The House of Favourite Newspapers

MAMA: MSUVA SIO WA MCHEZO MCHEZO

Simon Msuva

SIMON Msuva ni kiungo mshambuliaji wa Difaâ Hassani El Jadidi ya Morocco, licha ya kuwa alionekana ni mchezaji wa kawaida alipokuwa Tanzania, kwa sasa anawakilisha nchi vizuri na anaonyesha kuwa na dalili njema za ‘kutusua’ zaidi kimataifa.

Alitua El Jadidi mnamo Julai 29, mwaka jana kwa dau la dola 150,000 (Sh milioni 337), lakini ndani ya muda mfupi thamani yake imeongezeka na inatajwa kuwa ni euro 475,000 (Sh bilioni 1.3).

Hayo ni mafanikio ambayo yanaweza kuwa hamasa nzuri kwa vijana wengine wa Tanzania lakini nje ya uwanja staa huyo amekuwa akijipanga kwa kutengeneza maisha ambayo anaweza kuishi baada ya soka. Championi Ijumaa limezungumza na mama mzazi wa Msuva, Suzan James Msuva ambaye ameelezea mengi kuhusu mwanaye:

Akiwa mdogo uliona dada za kipaji chake?

“Ndiyo, kuna kitu niliona, pia alikuwa siyo mwepesi wa kukata tamaa. Alianza kutambaa akiwa na umri wa miezi saba, siku hiyo mimi na baba yake tulishangaa sana kwa jinsi alivyokuwa anatambaa na kurukia vitu. “Hadi leo, mimi na baba yake tunakumbuka tukio hilo, alikuwa mdogo lakini alifanya mambo ambayo yalionekana tofauti na umri wake.

Ulijisikiaje kumuona akicheza kwa mara ya kwanza?

Mama Mzazi wa Msuva, Suzan James Msuva akiwa na mumewe.

“Alipoanza kucheza na kuitwa katika timu ya taifa ya vijana ya Serengeti Boys nilifurahi sana na nikaanza kuomba kwa Mungu. “Tulishangaa na kuona kumbe inawezekana na sisi familia ya Msuva tumemtoa mtu anayetegemewa na taifa awali tulikuwa tunasikia kwa wenzetu tu.

Ulikuwa na kipingamizi chochote kwa Msuva?

“Awali sikupenda acheze mpira na sikumsapoti sana, pia nilikuwa sijui mambo ya mipira, nilitamani asome sana afike chuo kikuu kama vijana wengine.

“Lakini baba yake alinieleza kuwa mwanetu anaonekana anaujua mpira, hivyo akaniomba tumsapoti na kweli nilikubali, hadi leo tunamuombea sana aweze kufanikiwa huko aliko aweze kufika Ulaya hata akipata timu Hispania itakuwa vizuri.

Uliumizwa na nini alipokuwa anacheza Yanga?

“Kuna siku Yanga ilicheza na Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa, mashabiki walimzomea, niliumia sana kwa kuwa nilikuwa nikishuhudia tukio lile. Baada ya hapo tuliomba Mungu apate timu nyingine nje. “Kweli ikawa hivyo, yaani yunatamani afike mbali kama mwenzake Mbwana Samatta.  Msuva ana nyumba ngapi?

“Namshukuru Mungu, Msuva ametunufaisha sana wazazi wake, hapa tunapokaa ni nguvu yake, ametutoa Ubungo tulipoanza maisha na baba yake ambapo ndipo tulipokuwa tukiishi na kuhamia huku tulipo sasa. “Ana nyumba mbili alizojenga, moja hii tunayokaa wazazi wake na nyingine ipo Kinyerezi anaimalizia.

“Ukiachana na nyumba hizo pia ana viwanja vinne maeneo ya Madale, Kwembe, Bunju na Kinyerezi. “Gharama kwa jumla ya jumba hili tunayokaa hapa Mbezi Makabe inagharimu zaidi ya shilingi milioni 100 na alijenga kabla ya kwenda Morocco alipokuwa akicheza Yanga.

“Jumla ya gharama za mali zake haipungui shilingi milioni 300 pamoja na magari Toyota Harrier ya takribani Sh milioni 50 na Toyota Noah Sh milioni 50.

Una mshauri nini kuhusu ndoa?

“Kuoa kwa kweli ni mipango yake, hatuwezi kumzuia ni maamuzi yake mwenyewe, naona ni suala la malengo tu kwa sasa bado hajapanga. Sisi wazazi hatuna kipingamizi chochote kwake.

Ushauri kwa wadogo zake.

“Wanangu wote huwa nawaambia kabisa wasiwe watu wa kukata tamaa waangalie mfano hai kwa kaka yao ambaye amekuwa akifanya vyema.

Umejipangaje kulitumia jina la Msuva kujinufaisha kibiashara?

“Nina mpango wa kufungua saluni kubwa maeneo ya Kinondoni zitakuwa mbili ya kike na ya kiume itakayopewa jina la Msuva Family. “Nahitaji Msuva akiwa anakuja huku awe anatumia saluni hiyo kujipendezesha kwani yeye ni kijana anapenda kupendeza, ni matumaini yangu kuwa watu wengi wataunga mkono.

Msuva akija anakusaidia kazi? Chakula gani anapendelea?

“Msuva hana shida kabisa kulingana na jinsi nilivyowalea wanangu, ni mkarimu sana na ni msikivu akifika hapa huwa ananisaidia kupika chakula bila ya kujali kitu chochote.

“Wakati mwingine anataka kutuonyesha mapishi ya Kiarabu ni mpishi mzuri sana kwa kuwa hata huko aliko anajipikia mwenyewe. “Chakula anachokipendelea kwa upande wake ni wali maharage au kuku wa kukaanga au mchemsho lakini nyama hapendelei sana.

Vipi maisha ya Msuva kwa jumla na uhusiano na majirani?

“Msuva ni mtu wa watu tangu alipokuwa hapa alikuwa hana shida na mtu kila mmoja yeye ni rafiki yake na hapendi makuu na hata huko aliko Morocco anapenda kukaa karibu na Waarabu ili ajifunze lugha na tabia ya kule, wamekuwa wakimpenda sana. 

Kwa sasa unajishugulisha na nini?

“Awali nilikuwa mfanyakazi wa chuo kikuu katika upande wa usafi wa majengo lakini kwa sasa nimeamua kupumzika mwanangu amenitaka nipumzike kwa ajili ya kuendeleza miradi yangu ikiwemo ufugaji wa kuku hapa nyumbani.

Aidha, kwa upande wa mzee Msuva alimalizia kwa kuwataka wazazi wote kusapoti vipaji vya watoto wao ili kufanikisha ndoto zao kama walivyofanya wao kwa kusapoti ndoto za kijana wao. Pia anaomba Mungu amfanikishe Samatta ambaye ni mshambuliaji wa Genk ya Ubelgiji aweze kufanikiwa kufika mbali zaidi huku akiomba wachezaji zaidi wa Tanzania waweze kupata nafasi ya kucheza nje ili kufikisha idadi ya wachezaji 20 ili timu ya taifa iweze kushiriki Kombe la Dunia siku moja.

Na Khadija Mngwai

Comments are closed.