The House of Favourite Newspapers

TCRA Yaifungia Kwanza TV Miezi 6

KAMATI ya maudhui ya TCRA imeifungia televisheni ya mtandaoni ya Kwanza kwa muda wa miezi sita baada ya kukutwa na hatia ya kutoa taarifa inayohusu Dk Gwajima kupata ajali bila kutaja jina la kwanza jambo lililoelezwa kufanywa kwa makusudi kuikuza habari.

 

TCRA imezitoza faini ya Sh5 milioni na kuwapa onyo televisheni mtandao za Millard Ayo na Watetezi kwa makosa ya kutochapisha sera na mwongozo wa watumiaji katika chaneli zao za YouTube.

 

Kamati ya maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa adhabu kwa televisheni za mtandaoni kwa kukiuka misingi ya uandishi wa habari na utangazaji na kushindwa kuchapisha sera na mwongozo kwa watumiaji.

 

Chaneli za mtandaoni zilizokumbwa na rungu hilo ni Watetezi Tv, Millard Ayo na Kwanza Tv ambayo imepewa adhabu ya kufungiwa kwa miezi sita.

 

Akisoma uamuzi wa kamati Makamu Mwenyekiti, Joseph Mapunda amesema Kwanza Tv wamekutwa na kosa la kukiuka misingi ya uandishi wa habari na kanuni za utangazaji kwa kuchapisha habari iliyolenga kupotosha.

 

Amesema kupitia ukurasa wa facebook Kwanza tv iliweka video iliyobebwa na kichwa cha habari Dk Gwajima apata ajali.

 

Mapunda amesema kwa makusudi habari hiyo haikutaja jina la kwanza la Dk Gwajima hivyo kuzua taharuki hasa ikizingatiwa kuna mtu mwingine maarufu anayetumia jina hilo.

 

“Uongozi wa Kwanza Tv uliitwa mbele ya kamati ili kutoa utetezi wao, baada ya kusikiliza kamati ilijiridhisha kuwa wamefanya kosa hilo kwa makusudi ili kuikuza habari hiyo,”amesema Mapunda.

 

Pia Kwanza Tv ilikutwa na kosa la kutochapisha sera na mwongozo kwa watumiaji wake jambo linalowapa uhuru wa kuweka maudhui yoyote bila kujali athari zinazoweza kujitokeza.

 

Kwa makosa hayo mawili kamati ilifikia uamuzi wa kuifungia Kwanza Tv kwa muda wa miezi sita. Kosa la kutochapisha mwongozo kwa watumiaji wamekutwa nalo pia Millard Ayo na Watetezi Tv ambao wote wametozwa faini ya Sh5 milioni na kupewa onyo.

Comments are closed.