The House of Favourite Newspapers

TANASHA ANATEMBELEA NYOTA ZA MOBETO, ZARI?

MUNGU anapoamua kukuinua ni wakati wako tu ukifika, kikubwa ni kuweka jitihada. Hivi karibuni mpenzi wa Nasibu Abdul ‘Diamond’ Tanasha Dona amechomoka na wimbo wake unaokwenda kwa jina la Banger, swali ni kwamba kweli anaweza muziki, ameshawishiwa na Mondi au anatembelea nyota za wapenzi wa staa huyo wa zamani, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ na Hamisa Mobeto?

 

Uzuri ni kwamba dunia ya sasa kitu kizuri huwa kinaonekana. Unapotoa kazi yako kama hivi ya kimuziki, angalia muitikio wa comments za mashabiki utajua kama unakubalika au la.

Mashabiki wanajua muziki mzuri japo wao hawajui hata kushika kipaza sauti. Mashabiki ni wataalamu wa kuuchambua muziki kuliko hata Mwalimu Kashasha anavyofanya kwenye mpira.

 

NI SUALA LA MUDA

Tanasha kama kweli amekuja kwenye muziki bila kufuata ushawishi wa mtu, kama kweli ana kipaji halisi basi muda tu utazungumza maana uhai wa muziki wake ndio utakaotoa majibu kwamba ni mzugaji kwenye fani au la.

 

TUMUANGALIE ZARI

Zari aliingia kwenye muziki kabla hata hajakutana na Diamond, alishatoa ngoma kadhaa kama Jukila (Januari 24, 201), Hotter than Them (Machi 12, 2012), Toloba (Aprili 11, 2011) na baadaye alimalizia na Nkaaba aliyoitoa Januari 24, 2015.

Zari anaonekana alianza kuhangaikia muziki kitambo, alipoona unamtoa kwenye mstari akaamua kuuweka pembeni na kujikita zaidi kwenye uandaaji wa matamasha na mambo mengine ya kiburudani.

 

Alipoona yeye muziki sio mahali pake, akachungulia upande wa pili, akamuona Diamond ambaye amejilengesha kwenye masuala ya uhusiano, akasema hii ni fursa, akamtumia sana katika kutengeneza pesa zaidi katika matamasha mbalimbali waliyoyaandaa pamoja.

Penzi lilipokufa Februari 14 mwaka jana, Zari kwa sasa ameendelea na maisha yake katika miradi yake mingine ikiwemo shule ambazo zinatajwa kuwa alichuma akiwa na marehemu mume wake, Ivan Semwanga.

VIPI MOBETO?

Mobeto ambaye alitokea kwenye mashindano ya ‘umisi’, baada ya kutoka na Diamond na kufanikiwa kupata mtoto mmoja, naye aliamua kujikita kwenye muziki wakati ambao tayari wawili hao hawana maelewano mazuri.

Alianza kuachia Madam Hero (Septemba 18, 2018) baadaye akaja na Tunaendana (Novemba 18, 2018), akaufunga mwaka huku mashabiki wakionesha kumuunga mkono kutokana hasa na jinsi alivyojitangaza mitandaoni.

Mapema mwaka huu, mrembo huyo akaja na Sawa (Februari 17), wimbo huu ulipigwa madongo sana mitandaoni tofauti na zilizotangulia. Baada ya wimbo huo, Machi 27 amekuja na My Love ambao ndio unaendelea kutamba hadi sasa.

 

TATHMINI YA JUMLA

Kimsingi Mobeto kama kweli amedhamiria kwa dhati kufanya muziki na kipaji kipo basi akomae maana kweli kuna vitu vinapungua katika nyimbo zake, anaweza kuwa anabebwa na biti pamoja na video kali lakini suala la sauti bado ni changamoto kwake.

 

Zari yeye alishanyoosha mikono mapema, alichagua bega la kuingiza hela. Kaimba nyimbo zake za Kiganda lakini mwisho wa siku akaona isiwe tabu, karata yake ipo sehemu nyingine.

Tanasha japo inaelezwa kwamba aliwahi kujaribujaribu huko nyuma kuimba bila mafanikio, anapaswa naye kujitafakari na kuona kama anatosha kwenye muziki maana kiukweli hata huo wimbo alioanza nao bado haujaeleweka kivile.

Makala: Erick Evarist, Amani

Comments are closed.