SIRI ZA WEMA KUKONDA ZAVUJA !

DAR ES SALAAM: Jamani kwani Wema ana nini lakini? Ni sehemu ya kauli za mshtuko za baadhi ya mashabiki wa staa mkubwa wa sinema za Kibongo, Wema Isaac Sepetu, wenyewe wanamwita Tanzania Sweetheart.  Baadhi ya mashabiki hao wameonesha kushtushwa na afya ya Wema wao ambapo nyuma yake kuna siri nzito ambazo Risasi Mchanganyiko limedokezwa. Kwa muonekano wa sasa, Wema amekonda hivyo kupoteza kabisa ile shepu yake matata na kuwa na muonekano wa kitoto kama enzi zile anashiriki Shindano la Miss Tanzania mwaka 2006/07, akiwa chini ya umri wa miaka 18.

SIRI YA KWANZA

Kwa mujibu wa watu wa karibu wa Wema, mashabiki watakumbuka kuwa mwezi Julai, mwaka huu zilivuja habari za mwanadada huyo kufanyiwa oparesheni ya kupunguza mwili. Katika taarifa hizo pia ilidaiwa kuwa Wema alikatwa sehemu ya utumbo mpana (mkubwa) katika zoezi hilo la kujipunguza mwili lililofanyika nchini India, jambo ambalo mwenyewe alilipinga kwa nguvu zote.

Vyanzo hivyo vilidai kuwa, hiyo ni moja ya siri za kukonda kwa Wema kwani oparesheni za aina hiyo huwa hazitoi majibu haraka na hicho ndicho kilichotokea kwake.

“Huwa inachukua takriban miezi mitatu na kuendelea ndipo mabadiliko yanaanza kuonekana. “Mwanzoni (Wema) alikuwa anakanusha na kusema alikuwa anafanya sana mazoezi ya ‘gym’ na dayati, lakini sasa hivi kila kitu kipo wazi. “Jambo pekee linaloweza kusababisha mtu akakonda kwa kiasi cha Wema wa sasa ni oparesheni tu, hakuna kingine,” kilidai moja ya vyanzo hivyo. 

INAWEZEKANAJE?

Kwa mujibu wa daktari aliyezungumza na Risasi Mchanganyiko juu ya afya ya Wema aliyeomba hifadhi ya jina, njia hiyo ya kupunguza unene ambayo wengi huijua kama kukatwa utumbo kitaalam hujulikana kwa jina la Gastric Band. Alisema kuwa, katika njia hii, sehemu ya tumbo la binadamu inabanwa ili kulipunguza ukubwa na kuruhusu kiasi kidogo cha chakula kuingia.

“Ni njia ya kitaalam ya kupunguza unene, kinachofanyika ni kupunguza ukubwa wa tumbo kwa kulibana katika sehemu ya juu ili mtu anapokula chakula kidogo tu ajisikie ameshiba. “Hali hiyo humfanya kadiri siku zinavyokwenda kupungua unene,” alisema daktari huyo na kuongeza: “Ni njia inayoshauriwa kidaktari ya kupunguza unene, lakini mbali na faida hiyo, kuna madhara yanayoweza kuwapata wanaofanya uamuzi huu.

MADHARA YAKE

“Kwa mfano, lengo lako linaweza kuwa ni kupungua, lakini sasa ukakonda kupitiliza, hali ambayo pia kiafya siyo sawa. “Lakini pia, tiba hii ya kupunguza unene inafanyika kwa kufanyiwa upasuaji ambapo damu nyingi inaweza kupotea na kusababisha madhara makubwa.

“Matatizo yanayoweza kusababishwa na njia hii ya upasuaji ni mwili kupata mzio (allergy), kupata matatizo ya kupumua, damu kuganda kwenye miguu na kwenye mapafu, kuishiwa damu, kupata maambukizi kwenye damu na kupatwa na shambulio la moyo au kiharusi baada ya kumalizika kwa upasuaji. “Pia kunakuwa na kifaa maalum ambacho mtu huwekewa tumboni baada ya upasuaji, kinaweza kuhama sehemu kilipowekwa au kikayeyuka na kusababisha madhara kwa mhusika ambapo atalazimika kufanyiwa upasuaji tena.

“Utafiti unaonesha kwamba, kati ya asilimia 15-60 ya watu waliofanyiwa upasuaji huu, hulazimika kufanyiwa upasuaji mwingine ili kurekebisha dosari zilizotokea awali. “Baada ya upasuaji, mhusika anatakiwa kufuata masharti ya vyakula, vinginevyo atatapika na kupatwa na tatizo la kutanuka kwa koo. Pia kifaa kinachoachwa tumboni, kinaweza kusababisha majeraha ya tumbo na viungo vingine vya ndani.”

SIRI YA PILI

Kama mtakumbuka, wiki kadhaa zilizopita Wema alikumbwa na skendo nzito ya kusambaa kwa video na picha zake za kimahaba akiwa na mwanaume aliyemtambulisha kama mumewe mtarajiwa (future husband) aliyejulikana kwa jina la Patrick Christopher ‘PCK’. Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, jambo hilo lilimfedhehesha mno Wema ambapo alilazimika kuomba radhi, lakini bado anakabiliwa na kesi hiyo kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar.

Ilidaiwa kuwa, Wema ambaye alikuwa ameapa kuwa mtu bora kwenye jamii ili kujijenga kisiasa, alijikuta akichafuka kwa mara nyingine hivyo kumsababishia msongo wa mawazo.

“Ile ishu ilimfedhehesha sana Wema hasa pale alipotakiwa kuomba radhi na kufungiwa kujihusisha na kazi yake ya filamu hadi Aprili, mwakani. “Lakini mbali na skendo hiyo kulikuwa na madai mengine kuwa yule jamaa alimtapeli Wema mamilioni ya pesa kwa kumdanganya kuwa alitaka wafanye biashara pamoja kisha akaingia mitini.

“Pia kutokana na ishu hiyo, jambo lingine lililomsononesha na kumpa mawazo ambayo huchangia mtu kukongoroka ni kutakiwa kukutana na makundi ya watu 500 kwa gharama zake mwenyewe kisha kuwaeleza mambo yake mazuri ambayo wanapaswa kutarajia kutoka kwake,” kilitiririka chanzo kingine.

SIRI YA TATU

Ishu nyingine inayodaiwa kumsumbua Wema ni juu ya kupata mimba ambayo kwa mujibu wa jamaa huyo anayejiita mchumba wa staa huyo (PCK), anayo na ndiyo inamfanya kuwa hivyo alivyo.

Hivi karibuni jamaa huyo aliibuka na kuanika mazito kuwa Wema ana ujauzito wake. PCK alijinadi kuwa yeye ndiye atakuwa mwanamume wa kwanza kumpa mimba kwa kipindi chote ambacho Wema amekuwa akitafuta mtoto. Jamaa huyo alilieleza Risasi Mchanganyiko kuwa, kwa sasa ameshamuomba samahani mkewe wa ndoa, lakini alikubaliana na Wema kuwa atakuwa akimtunza mtoto.

“Mimi kwa sasa nimeamua kurudi kwa mke wangu kwa maana nimemuomba msamaha na amenikubalia hivyo kwa upande wa Wema, kwa vile ana mimba yangu, mimi niko tayari kumtunza mtoto,” alidai PCK ambaye pia ni msanii wa Bongo Fleva. Jamaa huyo aliendelea kufunguka kuwa, yeye na Wema, wanaendelea kuwasiliana vizuri tu na hakuna shida kati yao ila wapambe wa pembeni tu ndiyo wamekuwa wanaleta shida.

Alisema kuwa watu wamekuwa wakidai kuwa alikamatwa, jambo ambalo si kweli kwani yeye yupo wala hajakamatwa na hatakamatwa kamwe. “Ninawashangaa sana watu. Mimi na Wema tunaendelea kuwasiliana vizuri tu, bila matatizo yoyote yale, ila kuna wapambe ndiyo wanaleta shida, lakini sisi tuko poa,” alidai PCK.

WEMA ANASEMAJE?

Kufuatia mambo hayo yote, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Wema bila mafanikio, lakini likampata meneja wake, Neema Ndepanya. Alipoulizwa juu ya mambo hayo yanayozungumzwa kuhusu Wema na madai ya PCK kuwa ana mimba yake, Neema alisema kuwa katika vitu vya kuachana navyo ni huyo mwanamume kwani anahisi hana akili nzuri na anataka kuendelea kupata kiki kupitia jina la Wema ambaye hawezi kukubali hilo litokee.

“Huyo (PCK) nafikiri hayuko sawa kiakili hata kidogo na anachofanya anataka kutafuta kuendelea kupata kiki kupitia jina la Wema. “Sisi hatuko tayari, kwanza kama yeye ni mwanaume kweli, basi ajitokeze hadharani,” alisema Neema na kuongeza:“Kwanza jamaa huyo anasakwa na Polisi.”

WEMA ANAPENDWA…

Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wa Wema waliozungumza na Risasi Mchanganyiko walisema, pamoja na kukonda na kupoteza shepu yake, lakini bado wanampenda hivyo alivyo.

Loading...

Toa comment