The House of Favourite Newspapers

Tamko la Mtandao wa Wanawake Katiba, Uchaguzi na Uongozi Kuhusu Kuchapwa Viboko Kwa Wanawake

0

Mnamo tarehe 14/12/2022, Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi ulipokea kwa mshtuko mkubwa taarifa iliyonukuliwa na chombo kimoja cha habari kilichojulikana kama Gadi TV. Taarifa hiyo ya kushtusha, na kukasirisha inaelezea kitendo cha Diwani anayejulikana kwa jina la Macho Salehe wa Kata ya Kasisi, Wilaya ya Urambo, Mkoani Tabora kuwachapa viboko wanawake wakongwe kwa shutuma za kujishughulisha na masuala ya uchawi na ushirikina.

Taarifa hizi za viongozi kuhusishwa na vitendo vya ukatili na matumizi mabaya ya mamlaka hapa nchini zinazidi kuongezeka.Hivi karibuni katika kipindi cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, tulishuhudia binti mmoja aliyejulikana kama Florenencia Mjenda ambaye alieleza kupitia vyombo vya habari tukio la kupigwa na Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Mkoani Mbeya hadharani kwa kosa linalosemekana kukalia jukwaa kimakosa. Vitendo hivi vinaonekana kushika hatamu na vikikaliwa kimya vitaendelea kushamiri na kuota mizizi.

Ni jambo la kutafakarisha sana ikiwa viongozi ambao wamepewa dhamana na serikali na wananchi kuwaongoza kwa kufuata sheria na miongozo wao ndiyo wanakuwa wa kwanza kuvunja sheria. Ukatili wa kijinsia haukubaliki wakati wowote na mtu yeyote awe kiongozi ama raia wa kawaida. Uthubutu wa kuendelea kufanya vitendo hivi hususan katika kipindi hiki cha kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia vinakasirisha na kukera na vinaonyesha upungufu wa maadili na uvunjwaji wa sheria ambao unafifisha jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali pamoja na wadau wa masuala ya haki za wanawake na binadamu kwa ujumla.


USULI/CHANZO
Katika tukio hilo, mwanamke mmoja ametoa taarifa kuwa yeye, pamoja na wanawake wengine watatu na binti zao wawili mmoja akiwa mjamzito, wamechapwa viboko wakiwa wamemwagiwa maji na kupunguzwa nguo mwilini.

Kitendo hicho kimefanywa na Diwani wa Kata ya Kasisi, Wilaya ya Urambo, Mkoa wa Tabora kwa madai kuwa wanawake hao ni wachawi na washirikina ambao wamekuwa wakichukua vyakula vya watu kwa nguvu za kishirikina wakati wa usiku. Wanawake hao walipatwa na kadhia hiyo wakiwa katika shughuli zao za kujipatia kipato ambapo kufuatia tukio hilo walipoteza mazao na vitu mbalimbali. Tukio hilo pia liliwasababishia maumivu makali ya mwili na viungo, limewadhalilisha wao binafsi, familia zao na jamii nzima.

Mpaka taarifa hizi zinatufikia, tayari familia za wanawake hao zilikuwa zimelazimika kuhama makazi na kwenda kuishi maeneo mengine kwa kuogopa vipigo zaidi, kubomolewa nyumba zao na vitisho dhidi ya maisha yao ambavyo walivipata kutoka kwa Diwani huyo. Mtandao unajiuliza, Je usalama wa hawa watu uko wapi? Mali zao walizoacha zipo salama? Huko walipo wamepewa ulinzi? Vitendo hivi vya kikatili ni mwendelezo wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu huku wanawake wakiwa ndiyo wahanga wakubwa wa matukio hayo hapa nchini, havipaswi kufumbiwa macho, havivumiliki na havikubaliki na tunavilaani kwa nguvu zote.

KUHUSU SHERIA
Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi unatambua vema kuwa kitendo cha kuchapa (mtu) mwanamke ni kutokuheshimu utu wa mwanamke na ni matumizi mabaya ya mamlaka ambayo ni kinyume na Katiba na Sheria za Tanzania. Mathalani katika Ibara ya 12(i)i ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasisitiza kuwa kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake. Vilevile, ibara ya 13(i)ii imeainisha umuhimu wa usawa na haki bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.
Tanzania pia inatambua na kutekeleza maazimio ya Tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ambalo linasisitiza chini ya Ibara ya 3 haki ya kuwa huru na kulindwa, vilevile Ibara ya 9 ya Tamko hilo, inaeleza kuwa hakuna mtu anayepaswa kukamatwa kiholela na kuwekwa ndani au kulazimishwa kwenda uhamishoni. Vilevile, kitendo cha kujichukulia sheria mkononi, kujeruhi na kusababisha madhara ni kosa la jinai sawasawa na kifungu cha 225 na kifungu cha 228(a) cha sheria ya Kanuni ya Adhabu/ Penal Code [CAP. 16 R.E. 2022]
Aidha, kanuni kuhusu maadili ya madiwani zimeweka bayana umuhimu wa kuheshimu na kuzingatia sheria kwa madiwani ikiwa ni pamoja na kuendesha shughuli zao kufuatana na dhamana waliyopewa na wananchi.

KAULI YETU
Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi pamoja na kuipongeza Serikali kwa hatua ilizozichukua kufuatilia suala hili kupitia Wizara Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum; bado tunaona haja ya suala hili kuwekewa msisitizo na hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi ya wanaokwamisha zoezi la upatikanaji wa haki kwa ukatili mkubwa uliotendeka. Hivyo basi, Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi unalaani kitendo hicho na tunatoa wito kwa Serikali na jamii nzima kwa ujumla:
1. Tunatoa wito kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum; Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; pamoja na Jeshi la Polisi Tanzania kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kufanya upelelezi kwa wale wote waliohusika katika tukio hili la kinyama na la kusikitisha, kuwarejesha wanawake hao katika makazi yao pamoja na kuwapatia ulinzi. Pia tunashauri suala hili lifuatiliwe na kushughulikiwa kwa uwazi ili wananchi wote waweze kurejesha imani ya utawala wa sheria na upatikanaji wa haki kwa viongozi na serikali kwa ujumla.
2. Mtandao unaendelea kutoa wito kwa jamii kutovifumbia macho vitendo dhalilishi, vya kikatili, vya kinyama na vya uvunjifu wa haki kwa wanawake na jamii nzima, kuchukua hatua na kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi vitendo hivyo vinapofanyika
Mwisho, Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi unatoa pongezi za dhati kwa uongozi wa Gadi TV pamoja na mwandishi wa habari aliyehusika kuandaa rekodi hiyo kwa kutumia taaluma yake vizuri na kuwa mfano wa kuigwa na jamii,waandishi na vyombo vingine vya habari.
TAMKO HILI LIMETOLEWA NA MTANDAO WA WANAWAKE KATIBA, UCHAGUZI NA UONGOZI WENYE MASHIRIKA WATETEZI WA HAKI ZA WANAWAKE ZAIDI YA 150 HAPA NCHINI.

Leave A Reply