The House of Favourite Newspapers

Taxify kuanza kufahamika kwa jina la ‘Bolt’

KAMPUNI inayotoa huduma za usafirishaji Barani Afrika na Ulaya Taxify imebadilisha nembo na jina lake kuwa ‘Bolt’. Mabadiliko hayo ya alama ya utambulisho wa kampuni yamelenga kuenda sawia na malengo ya kampuni katika huduma za usafirishaji ambapo mpaka sasa tayari imepanua huduma za safari zake kwenye magari na pikipiki.

 

Akizungumza na na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu mabadiliko hayo Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi mwenza wa Bolt, Markus Villig, alisema jina hilo jipya la Bolt litaanza kufahamika hatua kwa hatua katika masoko ya kimataifa katika wiki zijazo.

 

Alisema Taxify ilizinduliwa miaka mitano iliyopita kwa malengo ya kutoa huduma za usafiri mijini kwa njia rahisi na bei nafuu.

“Kampuni hiyo ya kiteknolojia kutoka Estonia imefanikiwa kukua na kuvuka mipaka tangu kuanzishwa kwake ambapo sasa imewafikia wateja milioni 25 katika nchi zaidi ya 30 duniani, na kuifanya kuwa kampuni inayoongoza barani Ulaya na Afrika.

“Ilikuwa pia kampuni ya kwanza ya kurahisisha huduma za usafiri na kwa sasa inafanya kazi katika kupanua huduma ya usafiri wa pikpiki kwenye miji kadhaa ya Ulaya,” alisema.

Aidha, Meneja Mkazi nchini Tanzania kutoka Bolt, Remmy Aseka alisema bidhaa ya kwanza ya kampuni hiyo ya usafirishaji ilikuwa ni kutoa suluhisho la kurahisisha upatikanaji wa huduma za teksi kwa
wateja wake.

 

“Tumefanikiwa kuongeza uboreshaji katika malengo yetu, tumeanza pia kukuza jina la kampuni yetu katika maeneo mbalimbali. Lengo letu ni kutatua matatizo ya usafiri kwa kiwango kikubwa zaidi, tunataka jina la kampuni liendane na mambo yajayo ya kampuni na sio yaliyopita. Jina jipya la Bolt linamaanisha kufanya jitihada bila kutumia nguvu, hasa uzoefu wa kuzunguka katika mji kwa gari, pikipiki au usafiri wa umma.

 

“Pia inaendana na matarajio yetu kuwa baadaye huduma za usafirishaji zitakuwa kwa njia ya umeme. Pia watumiaji wa Bolt hawatahitaji kufanya mabadiliko yoyote kwenye program zao kwa kuwa Bolt itajibadilisha moja kwa moja kwenye program hizo,” alisema.

Comments are closed.