The House of Favourite Newspapers

Tatizo la Mimba Kutoka Mara kwa Mara

WIKI iliyopita tulieleza sababu ya mimba kuharibika tunamalizia kwa haya:

MIMBA KUTOKUA

Ikiwa mimba itaacha kuongezeka au kukua ni dalili nyingine ya mimba kuharibika, leo tutaeleza tatizo la mimba kutoka mara kwa mara.

Kila mtu aliye mjamzito anategemea mimba iwe inakua kila siku na iwe kubwa kulingana na umri unavyozidi kwenda mbele, ikiwa mimba iko vilevile kwa miezi kadhaa, yaani haikui au ukubwa wa tumbo haubadiliki ujue kwamba mimba hiyo imeharibika, ili kupata uhakika wahi hospitali kupimwa.

KUTOKA VIPANDE VYA NYAMA SEHEMU ZA SIRI

Ikiwa mama mjamzito atakuwa akitokwa na vipande vya nyama sehemu za siri ni dalili mbaya sana. Kutokwa na vipande vya nyama sirini ni kuashiria kwamba kuna mtoto ameharibika tumboni na mama huyu anatakiwa asafishwe kuondoa masalio yaliyobaki ili mama asiweze kupata madhara zaidi. Kama nilivyosema mwanzoni mimba nyingi zinazoharibika hasa kwa nchi zetu za Kiafrika huwa kuna uzembe wa watu kutaka kujitibu wenyewe, kutokwenda kliniki mapema na kutofuata ushauri wa kitaalamu.

Mada ya leo ni mimba kutoka mara kwa mara, hilo ni tatizo linalotokea kwa wajawazito ambao mara zote wanakumbwa wakiwa na mimba yenye umri wa chini ya wiki 20 na zikawa zimetoka mara tatu au zaidi. Mimba hizo kitaalamu huitwa Recurrent Miscarriage au Recurrent Pregnancy Loss . Karibu asilimia moja ya wanawake wenye uzazi hukumbwa na tatizo hili. Hatari ya tatizo hili kutokea huongezeka kadiri umri wa mwanamke unavyoongezeka.

SABABU

Kuna sababu nyingi za mimba kutoka mara kwa mara kama vile matatizo ya mji wa mimba ya kuzaliwa nayo yaani Congenital Malformation . Kizazi huwa hakina umbo au nafasi ya kutosha kuruhusu mtoto akue mpaka kuzaliwa. Sababu nyingine ni mjamzito kuwa na vivimbe vya mji wa uzazi Uterine Fibroids na shingo ya uzazi kulegea kitaalamu huitwa Cervical Incompetence .

Kadiri mimba inavyokua, shingo ya uzazi hushindwa kuhimili na hivyo mimba hutoka. Tatizo lingine ni kushikana kwa kuta za mji wa mimba kilaamu huitwa Asherman’s Syndrome au mjamzito kuwa na kisukari au kuwa na ugonjwa wa vivimbe vya ovari Polycystic Ovarian Syndrome au kuwa na upungufu wa homoni ya tezi ya shingo Hypothyirodism na mjamzito kuwa na ugonjwa wa Thrombophilia.

DALILI

Mara nyingi tatizo hili hutokea hasa mimba ikiwa bado changa, dalili zikijionesha wiki ya 10 au kuendelea kidogo. Mimba inayofuata kuharibika huwa katika wastani wa umri uleule wa mara ya kwanza au chini ya hapo kidogo. Dalili kuu huwa ni kutokwa na damu ukeni, mjamzito kusikia maumivu ya tumbo hasa chini ya kitovu na kiunoni na mara nyingine kutoa uchafu au sehemu ya mimba iliyoharibika. Wakati mwingine homa na kutapika vinaweza kuambatana na dalili hizo.

Itaendelea wiki ijayo

Comments are closed.