The House of Favourite Newspapers

Stamico Yazidi Kupaa Kwenye Sekta Ya Madini

0
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Dk. Venance Mwasse (kulia) baada ya kuzindua kituo cha mafunzo kwa wachimbaji wadogo Itumbi – Chunya mkoani Mbeya. Wengine Mwenyekiti wa Bodi ya Stamico, Meja Jenerali mstaafu Michael Isamuhyo (wa pili kulia na Katibu Mkuu wizara ya madini, Profesa Simon Msanjila).

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limezidi kupaa kwenye sekta ya madini baada ya Wizara ya madini kushirikiana na shirika hilo kuzindua kiwanda kipya cha mfano cha uchenjuaji dhahabu kilichopo Itumbi- Chunya mkoani Mbeya.

 

Kiwanda hicho ambacho ni kituo mfano cha mafunzo kwa wachimbaji wadogo, ni muendelezo wa Shirika hilo kuwafikia wachimbaji hao ili kuwapatia mafunzo yatakayowawezesha kuchimba kitaalamu zaidi.

Akizundua kituo hicho, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyogo aliipongeza Stamico kwa kudhihirisha kuwa ni shirika linalojiendesha kwa faida baada ya kuanza kutoa gawio kwa serikali ambapo mwaka 2019 ilitoa kiasi cha Sh bilioni moja na mwaka huu imetoa Sh bilioni 1.1.

 

Aidha, alisisitiza Stamico kuhakikisha wanatoa kipaumbele kwa wakazi wa maeneo jirani na kilipo kituo hicho ili waweze kunufaika na matunda ya kuwepo kwa mradi huu.

Pia alitoa wito kwa wachimbaji wadogo wa Itumbi na maeneo jirani kukitumia kituo hicho kujifunza na kupata taarifa mbalimbali kuhusiana na shughuli za utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji pamoja na biashara ya madini kwani kituo kimejengwa kwa ajili yao.

 

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Dk. Venance Mwasse alisema kituo hicho ni cha tatu kumilikiwa na Stamico baada ya vituo vya Katente (Bukombe) na Lwamgasa (Geita).

Alisema mafunzo yatakayotolewa kwenye vituo hivyo ni pamoja na utafutaji, uchimbaji, uchenjuwaji na biashara ya madini kupitia.

Alisema Stamico itaendelea kukuza uelewa wachimbaji kwa teknolojia rahisi na isiyokuwa na athari kwa afya na mazingira pamoja na majukumu mengine.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Stamico, Meja Jenerali mstaafu Michael Isamuhyo ameishukuru Serikali kwa namna ilivyoelekeza nguvu zake na fedha katika kuwasaidia vijana na kubainisha kuwa katika kipindi hiki vijana wanatazamwa kwa namna ya pekee katika kuharakisha maendeleo ya jamii.

Pamoja na hayo, Isamuhyo amebainisha kuwa wajibu wa Stamico kuwa ni pamoja na kufanya tafiti katika maeneo mbalimbali na kubaini mashapo yaliyopo na kutenga kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

“Katika kutekeleza hilo tayari shirika hilo limefanya tafiti 23 kati ya hizo zipo mkoani Chunya ambapo ni eneo la Itumbuli, Sangambi na Shoga,” alisema.

NA MWANDISHI WETU

 

Leave A Reply