The House of Favourite Newspapers

Tanzania yazungumza na mwakilishi wa WHO kuhusu Ebola

SERIKALI ya Tanzania imefanya mazungumzo na mwakilishi mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu uchunguzi wa ugonjwa wa Ebola nchini humo. Kwa mujibu wa ukurasa wa Twitter wa Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania Dkt Hassan Abbas, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Dkt Damas Ndumbaro, ndiye aliyekutana na mwakilishi mkazi wa WHO nchini Tanzania Dkt Tigest Katsela Mangestu.

Kwa mujibu wa Dkt Abbas serikali imemwita Dkt Mangestu ili kupata undani wa hoja za shirika hilo ambazo zimeripotiwa na vyombo vya habari. Dkt Abbas pia amedai kuwa katika mazungumzo hayo,

“WHO imeafiki kuwa kama kuna mahitaji ya kupata taarifa zaidi kutoka Serikali ya Tanzania lazima utaratibu ulioanishwa katika miongozo ya taasisi hiyo na ambayo imeridhiwa na Serikali ifuatwe kikamilifu,” imesema taarifa.

Mwishoni mwa wiki WHO ilitoa taarifa ya kulalamikia ukosefu wa ushirikiano kutoka serikali ya Tanzania katika utoaji taarifa kuhusu matukio yanayoshukiwa kuwa vya Ebola nchini. Katika taarifa yake ya malalamiko, shirika hilo limeeleza kwamba uwazi na kasi katika kukabiliana na virusi vya ugonjwa huo hatari ni muhimu katika kudhibiti mlipuko ambao tayari umetajwa kuwa janga la afya duniani.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa Jumamosi, WHO imeeleza kwamba kufuatia taarifa zisizokuwa rasmi kuhusu matukio ya ugonjwa huo na jitihada zake kupata taarifa kutoka kwa idara husika Tanzania kuhusu hali nchini humo, mpaka sasa hawajapokea data za kliniki, matokeo ya uchunguzi, mawasiliano na watu husika na hata matokeo ya uchunguzi wa maabara waliofanyiwa wagonjwa wanaoshukiwa.

WHO ilituma kundi la wataalamu kuchunguza tukio la ugonjwa usiojulikana na ubalozi wa Marekani ulifuatilia hatua hiyo kwa kutoa tahadhari.

Hatua hiyo ilisababisha uvumi katika mitandao ya kijamii kwamba ugonjwa huo hatari umeingia nchini Tanzania. Serikali ya Tanzania ilifutilia mbali uvumi kwamba kuna matukio ya ugonjwa wa Ebola nchini humo.

Waziri wa Afya nchini humo Bi Ummy Mwalimu aliwaambia wanahabari Septemba 14 kwamba hakuna kisa hata kimoja cha ebola katika taifa hilo. Alisema kwamba taifa hilo limejiandaa kukabiliana na mlipuko wowote wa ugonjwa na tayari limefanya majaribio ili kujua jinsi ilivyojiandaa huku ikiweka tayari vituo vya kuwatenga waathiriwa.

Chanzo :BBC Swahili

Comments are closed.