The House of Favourite Newspapers

Tanga: Mgombea wa CHADEMA Nusura Aporwe Fomu

Mapema majira ya saa tano leo Jumatatu, Agosti 20, 2018, Mgombea Ubunge Jimbo la Korogwe Amina Ally Saguti akisindikizwa na Viongozi wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Mkoa wa Tanga na Wilaya na Jimbo la Korogwe amefika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Korogwe kurejesha fomu zake za kugombea ubunge, lakini katika hali ya kushangaza Msimamizi wa Uchaguzi amekataa kupokea fomu hizo kwa madai kuwa ameelekezwa apokee fomu zote saa kumi jioni.

 

Mbali ya kukataa kupokea fomu hizo, Msimamizi huyo aliyejulikana kwa jina la Samia, aliondoka ofisini kwake na kuelekea mahali ‘kusikojulikana’.

Viongozi pamoja na Mgombea Ubunge Amina Saguti wakalazimika kwenda kumuona Mkurugenzi wa Wilaya ya Korogwe lakini wakiwa njiani (ofisini hapo) akatokea mtu aliyejaribu kumnyang’anya fomu Bi. Amina. Jaribio ambalo lilishindikana baada ya watu waliokuwepo eneo hilo kufanikiwa kumzuia ingawa aliweza kukimbia na kuondoka kwa pikipiki iliyokuwa ikiendeshwa na mtu mwingine.

 

Baada ya kushindwa kwa jaribio hilo, viongozi hao wa CHADEMA pamoja na mgombea walifika ofisini kwa Mkurugenzi (ambaye imedaiwa kuwa ni mgeni hapo na ameanza majukumu yake leo) ingawa hawakufanikiwa kumuona kwa sababu naye alitoka kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, kwa madai kuwa alikuwa ameitwa huko.

 

Hadi sasa mgombea huyo yuko Ofisi ya Mkurugenzi kusubiri kurejesha fomu hizo. Tayari Chama kupitia kwa Katibu Mkuu Dkt. Vincent Mashinji kimewasiliana na Mkurugenzi wa NEC, Dkt. Athumani Kihamia kwa ajili ya hatua za haraka kuhakikisha fomu zinapokelewa kwa ajili ya uteuzi.

 

Huko Monduli, tayari Mgombea kwa tiketi ya CHADEMA ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Lepurko, Yonas Masiaya Laizer amesharejesha fomu zake za kugombea jimbo hilo.

 

Kwa upande wa Jimbo la Ukonga, Mgombea Ubunge wa CHADEMA Asia Daudi Msangi anarejesha fomu zake mchana huu (muda huu) katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Jengo la Anatouglou.

Afisa Habari ya Chadema 

Tumaini Makene

Comments are closed.