The House of Favourite Newspapers

TEKNOLOJIA YA KUKATA TIKETI YA MABASI KWA SMS ZA KAWAIDA

Imeanza kuzoeleka kwamba siku hizi teknolojia inaweza kufanya hata yale ambayo miaka michache iliyopita hayakuwa yakiwezekana tena! Ukitaka teksi, siyo lazima utembee mpaka kwenye vituo vya teksi kuzungumza na dereva, mkubaliane kisha ndiyo safari ianze.

Kwa kutumia simu janja yako (smart phone), huduma zimerahisishwa sana kwamba unaweza kupakua applications mbalimbali, kama Ubber, Taxify na kadhalika, kisha ukawa na uwezo wa kuita teksi mpaka mlangoni kwako kwa kubofya tu simu yako! Na si hivyo tu, ukajua mpaka bei ya safari unayotaka kwenda bila kuzungumza chochote na dereva.

Ni teknolojia ambayo tayari ipo Bongo na wajanja kibao wanaendelea kuifurahia kila siku. Hata hivyo, ili uweze kunufaika na teknolojia hii, lazima uwe na uwezo wa kumiliki smart phone! Vipi kwa wenzangu na mimi wanaomiliki simu za kawaida, zisizo na intaneti au maarufu kama vitochi?

Kwa taarifa yako, ukuaji wa teknolojia umewezesha kugundulika kwa teknolojia nyingine kali zaidi na rahisi, ambapo hata wewe unayemiliki kitochi, unaweza kupata huduma za mtandao kwa urahisi kabisa, tena ukitumia meseji za kawaida tu!

Achana na teknolojia zinazotumika kwenye nchi zilizoendelea, hii imegunduliwa na Wabongo, na unaweza kuitumia popote nchini, iwe upo Nanjilinji, Iguguno, Manyoni au Meatu, cha msingi uwe na kisimu chako cha tochi tu.

Safari Bomba ni huduma ya kisasa inayomuwezesha Mtanzania, hasa anayetaka kusafiri na mabasi ya mikoani, kuweka kukata tiketi kwa kutumia mfumo wa meseji za kawaida, ambao haumlazimu mtu kuwa na smart phone.

Unachukua kisimu chako, unatuma meseji, unaelekezwa nini cha kufanya na hatimaye unalipia tiketi yako ukiwa hapohapo ulipo, unapata seat kwenye basi ulipendalo na asubuhi ikifika, unaenda stendi na begi lako, unaingia kwenye basi na safari inaanza, kwa urahisi kabisa.

Huduma hii, imevumbuliwa na kampuni ya kizalendo ya GIKI & SIDERITE CO. LTD inayomilikiwa na vijana wa Kitanzania wanaosoma ng’ambo, ambao ni Paschal Giki na Said Hafidh Abdallah (Siderite) ambapo tayari imeshaanza kufanya kazi Bongo.

Kwa mujibu wa Wabongo hao, unachotakiwa kufanya ni kutuma meseji ya kawaida, kwenda katika namba maalum ya simu, ukieleza unataka tiketi ya kutoka wapi kwenda wapi na kwa kutumia basi gani na utapandia kituo gani.

Muda mfupi baadaye, meseji yako inajibiwa, ikikueleza mabasi ambayo yana nafasi na bei ya kila basi kwa safari uliyoichagua. Baada ya hapo, utatakiwa kuchagua namba ya siti na basi kulingana na meseji uliyotumiwa, na muda mfupi baadaye, utaletewa meseji ya kuonesha kwamba siti uliyoichagua tayari imehifadhiwa kwa ajili yako.

Utatumiwa maelezo ya namna ya kulipia, ambapo ni kwa namba maalum zilizosajiliwa kisheria, utalipia kwa kutumia mitandao ya simu na ukishakamilisha malipo, utaletewa ujumbe unaoonesha kwamba muamala wako umekamilika na unatumiwa namba ya mtu wa huduma kwa wateja ambaye kama kuna jambo hujalielewa, utampigia kwa ufafanuzi zaidi.

Baada ya hapo, unachotakiwa kufanya ni maandalizi ya safari, muda wa safari ukifika unaenda stendi na kusubiri basi ulilolichagua, likifika unaingia na kumtajia kondakta jina lako, anakuonesha siti yako na safari inaendelea, simpo kabisa.

Kuhusu usalama wa fedha zako na uhakika wa unachokifanya, upo utaratibu maalum ambao utakuwezesha kutuma fedha kwenye namba iliyosajiliwa kisheria, kama ambavyo unaweza kutoa au kutuma fedha kwa mawakala wa mitandao ya simu, kwa hiyo hakuna mianya ya kutuma kwa matapeli wale wa ‘tuma kwenye namba hii’ na ili kuwa na uhakika zaidi, tembelea kwenye tovuti yao, http://www.safaribomba.com.

Uzuri zaidi ni kwamba teknolojia hii ni ya Kitanzania, imevumbuliwa na Watanzania kwa ajili ya Watanzania! Ama kwa hakika, yajayo yanasisimua sana.

Comments are closed.