The House of Favourite Newspapers

TFF Sasa Wafanya Kazi Kwenye Magari

Sweetbert Lukonge |CHAMPIONI| Dar es Salaam

UONGOZI wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mpaka sasa haujui ni lini ofisi zake zitafunguliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tangu ilipozifunga Machi 16, mwaka huu kutokana na shirikisho hilo kudaiwa kusuasua kulipa deni la Sh bilioni 1.1 linalodaiwa tangu mwaka 2010.

Kutokana na hali hiyo, uongozi huo wa TFF ulilazimika kuhamia katika hosteli zake zilizopo pembeni kidogo na zilipo ofisi hizo lakini kutokana na ufinyu wa nafasi, baadhi ya wafanyakazi wake wanalazimika kufanyia kazi zao nyumbani au kwenye magari yao ambayo huyapaki nje ya ofisi hizo.

Hosteli hizo pia zinatumiwa na timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ ambayo inajiandaa na Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa alisema kuwa wamejitahidi kadiri ya uwezo wao kuhakikisha TRA inawafungulia ofisi hizo lakini wamegonga mwamba na sasa wanapata usumbufu mkubwa katika uendeshaji wa shughuli zao za kila siku kwa ajili ya maendeleo ya soka.

“Tunakabiliwa na changamoto nyingi sana kusema kweli lakini licha ya jitihada zetu za kuomba TRA watufungulie ofisi zetu kugonga mwamba, bado hatujakata tamaa, tunaendelea kutafuta njia nyingine ambayo itatuwezesha kulimaliza suala hili kwani limetuumiza sana takribani miaka nane sasa tumekuwa tukisumbuana na TRA.

“Jambo kubwa ambalo linasumbua zaidi mpaka ikafikia hatua hiyo ya kufungiwa ofisi lakini pia kukamatwa kwa mali za TFF mbalimbali ni Sh milioni 600 ambazo zilitokana na kodi za mishahara ya makocha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ambao walikuwa wakilipwa na serikali.

“Kiasi hicho cha fedha kilitakiwa kuwa kinakatwa na Hazina ambao ndio waliokuwa wakihusika na suala zima la malipo ya mishahara hiyo lakini kwa vile katika vitabu ya TRA iliandikwa TFF, ndiyo maana wamekuwa wakitusumbua kila wakati.

“Hata hivyo, tunachofanya sasa ni kuomba mazungumzo kati yetu TFF, Hazina, TRA na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ili tuweze kuliweka sawa hili na ikiwezekana TFF iondolewe katika vitabu vya TRA kuhusiana na deni hilo kwa sababu haihusiki,” alisema Mwesigwa na kuongeza:

“Hizo fedha nyingine katika deni hilo la Sh bilioni 1.1 pia zinatokana na penalti ya kuchelewa kulipa deni hilo.”

 

Subscribe kwenye YouTube Chanel yetu ya Global TV Online ili zote kali zinazotufikia iwe nisiasa, michezo, comedy, burudani, stori za mastaa, muziki na nyingine zikufikie kwa wakati.

Comments are closed.