake waliofariki kutokana na ugonjwa wa COVID-19.

TAFITI ZINAVYOONESHA

Kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Afya Duniani iliyotolewa na Taasisi ya Global Health na kupewa jina la Global 50/50, zaidi ya asilimia 50 ya vifo vitokanavyo na Corona duniani, ni wanaume.

Marekani ambayo inaongoza kwa maambukizi duniani kwa kuwa na watu 123,781, inaonesha katika jimbo la Florida pekee asilimia 60 walioambukizwa ni wanaume na asilimia 40 ni wanawake, lakini asilimia 70 ya vifo ni wanaume huku wanawake wakiwa ni asilimia 30.

Hali hiyo ilionekana China ambapo uchambuzi timu ya wanasayansi kutoka nchini humo, ulionesha kiwango cha vifo kwa wanaume ni asilimia 2.8 kwa wanaume ikilinganishwa na asilimia 1.7 kwa wanawake.

Huko Italia, imehesabiwa kuwa wanaume waliofariki kwa COVID-19 ni asilimia 71, wanawake asilimia 29. Italia ndio inaongoza kwa vifo duniani kwa kuwa na 10,023 hadi kufikia Machi 29 mwaka huu. Nchini Uhispania, utafiti uliotolewa na Taasisi ya Carlos III Health Institute (ISCIII), wiki iliyopita ulionyesha idadi ya wanaume wanaokufa ni mara mbili ikilinganishwa na wanawake.

Katika visa 16,000 vya Corona vilivyoripotiwa, kati yake vifo 566 vilitokea ambapo takwimu zilionesha asilimia 52 wanaoathiriwa pakubwa ni wanaume kuliko wanawake, kwamba wanaume 376 walifariki ikilinganishwa na wanawake 190.

KWA NINI WANAUME WAKO HATARINI ZAIDI?

Akizungumza na UWAZI, Daktari kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Sadick Sizya alisema hali hiyo inasababishwa na vitu kadhaa ambavyo ni mtindo wa maisha, sababu za kibaolojia na kimazingira.

Alisema mtindo wa maisha unatokana na ukweli kwamba wanaume ndio watendaji wakubwa wa shughuli nyingi za kila siku, hivyo wanakuwa kwenye hatari kubwa ya kupatwa na maambukizi. “Lakini pia hupenda kujumuika pamoja na jamii, kwa mfano kwenye viwanja vya michezo, vijiwe vya kahawa, kwenye magazeti, baa na sehemu nyingi za starehe,” alisema.

Hoja hiyo ya Dk. Sizya iliungwa mkono na Mkurugenzi wa Taasisi ya UCL Centre for Gender and Global Health, Profesa Sarah Hawkes iliyofanya utafiti huo kwa niaba ya WHO. Alisema mtindo wa maisha umekuwa ukibadilishwa katika mataifa yote, lakini wanasayansi bado hawawezi kufahamu sababu hiyo ya vifo vingi kuwa vya wanaume pekee.

“Inaonesha wazi kuwa ugonjwa wa Covid-19 unabagua kwa umri na kwa hali za kiafya. Lakini imekuwa ikionekana kuwa pia unabagua kwa jinsia ya kiume kwa sababu, wanaume waliokutwa na virusi hivyo ndio waliofariki zaidi ikilinganisha na wanawake,” alisema.

Alisema tafiti za taasisi hiyo zilionesha kuwa wanaume wengi waliofariki kwa Corona ni wale wenye umri kuanzia miaka 70.

“Kwa sababu mfumo kinga wa wanaume huzidi kuwa dhaifu kutokana na mtindo wa maisha wakati wanaendelea kuufikia uzee,” alisema. “Jibu la kweli, hakuna mmoja wetu anayejua nini husababisha tofauti hii,” alisema Prof. Hawkes. Alisema uvutaji wa sigara umeonekana kuwa mojawapo ya chanzo kikuu cha vifo vingi kwa wanaume.

Alisema huko China, zaidi ya asilimia 50 ya wanaume wanavuta sigara ikilinganishwa na asilimia mbili ya wanawake. Kwa hiyo, tofauti za kiafya kati yao zinadhihirishwa na afya ya mapafu ambayo kwa asilimia kubwa, wanaume ndio wameathiriwa na moshi wa sigara.

Hoja ya kuvuta iliungwa mkono na utafiti uliochapishwa Februari 28 mwaka huu na timu ya wachunguzi wa tabia za Corona nchini China ambapo ilionesha kuwa asilimia 12 ya wavutaji sigara walipatwa na virusi vya Corona huku asilimia 26 waliishia kufariki au kuwa katika hali ya mahututi.

Ripoti hiyo ilisema uvutaji sigara pia inaweza kutumika kama njia ya kuambukizwa mara ya kwanza kwani wavutaji sigara hugusa midomo yao zaidi na wanaweza kutumia sigara iliyosheheni virusi hivyo.

Italia, karibu asilimia 28 ya wanaume na wanawake asilimia 19 ni wavutaji. Tofauti hizo hazipo karibu kabisa kama ilivyo nchini China. Lakini wanaume wanaendelea kuathiriwa zaidi ya Corona.

SUALA LA TABIA KUTOFAUTIANA KIJINSIA

Uchunguzi timu hiyo ya wanasayansi kutoka China walisema kuwa, wanaume hawana desturi ya kunawa mikono kwa kutumia maji safi na sabuni sambamba na kutafuta huduma za kitabibu kwa kuwa tu na hulka ya kudharau sana huduma za afya.

SABABU ZA KIBAIOLOJIA

Hata hivyo, kuna imani inayokua miongoni mwa wataalam kwamba, sababu za msingi zaidi za kibaiolojia pia zinahusika.

“Wanawake wana mfumo kinga ndani ya miili yao wenye uwezo wa kukabiliana na magonjwa mbalimbali ikilinganishwa na wanaume. Wanawake wana uwezekano mkubwa wa kuathiriwa zaidi na magonjwa sugu ya mwili kama kansa, kisukari, moyo na kuna ushahidi mzuri kwamba wanawake hutoa seli askari bora kwa chanjo dhidi ya mafua au homa,” alisema Prof Paul Hunter, kutoka Chuo Kikuu cha East Anglia.

Utafiti mwingine uliofanywa na Profesa Sabra Klein kutoka taasisi ya Johns Hopkins Bloomberg School of Public Health, Marekani alisema: “Uchunguzi unaonesha kuwa vifo vingi ni vya wanaume katika nchi za China, Italia na Uhispania. Tunaona hii licha ya kuwa na tamaduni tofauti.

“Wakati ninapoona hivyo, inanifanya nifikirie kwamba lazima kuwe na kitu kwa wote kinachochangia hii. Sidhani kama sigara ndio sababu inayoongoza.” Tafiti za awali, pamoja na ule wa Klein, umebaini kuwa wanaume wanayo kinga ndogo ya asili ya magonjwa ya kuambukiza kama vile homa ya ini (Hepatitis C) na Virusi Vya Ukimwi (VVU).

“Sifa ya miili ya wanaume inaonesha kuwa kinga haiwezi kuwa na mwitikio mzuri katika kuanza mapambano dhidi ya virusi vipya. “Homoni inaweza pia kuwa sababu ya wanaume kufariki zaidi, homoni ya Oestrogeni imeonyesha kuzipa nguvu zaidi seli za kinga mwilini.

Aidha jeni nyingi ambazo husimamia mfumo wa kinga zimewekwa kwenye kundi la chromosome ya X (ambayo wanaume wana moja, na wanawake wana mbili) na kwa hivyo, inawezekana kwamba jeni zingine zinazohusika katika mwitikio wa kinga zinafanya kazi zaidi kwa wanawake kuliko kwa wanaume.

“Tofauti za kijinsia katika mwitikio wa kinga dhidi ya Covid-19 zinaweza kuonekana kwenye uchunguzi wa mfumo kinga ambao unaendelea ulimwenguni kote,” alisema Prof. Klein.

Klein alisema tayari amekagua tafiti za jambo hilo kutoka kwa timu ya wanasayansi waliopo nchini China, ambazo zimechukua sampuli za damu kutoka kwa wagonjwa wakati wote wa maambukizo. “Tunaweza kutarajia zaidi juu ya hili hivi karibuni,” alisema.

Mwishowe, Hawkes alisema, baiolojia, mtindo wa maisha na tabia zote zinaingia katika kuleta majibu ya utofauti huo wa vifo kati ya wanaume na wanawake.

Alisema inasikitisha kuona kuwa ni nchi sita tu kati ya 20 ambazo hadi sasa zimechapisha ripoti ya idadi ya kesi na vifo, kulingana na takwimu zilizoandaliwa kwenye ripoti ya Shirika la Afya duniani iliyopewa jina la Global Health 50/50.

WALIOAMBUKIZWA CORONA TANZANIA WAFIKIA 19

Aidha, katika hatua nyingine Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema wagonjwa wa COVID-19 nchini wamefikia 19, baada ya watano kuongezeka jana. Taarifa iliyotolewa na waziri huyo Machi 30 mwaka huu, imeeleza kuwa wagonjwa hao watano walifanyiwa vipimo katika maabara kuu ya Taifa.

“Kati ya wagonjwa hawa, watatu ni kutoka Dar es Salaam na wawili kutoka Zanzibar ambao taarifa zao zimetolewa na Waziri wa Afya Zanzibar. “Hivyo, sasa jumla ya wagonjwa wa Corona ni 19 akiwemo mgonjwa mmoja aliyetolewa taarifa na Waziri wa Afya Zanzibar Machi 28, 2020,” alisema.

Kuhusu taarifa za wagonjwa wapya wa Dar es Salaam, Ummy alisema mwanaume mwenye miaka 29 Mtanzania, alikutana na raia wa kigeni kutoka miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi. “Mwanamke mwenye miaka 21 Mtanzania ambaye ni miongoni mwa watu waliokuwa wakifuatiliwa. “Mwanaume mwenye umri wa miaka 49, Mtanzania ambaye pia ni miongoni mwa watu waliokuwa wakifuatiliwa.”

Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa kazi ya kufuatilia watu wote wa karibu waliokutana na wagonjwa hao inaendelea, kuwataka watu kuendelea kuchukua tahadhari ili kujikinga na ugonjwa huo ambao hadi jana, watu zaidi ya 34,843 wameripotiwa kufariki kwa ugonjwa huo.

Leave A Reply