The House of Favourite Newspapers

Tanzania Na Ufaransa Waingia Makubaliano Ya Kushirikiana Katika Sanaa Na Utamaduni Kupitia Basata Vibe

0
Waziri wa Sanaa na Utamaduni Dkt. Damas Ndumbaro (kushoto) na Balozi Mdogo wa Ufaransa hapa nchini, David Guillon wakiliana saini mkataba wa kushirikiana masuala ya sanaa na utamaduni.

Dar es Salaam, 14 Septemba 2023: Nchi ya Tanzania na Ufaransa zimeingia makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya sanaa na utamaduni kupitia mradi wa Basata Vibes unaotarajiwa kukuza hadhi ya sanaa na vipato kwa wasanii wa nchi hizi mbili kupitia ushirikiano huo.

Hafla ya makubaliano hayo ilifanyika jana Alhamis katika Kituo cha Utamaduni wa Watu wa Ufaransa cha Alliance  kilichopo Upanga jijini, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Sanaa na Utamaduni, Dkt. Damas Ndumbaro.

Balozi wa Basata, Mrisho Mpoto ‘Mjomba’ (kushoto) na wageni wengine waalikwa wakishuhudia matukio kwenye hafla hiyo.

Upande wa Ufaransa uliwakilishwa na Balozi Mdogo wa Ufaransa, David Guillon na Mkurugenzi wa kituo hicho, Bi Flora Valleur pamoja na raia wengine wa Ufaransa.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri Ndumbaro alisema lengo la mradi huo wa Basata Vibes ni kuunganisha sanaa na utamaduni wa Ufaransa na Tanzania ili kupiga hatua kwa pamoja.

Waziri Ndumbaro amesema pamoja na kuunganisha tamaduni hizo lengo lingine ni kuboresha na kuongeza kipato kwa wasanii wetu ambao kupitia Basata Vibe watakuwa wakifanya kazi kimataifa na kujiingizia pesa za kigeni.

Ameendelea kusema kuwa kupitia mradi huo wasanii wa hapa nchini watakuwa wakienda kufanya sanaa Ufaransa na wasanii wa Ufaransa na watakuwa wakija kufanya sanaa hapa nchini.

Waziri Ndumbaro katika kuongezea amesema ushirikiano huu mwema unaweza kupiga hatua mpaka kufikia kwenye masuala ya soka.

Wasanii wakitumbuiza kwenye hafla hiyo.

Kwa upande wake Balozi Mdogo wa Ufaransa hapa nchini, Guillon amesema amefurahishwa sana na mradi huo na kuahidi kuusimamia vyema ili kuhakikisha unafikia malengo waliyotarajia.

“Hii ni hatua kubwa sana ya ushirikiano na mimi kama balozi nitahakikisha mradi huu nausimamia vyema kama tulivyokubaliana kwa manufaa ya sanaa ya nchi hizi mbili.”

Baada ya kusema hayo, balozi huyo na Waziri Ndumbaro walitiliana saini mkataba huo wa ushirikiano huku ukishuhudiwa na wadau mbalimbali.

Balozi Mdogo wa Ufaransa, David Guillon akizungumza kwenye hafla hiyo.

Miongoni mwa waliohudhuria ulitilianaji saini wa mkataba huo ni mabalozi wa Basata, Mrisho Mpoto ‘Mjomba’ na Ritha Paulsen ‘Madam Rita’, wengine ni Katibu Mtendaji wa Basata Dkt. Kedmon Mapana, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Filamu, Emmanuel Ndumukwa, Rais wa Shirikisho la Muziki, Ado Novemba na wengineo.    HABARI/PICHA NA RICHARD BUKOS/ GLOBAL PUBLISHERS

Leave A Reply