The House of Favourite Newspapers

Siri Misikiti, Shule za Kiislamu Kuungua Moto

0

MFULULIZO wa matukio ya ajali za moto katika misikiti na shule mbalimbali za Kiislamu jijini Dar es Salaam, yamewatikisa viongozi wa dini hiyo na kuamua kutafuta majibu ya maswali yatokanayo na matukio hayo ambayo vyanzo vyake havijafahamika. UWAZI linaripoti.

 

Hatua hiyo imekuja baada ya kutokea ajali tatu za moto katika kipindi cha mwaka huu ambazo licha ya kusababisha hasara ya vitu na mali mbalimbali, pia zimegharimu uhai wa wanafunzi watatu.

Ajali hizo zimetokea katika kipindi cha mwezi huu pekee, hali ambayo mbali na kuzua hofu, pia imeibua hisia tofauti kwa waumini wa dini hiyo na Watanzania kwa ujumla.

 

JULAI 18, 2020

Katika tukio mojawapo la hivi karibuni ambalo lilishtua pakubwa jamii ya Kiislamu, ni ajali ya moto ambayo iliunguza sehemu ya Shule ya Mivumoni Islamic Seminary iliyoko ndani ya Msikiti wa Mtambani, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

 

Mwalimu wa shule hiyo, Mariki Balongo, alisema moto huo ulianza muda wa saa 9:30 asubuhi, Julai 18, 2020 katika stoo ya shule hiyo.

Katika ajali hiyo, hakuna mwanafunzi aliyeathirika na tukio hilo, bali baadhi ya vifaa vya shule na vya wanafunzi, viliteketea kwa moto.

 

Hata hivyo, Balongo alisema chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.

“Ni kweli moto ulitokea sehemu ya stoo ya shule, ulianza saa tatu na nusu asubuhi. Hakuna mwanafunzi aliyedhurika, lakini baadhi ya vifaa viliungua.

“Chanzo cha moto hakijulikani ni nini hadi sasa. Na sidhani kama itakuwa umeme sababu kwenye hiyo stoo, hakuna swichi zaidi ya taa ambayo swichi yake iko nje,” alisema Balongo.

 

JULAI 17, 2020

Tukio kama hilo, pia lilitokea katika Shule ya Sekondari ya Kinondoni Muslim ya jijini Dar es Salaam na kuteketeza baadhi ya vitu vya wanafunzi.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kinondoni, Shamba Vicent Muhepwa, alisema madarasa 11 kati ya 15 ya shule hiyo, yaliteketea kwa moto.

 

Mbali ya madarasa hayo, vifaa na samani za shule hiyo, pia viliteketea kwa moto huku walimu na wanafunzi wote wa shule hiyo wapatao 218 wakisalimika.

Alisema moto huo ulianza muda wa alasiri wakati shughuli za kila siku zikiendelea, akaongeza kuwa walifanikiwa kuwaokoa wanafunzi wote zaidi ya 200 na kati yao, wawili walijeruhiwa na kupelekwa hospitali.

 

Hata hivyo, chanzo cha moto huo hakijajulikana hadi sasa wakati uchunguzi wa Jeshi la Zimamoto ukiendelea.

 

JULAI 4, 2020

Mfululizo wa matukio hayo kwa mwezi huu, ulianza Julai baada ya moto kuzuka katika Shule ya Sekondari ya Kiislamu ya Ilala jijini Dar es Salaam na ulisababisha vifo vya wanafunzi watatu, huku ukiharibu mali za shule hiyo.

 

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi ambaye ni kamanda wa mkoa wa kipolisi wa Ilala; Zubari Chembela, alisema shule hiyo ya Ilala Islamic, iliyopo mtaa wa Arusha na Kasulu, inamilikiwa na Islamic Foundation Development (IFD) chini ya msikiti unaoitwa Masjid Shafi.

 

Moto ulioanza muda wa saa nane usiku, ulitokea kwenye moja ya hosteli wanapokaa wanafunzi wa kiume huku chanzo cha moto hadi sasa hakijafahamika.

 

MEI 17, 2016

Hii ni mara ya pili moto kuibuka katika shule hiyo ya Ilala kwa kuwa mwaka 2016, kulitokea ajali kama hiyo ambayo hadi leo chanzo chake bado hakijaweza fahamika mara moja.

 

Vilevile katika Msikiti wa Mtambani, nako pia kulitokea ajali ya moto Agosti, 2014 na kuuteketeza huku chanzo chake kikiwa hakijulikani hadi sasa.

 

VIONGOZI WANASEMAJE?

Aidha, kufuatia mfululizo wa matukio hayo, Mkuu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu nchini, Shehe Mussa Kundecha, alisema mfululizo wa matukio hayo umewashtua sana.

 

“Kwa sababu Ilala imerudia mara mbili, Mtambani imerudia mara mbili, Kinondoni Muslim ni mara ya kwanza,” alisema na kuongeza kuwa, kutokana na hali hiyo, sasa wanaangalia chanzo cha matukio hayo yanayoathiri misikiti na taasisi za Kiislamu.

 

“Kwa sababu kumekuwa na misigano kati ya shughuli za kidunia na vituo vyetu vya kidini. Kwa hiyo, tunafanyia kazi vitu vya aina mbili; kwanza kukaa na viongozi wetu kuelimishana juu ya jambo hili, pili tumefanya mpango wa kuomba watu wa jeshi la zimamoto ili tukae nao kufanya semina kuhusiana na vyanzo vya moto na sababu zake ili tuvipe somo vituo vyetu,” alisema.

 

Alisema wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa maeneo ya misikiti, tahadhari za moto zipo kwa sababu ni sehemu ambayo watu wanaingia na kutoka.

 

“Lakini hicho kipindi cha kuingia na kutoka, kunaweza kutokea jambo, na tunafikiri kuna haja ya semina hizi ili kuongeza tahadhari za kuzuia moto.

 

“Lakini pia kama ilivyo kwenye mahoteli, kuna vifaa vya kuzuia moto, lakini bado kwenye majumba yetu ya ibada na shule, hayajajengwa kwa mfumo huo. Kwa hiyo, tunajaribu kuyaona haya mapungufu ili tuone wataalam watakachotushauri, tunaweza kuyamaliza kwa namna gani,” alisema.

 

NI HUJUMA?

Shehe Kundeka alisema, kwa sasa haiwezekani kusema moja kwa moja kuwa kuna hujuma kutokana na mfululizo wa matukio hayo kwa sababu misikiti na taasisi hizo zinaonesha bado hazina mifumo thabiti ya kudhibiti moto.

 

“Usimlaumu anayekutilia shaka, angalia ulipokaa, ukikaa mahali panapotia shaka usimlaumu anayekuangalia vibaya, lakini kama tukiwa na tahadhari zote, ni rahisi sasa kwenda kunakofuata, kwa hiyo tusikimbilie hujuma kwanza.

 

“Kwa mfano kule Ilala, huko zamani kulikuwa na msigano wa makundi ya msikiti, basi dhana ya matukio ya moto ikaenda huko sana, kwamba itakuwa hujuma kutokana na makundi hayo yanayotofautiana, lakini sio vizuri kulemaa na ugonjwa huo wa hujuma.

 

“Tusitafsiri kuwa ni hujuma moja kwa moja kwa sababu watu wanaotumia magari ndani yake, wana fire extinguisher, lakini ikitokea tatizo, hawezi kutumia,” alisema.

 

Hoja ya Shehe Kundecha iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Shehe Hamis Mataka ambaye naye alisisitiza kuwa kuhusu uchunguzi wa matukio hayo, wanasubiri matokeo ya uchunguzi wa vyombo vya usalama.

 

“Tunasubiri wakamilishe uchunguzi wao wa kitaalamu ili tujue tuanzie wapi. Kwa sababu uchunguzi ukikamilika, utaondoa dhana zinazoibuka,” alisema Shehe Mataka.

STORI: MWANDISHI WETU, DAR

Leave A Reply