The House of Favourite Newspapers

SOMA HIYO..KAGERE, OKWI WAUA MWARABU TAIFA

SIMBA jana Jumamosi waliwaonyesha Waarabu JS Saoura kuwa wao sio wa mchezomchezo baada ya kuwazamisha kwa mabao 3-0. Simba ambao walikuwa katika uwanja wa nyumbani wa Taifa jijini Dar es Salaam walianza vizuri kwenye mechi yao ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku ikitoa onyo kwa timu zote katika michuano hiyo.

 

Mabao ya Simba mawili yalifungwa straika Medie Kagere na jingine Emmanuel Okwi, Bao la kwanza la Simba lilifungwa dakika ya 45 ikiwa ni muda mfupi kabla ya mapumziko baada ya Okwi kuwapangua mabeki wa Saoura kabla ya Kagere kuongeza msumari wa pili katika dakika 51 kipindi cha pili.

Dakika ya 67, Kagere alionyesha umahiri wake tena kwa kuchopu mpira na kufunga bao la akili mingi ambalo liliwaongezea maumivu
mabeki wa Saoura.

 

Simba ambao wananolewa na Mbelgiji Patrick Aussems, walitawala kwa muda mrefu pambano hilo ambapo Saoura walicheza kwa tekniki yao ya kupoteza muda huku wakijiangusha muda mwingi. Simba ambao katika pambano hilo walimshuhudia straika wao John Bocco akitolewa uwanjani kipindi cha kwanza baada ya kupata maumivu na nafasi yake kuchukuliwa na fundi Kagere ambaye ni raia wa Rwanda, walianza wakiwa na imani ya ushindi kwa asilimia 100. Katika pambano hilo dakika za mwanzoni tu kiungo wao, Hassan Dilunga alikosa bao baada ya kupiga shuti ambalo lilitoka.

Dakika 18 Okwi alikosa bao la wazi baada ya kupiga shuti akiwa ndani ya 18 lakini hata hivyo liligonga mwamba na kurudi uwanjani kabla ya kuondolewa. Dakika ya 35, Simba walifanya tena shambulizi ambapo shuti kali la Okwi liliondolewa na kipa wa Waarabu hao ambaye jana alifanya kazi ya ziada lakini maji yakazidi unga. Simba walikosa mabao kupitia kwa Nicholaus Gyan na Jonas Mkude kwa nyakati tofauti.

 

Mara baada ya kipindi cha kwanza kumalizika kocha wa JS Saoura, Nagil Neghiz aliwavamia marefa na kulalamika juu ya bao ambalo walifungwa na Simba kiasi ambacho kilimfanya pia Aussems kuingia uwanjani.

ULIMWENGU APATA WAKATI MGUMU Mshambuliaji wa JS Saoura, Mtanzania, Thomas Ulimwengu alijikuta kwenye wakati mgumu katika mchezo huo kutokana na kuzomewa na mashabiki wa Simba alipoingia kipindi cha pili akitokea benchi. Licha kuzomewa na mashabiki hao, Spoti Xtra lilimshuhudia mchezaji huyo akicheka bila ya kuwajali mashabiki hao ambao walikuwa wakimzoea kabla ya kukaa kwenye benchi akitokea vyumbani.

 

Hali hiyo iliendelea dakika 57 kufuatia mchezaji huyo kuingia kuchukua nafasi ya Younes Koulkheir, ambapo mashabiki walilipuka kwa kelele za kumzomea Katika hatua nyingine jana Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa na Naibu Spika wa Bunge Tulia Atkson waliungana na mashabiki uwanjani hapo. Waziri Majaliwa aliingia dakika ya 51 ambapo alishuhudia bao la pili la Simba lililofungwa na Kagere, lakini Tulia alikuwepo kuanzia mwanzoni mwa mchezo huo.

MO ASHANGILIWA Mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ aliingia uwanjani majira ya saa 9:43 alasiri na kuibua shangwe uwanja mzima kwa mashabiki kumshangilia wakiimba jina lake. Kikosi cha Simba kilikuwa hivi; Aishi Manula, Nicholaus Gyan, Mohamed Hussein Tshabalala, Juuko Murshid, Paschal Wawa, James Kotei, Hassan Dilunga/ Muzamiru Yasin, Jonas Mkude, John Bocco/ Meddie Kagere, Emmanuel Okwi/Shiza Kichuya na Clatous Chama.

STORI NA SAID ALLY NA IBRAHIM MUSSA

Comments are closed.