The House of Favourite Newspapers

Tamasha la Faith Baptist Church, Jamhuri kunoga

KESHO Jumapili nyasi za Uwanja wa Jamhuri, Morogoro zitawaka moto kutokana na tamasha kubwa la Faith Baptist Church kufanyika uwanjani hapo. Tamasha hilo litafanyika uwanjani hapo ambapo kwa mwaka huu itakuwa mara ya tano mfululizo kufanyika.

 

Tamasha hilo ambalo huandaliwa na Kanisa la Faith Baptist litahusisha mahubiri pamoja na mechi kati ya Yanga na Mawenzi Market.

 

Muandaaji wa tamasha hilo, Mchungaji, Jerry Wyatt, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, mbali na mechi hiyo ya kirafiki kati ya Yanga na Mawenzi, pia kutakuwa na mahubiri ambayo yatatolewa na yeye wakati wa mapumziko.

 

“Tamasha letu la Faith Baptist Church linafanyika Julai 28, katika Uwanja wa Jamhuri. Kutakuwa na mechi kati ya Yanga na Mawenzi Market ya hapa Morogoro.

“Lakini wakati wa mapumziko kutakuwa na waimbaji kutoka kanisani kwetu ambao wataimba pamoja na mimi nitahubiri wakati huo, lakini pia tutakuwa na zoezi la kugawa vitabu vidogo vya Yohana na Warumi. “Kwenye tamasha hilo hakuna kiingilio, itakuwa bure na tunawakaribisha watu wote waje siku hiyo.

 

Tamasha hilo litaanza asubuhi ambapo tutafanya ibada kisha baadaye ndiyo mambo hayo yataendelea. “Huu ni mwaka wa tano tunalifanya tamasha hili ambapo huwa mwishoni mwa mwezi wa saba.

 

Hadi sasa bado mgeni rasmi hajathibitisha lakini tutakuwa na wageni wengine kutoka nchini Marekani. “Tumefanya tamasha hili liwe bure kwa sababu tunataka watu waje kwa wingi siku hiyo,” alisema Mchungaji Jerry.

Comments are closed.