The House of Favourite Newspapers

STARS LAZIMA KIELEWEKE TAIFA LEO

LUGHA rahisi unayoweza kutumia leo kuzungumzia mechi ya Taifa Stars ni kwamba tushinde yetu. Sisi tushinde mechi yetu na Uganda leo pale Taifa.

 

Matokeo ya mechi ya wengine tutayajua baadaye na tutajuana hukohuko mbele kwa mbele. Wikiendi iliyopita Simba walishinda yao dhidi ya AS Vita wakaweka historia. Sasa wako kwenye robofainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Kazi moja imekwisha sasa tunaingia kumaliza nyingine.

Lazima Uganda apigwe Stars ifuzu Afcon 2019
nchini Misri. Hakuna miujiuza inayoweza kuivusha Stars zaidi ya ushindi dhidi ya Uganda leo ambao tayari wao wameshafuzu.

 

MTIHANI ULIPO

 

Kwenye kundi L ilipo Stars, tayari Uganda imeshafuzu lakini bado limekaa kimtego sana. Stars inapaswa kushinda tu leo lakini itategemea na matokeo ya Lesotho na Cape Verde kwa vile Stars na Lesotho wana pointi 5 kila mmoja. Mtihani uko hivi; kama Stars akishinda na Lesotho akashinda ugenini. Tumelala.

 

Hatuendi kokote. Tutakuwa tumelingana pointi na Lesotho lakini yeye atakuwa na faida kubwa kwavile aliifunga Stars kwake na hata Dar es Salaam alipata sare ya bao 1-1 ambayo inambeba pia.

KIKANUNI

Timu zikifungana kwa pointi kinacho fuatwa kuangaliwa ni tofauti ya mabao timu hizo zilipokutana zenyewe kwa zenyewe. Kumbuka Lesotho ana faida aliipiga Stars kwake na akadroo Dar. Kingine kitakachoangaliwa ni matokeo yao kwenye mechi zao na vilevile idadi ya mabao mechi ugenini.

 

Hivyo Stars inapaswa kushinda kwanza mechi yake dhidi ya Uganda jioni hii halafu waombee Cape Verde amsimamishe Lesotho.

 

CAPE VERDE ATATUBEBA?

 

Hawezi kukubali kupoteza nyumbani kwavile hesabu za leo zinaweza kumbeba. Kama Cape Verde akishinda na Stars akipoteza kwa Uganda, Cape Verde atafikisha pointi saba na atafuzu. Hivyo atataka kushinda ili asubiri lolote linaloweza kutokea Tanzania na kama isipokuwa riziki itamsaidia kupanda kwenye viwango vya ubora. Mechi ya awali walitoka sare ya bao 1-1.

 

MZUKA WETU

 

Nahodha wa Tanzania, Mbwana Samatta amesisitiza kwamba leo hawataki kingine zaidi ya ushindi, hayo mengine watajua baadaye. Stars ina kikosi chake chote na kila mmoja
amesisitiza kwamba lazima kieleweke.

 

Kamati maalum ya saidia Stars ishinde imetenga dau dola 5000(zaidi
ya Sh.11milioni) kwa kila mchezaji kama timu ikishinda. Viongozi mbalimbali wa Serikali na
wadau wameungana kwa pamoja na kushinikiza kauli moja ya “zima TV twende uwanjani”.

 

UGANDA Ilikuwa kambini nchini Misri ikijiandaa na mchezo wa leo. Lakini wachambuzi wa soka nchini Uganda wanasema kwamba
timu yao ilikwenda Cairo kuzoea hali ya hewa na kujiandaa kisaikolojia kwa mechi za fainali.

Comments are closed.