The House of Favourite Newspapers

Tanzania Yaweka Historia Katika Maendeleo na Ustawi wa Sekta ya Masoko ya Mitaji Kwa Mwaka 2023

0
CPA. Nicodemus Mkama

Tanzania imeweka alama kubwa ya mafanikio katika maendeleo na ustawi wa sekta ya masoko ya mitaji katika kipindi cha mwaka 2023, ambapo bidhaa mpya na bunifu zinazowezesha kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi zimeidhinishwa na kuorodheshwa katika soko la hisa kwa mafanikio makubwa.

 

Bidhaa hizo ni pamoja na hatifungani za kijani yaani green bond, hatifungani zenye mguso kwa jamii yaani social bond na hatifungani zenye kukidhi misingi ya Shariah yaani Sukuk bond. Matokeo haya yameiweka Tanzania katika ramani ya masoko ya mitaji ulimwenguni yanayotoa bidhaa mpya na bunifu, zinazovutia wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.

Mafanikio hayo yametokana na mazingira wezeshi, shirikishi na endelevu ya kisera, kisheria na kiutendaji ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi madhubuti wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Aidha, sera za uchumi wa kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa zinazotekelezwa chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, zimekuwa chachu yenye matokeo chanya katika kukuza ushiriki wa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa na hivyo kuleta mafanikio makubwa zaidi katika masoko ya mitaji.

CMSA, ambayo ni Mamlaka yenye jukumu la kusimamia na kuendeleza masoko ya mitaji hapa nchini imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza mikakati ambayo imewezesha kufikia mafanikio hayo. Mamlaka imetekeleza mikakati ambayo imewezesha kufungua Nyanja na fursa mpya katika masoko ya mitaji.

Mikakati hiyo ni pamoja na: kuanzisha bidhaa na huduma mpya, bunifu, zenye mlengo maalum na matokeo chanya kwa jamii; matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika kutoa huduma; kuongeza idadi ya wataalamu wanaokidhi viwango vya kimataifa; na kutoa elemu kwa umma kuhusu fursa zinazopatikana katika masoko ya mitaji.

Jitihada hizi zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji na mauzo katika soko la hisa, ambapo thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji imeongezeka kwa asilimia 10.1 na kufikia shilingi trilioni 37.4 katika kipindi kilichoishia Desemba 2023, ikilinganishwa na shilingi trilioni 33.9 katika kipindi kilichoishia Desemba 2022.

Jumla ya mauzo ya hisa na hatifungani yameongezeka kwa asilimia 31.0 na kufikia shilingi trilioni 4.2 katika kipindi kilichoishia Desemba 2023, ikilinganishwa na shilingi trilioni 3.7 katika kipindi kilichoishia Desemba 2022.

Mauzo ya hatifungani yameongezeka kwa asilimia 29.4 na kufikia shilingi trilioni 3.9 katika kipindi kilichoishia Desemba 2023, ikilinganishwa na shilingi trilioni 3.0 katika kipindi kilichoishia Desemba 2022; na Mauzo ya hisa yameongezeka kwa asilimia 68.5 na kufikia shilingi bilioni 225.2 katika kipindi kilichoishia Desemba 2023, ikilinganishwa na shilingi bilioni 133.7 katika kipindi kilichoishia Desemba 2022;

Aidha, thamani ya Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja imeongezeka kwa asilimia 51.2 na kufikia shilingi trilioni 1.8 katika kipindi kilichoishia Desemba 2023, ikilinganishwa na shilingi trilioni 1.2 katika kipindi kilichoishia Desemba 2022.

 

Fungu la 10 la Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana limeipa CMSA jukumu la kuanzisha kuendeleza na kusimamia masoko ya mitaji hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuandaa kanuni na miongozo ya utoaji wa bidhaa na huduma mpya, bunifu na zenye mlengo maalum.

Katika kutekeleza jukumu hili, katika kipindi cha mwaka 2023, CMSA imeshirikiana na wadau wa masoko ya mitaji kuandaa miongozo ya kuendesha na kusimamia bidhaa za mitaji halaiki yaani Guidelines for Operations and Regulations of Crowdfunding.

Bidhaa hizi zitawezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo za kampuni changa, ndogo na za kati yaani startup, micro, small and medium enterprises. Aidha, CMSA imeshirikiana na wadau wa masoko ya mitaji kuandaa miongozo ya utoaji wa hatifungani zinazokidhi misingi ya Shariah yaani Guidelines for Corporate Sukuk Bonds. Miongozo hii imeidhinishwa na Wizara ya Fedha na imefanikiwa kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali kwa matumizi ya umma.

 

CMSA pia imeshirikiana na wadau wa masoko ya mitaji kuandaa miongozo ya utoaji wa bidhaa zenye mlengo maalum zinazolenga kupata fedha za kutekeleza miradi inayotunza na kuhifadhi mazingira na yenye mguso na matokeo chanya kwa Jamii yaani Draft guidelines for sustainability bonds.

Uwepo wa Miongozo hii utawezesha hatifungani za kijani (green bonds), hatifungani za bluu (blue bonds) na hatifungani zenye mguso kwa jamii (social bonds) kutolewa zaidi kwa umma na kuorodheshwa kwenye soko la hisa. Rasimu ya Miongozo hii imesambazwa kwa wadau kwa ajili ya kupata maoni na baada ya hapo itawasilishwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya kupata idhini na hatimaye kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali kwa matumizi ya umma.

 

Maandalizi ya Miongozo hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Serikali wa njia mbadala za kugharamia miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi yaani Alternative Project Financing (APF) Strategy wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu.

CMSA pia imetekeleza mkakati wa kuwezesha utoaji wa Hatifungani za Serikali za Mitaa na Taasisi za Umma yaani Municipal and Subnational Bonds ili kuwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa (Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya) na Taasisi za Umma, ikiwa ni pamoja na Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira kupata fedha za kugharamia miradi ya kimkakati yenye uwezo wa kujiendesha kibiashara.

Jitihada hizo zimeiwezesha Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Jiji la Tanga (Tanga-UWASA) kuwa Taasisi ya kwanza nchini kukidhi vigezo na kupata idhini ya CMSA ya kutoa hatifungani ya miaka 10 yenye thamani ya shilingi bilioni 53.1 itakayowezesha kupata fedha za kutekeleza shughuli za ujenzi wa miundombinu ya maji na utunzaji wa mazingira katika jiji la Tanga.

Hatifungani hii itakuwa ni hatifungani ya kwanza nchini Tanzania kutolewa na Taasisi ya Serikali na ambayo inakidhi matakwa ya Kanuni za Jumuiya ya Kimataifa ya Masoko ya Mitaji ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira (the first Sub-National Water Infrastructure Green Revenue Bond).

  Katika jitihada za kuongeza wataalamu wenye weledi na ujuzi kwa ngazi ya kimataifa kwenye masoko ya mitaji, CMSA kwa kushirikiana na Taasisi ya Uwekezaji na Dhamana ya nchini Uingereza yaani Chartered Institute for Securities and Investment imetoa mafunzo yanayotambulika kimataifa kwa watendaji wa masoko ya mitaji hapa nchini.

Mafunzo haya yamewezesha kujenga uwezo na ufanisi kwa watendaji wa masoko ya mitaji, ambapo idadi ya wataalamu wanaokidhi viwango vya kimataifa imeongezeka kwa asilimia 8.3 na kufikia 798 katika kipindi kilichoishia Desemba 2023 kutoka 737 katika kipindi kilichoishia Desemba 2022.

Mafunzo haya yamewapatia wataalamu wa masoko ya mitaji fursa ya kupata leseni za kutoa huduma katika masoko ya Kitaifa, Afrika Mashariki na kimataifa. Aidha, mafunzo haya yamewezesha idadi ya watendaji wa masoko ya mitaji wenye leseni ya CMSA kuongezeka kwa asilimia 27.8 na kufikia 184 katika kipindi kilichoishia Desemba 2023 kutoka 144 katika kipindi kilichoishia Desemba 2022.

Katika mwaka wa Fedha 2024/2025, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imepanga kutekeleza yafuatayo:-

 

  • kuhakikisha Rasimu ya Miongozo ya utoaji wa bidhaa zenye mlengo maalum zinazolenga kupata fedha za kutekeleza miradi inayotunza na kuhifadhi mazingira na yenye mguso na matokeo chanya kwa Jamii yaani Draft guidelines for sustainability bonds inakamilika na kuwasilishwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya kupata idhini na hatimaye kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali kwa ajili ya utekelezaji;
  • Kutekeleza Mpango Mkakati wa elimu kwa umma kuhusu fursa na faida zinazopatikana kwenye masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na kutoa machapisho mbalimbali magazetini, kushiriki kwenye mahojiano ya vipindi vya Redio na Runinga, kutoa semina, warsha na makongamano kwa makundi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vijana, wanawake na walemavu;
  • Kuendelea kusimamia masoko ya mitaji kwa kutumia mfumo unaozingatia vihatarishi (Risk Based Supervision) ili kuhakikisha kwamba biashara katika masoko ya mitaji inafanyika kwa kufuata sheria, taratibu na miongozo inayolenga kulinda maslahi ya wawekezaji, kuimarisha uadilifu wa watendaji na usalama wa masoko pindi kunapotokea viashiria vya hatari;

 

  • Kuongeza idadi ya bidhaa, ambapo Mamlaka itaendelea kutoa miongozo ya utoaji na usimamizi wa bidhaa na huduma mpya, bunifu, na zenye mlengo maalum;
  • Kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Uwekezaji na Dhamana ya nchini Uingereza (Chartered Institute for Securities and Investment – CISI) katika kuendesha mafunzo yanayotambulika kimataifa kwa watendaji wa masoko ya mitaji hapa nchini ili kuongeza ufanisi na idadi ya wataalam wa masoko ya mitaji wanaokidhi viwango vya kimataifa; na

 

  • Kuimarisha matumizi ya teknolojia katika kutoa huduma za masoko ya mitaji, ambapo CMSA imepanga kuboresha mifumo ya kidigitali inayowezesha kununua na kuuza bidhaa za masoko ya mitaji. Hatua hii inatarajiwa kuongeza ushiriki wa wananchi mijini, vijijini na Diaspora katika masoko ya mitaji, na hivyo kuchangia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha yaani National Financial Inclusion Framework (NFIF III) 2023 – 2028.

 

Sekta ya Masoko ya Mitaji Tanzania ni imara na himilivu. Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) itaendelea na jitihada zenye lengo la kuchagiza na kutoa mchango chanya katika kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu. Aidha, CMSA itaendelea kujenga mazingira wezeshi na shirikishi ili kuwezesha taasisi katika sekta ya umma na binafsi kutumia masoko ya mitaji ili kupata fedha za kutekeleza miradi na shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuuza hisa kwa umma (equity financing); hatifungani za miundombinu (infrastructure bonds); hatifungani rafiki wa mazingira (green bonds); hatifungani za bluu (blue bonds); na hatifungani za taasisi za Serikali (subnational bonds).

 

Leave A Reply