The House of Favourite Newspapers

Taifa Stars Yatinga Afcon, Yaifunga Uganda Taifa

NI zamu yetu kufuzu Afcon 2019 baada ya miaka 39 kupita bila timu ya Taifa kufuzu kushiriki michuano ya Afcon hatimaye leo nguvu ya mashabiki imeonekana na morali ya wachezaji imekuwa juu.

Katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa leo Stars wamewatoa kimasomaso mashabiki wa Tanzania baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Uganda ambao tayari wao wamefuzu Afcon wakiwa na pointi 13 kwenye kundi L.
Kipindi cha kwanza Stars walianza kwa kasi ambapo dakika ya 21 waliandika bao la kwanza kupitia kwa mshambuliaji Simon Msuva akitumia pasi ya John Bocco na kufanya kipindi cha kwanza kukamilika kwa Stars kuwa kifua mbele kwa bao 1.
Kipindi cha pili, Erasto Nyoni aliandika bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 51 baada ya mchezaji wa Uganda kunawa eneo la hatari mpira uliopigwa na Mbwana Samatta.
Dakika ya 57 Agrey Morris aliandika bao la tatu baada ya kutumia pasi ya John Bocco akamaliza kwa kichwa matata na kufanya Stars kuwa mbele kwa mabao 3-0.
Ushindi huo unatoa nafasi kwa Stars kufuzu baada ya miaka 39 kwani kwenye kundi D kwa sasa wamefikisha pointi 8 huku Uganda ambao walitangulia mapema kufuzu wakiwa na pointi 13.
Mchezo ambao ulikuwa unatazamwa pia ulikuwa kati ya Lesotho na Cape Verde ambapo umekamilika kwa suluhu na kufanya Cape Verde kuwa na pointi 5 huku mpinzani wa Stars Lesotho akimaliza akiwa na pointi 6 akiwa nafasi ya 3.
Afcon 2019 ni zamu yetu kwenda Misri baada ya ushindi huo, mshikamano na umoja kwa wachezaji pamoja na mashabiki umeonyesha namna halisi ya uzalendo.
PICHA NA MUSA MATEJA ~ GPL

Comments are closed.