The House of Favourite Newspapers

TAJIRI KORTINI KWA KUKWEPA KODI NA KUJIPATIA BIL. 188.9/=

Mfanyabiashara Mustapha Kambangwa (34) mkazi wa Kongowe Mbagala, jijini Dar es Salaam (mwenye shati ya drafti nyuma ya askari) alipofikisha Mahakama ya Kisutu.

 

MFANYABIASHARA Mustapha Kambangwa  mkazi wa Kongowe Mbagala, jijini Dar es Salaam amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kukwepa kodi na kujipatia Sh.bilioni 188.9 kupitia mashine ya kieletroniki (EFD).

Mwendesha mashtaka wa Serikali Mwandamizi, Christopher Msigwa, akimsomea mashtaka  mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Mtenga, imedaiwa kuwa katika siku tofauti kati ya Juni Mosi, 2016 na Novemba 2, 2018  Kambangwa alijifanya mtu aliyesajiliwa kuwa mlipa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na kukusanya kodi ya VAT  Sh.188,928,752,166 kwa kujifanya anakusanya fedha hizo kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Shtaka la pili, mtuhumiwa  amedaiwa kati ya Juni Mosi, 2016 na Novemba 2, mwaka huu, kwa udanganyifu alitumia mashine ya kieletroniki (EFD) yenye namba 03TZ842011315 iliyosajiliwa kwa jina la Kampuni ya Abraham’s Group LTD kukwepa kodi ya VAT yenye thamani kiasi hicho cha fedha.

Aidha mshtakiwa amedaiwa kuwa katika tarehe na kipindi hicho alijipatia au kujimilikisha fedha hizo alizozipata kutokana na makato ya kodi ya VAT ambazo zilipaswa kutolewa kwa Kamishna wa TRA, ikadaiwa mshitakiwa alitenda kosa hilo huku akijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la ukwepaji kodi.

Aidha imedaiwa kuwa mshtakiwa kwa vitendo vya makusudi vya kukwepa kodi alitumia mashine ya EFD na huku akijua kwamba hajasajiliwa kama mlipa kodi ya VAT na aliisababishia hasara Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya Sh. 188,928,752,166.

Hata hivyo, mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu chochote  mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali kutoka kwa DPP.

Wakili wa Utetezi, Shamo Shadrack,  aliiomba mahakama kupanga tarehe ya karibu ili kupinga  mashtaka hayo dhidi ya mshtakiwa na kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 17 mwaka huu kwa upelelezi haujakamilika.

 

Comments are closed.