The House of Favourite Newspapers

The Darkest Hours (Saa Za Giza Totoro)- 2, Uchungu Uliponizidia, Niliinuka na Kuzunguka Nyuma ya Nyumba Yetu..

0

ILIPOISHIA: Uchungu uliponizidia, niliinuka na kuzunguka nyuma ya nyumba yetu, mahali kulipokuwa na makaburi mawili, moja la marehemu baba na lingine la marehemu mama. Nilipiga magoti na kuyainamia, machozi yakawa yananitoka kwa wingi huku uchungu mkali ukizidi kunitesa moyoni mwangu.

SASA ENDELEA…

“Naomba mnisamehe wazazi wangu! Yawezekana napitia haya kwa sababu sikuyatilia maanani mafundisho yenu, nateseka mtoto wenu, sina mahali pa kuegamia, imefika mahali sioni tena sababu ya kuendelea kuishi,” nilisema huku machozi yakiendelea kunitoka kwa wingi sana.

 

Waliosema kulia ni dawa hawakukosea, baada ya kulia kwa muda mrefu angalau nilianza kujihisi kama kuna mzigo fulani mkubwa umepungua ingawa macho nayo sasa yalikuwa yamevimba na kuwa mekundu sana. Niliinuka na kuanza kutembea taratibu kurudi ndani huku moyoni nikijiambia kwamba sikuzaliwa kufeli.

 

Kwanza nilipata ujasiri wa kukabiliana na tatizo kubwa la Saima, ambaye mpaka muda huo nilikuwa sijui huko aliko kama yuko hai au la! Lakini pia ilikuwa ni lazima nipambane kurejesha kila kilichokuwa changu kisha kikapotea.

 

Ilikuwa ni kazi ya hatari lakini hakukuwa na jinsi, sikuwa tayari kurudi kwenye mateso yale niliyokulia tangu nikiwa mdogo. Nilikuwa naijua hatari ambayo naenda kukabiliana nayo lakini sikuwa na namna, ilikuwa ni lazima nipambane.

Kwa jinsi nilivyokuwa nimeamua kuishi, sikuwa mtu wa matatizo kabisa na niliamua kuwa hivyo kutokana na historia yangu kutokuwa nzuri kwenye suala zima la maisha yangu binafsi lakini hiki kilichokuwa kinaendelea kwa sasa, kilinikumbusha maisha yangu ya nyuma, nikajikuta nikitamani kurudi kwenye maisha yangu ya zamani, ambayo huwa ni chukizo kubwa kwa wanadamu mpaka kwa Mungu.

 

“Hata Mungu wangu utakuwa shahidi wangu kwa hili, sina namna! Itabidi tu iwe hivyo,” niliwaza huku machozi yakinitoka tena. Nilisimama na kutembea kikakamavu mpaka nyuma ya nyumba yetu ambayo sasa ilikuwa imechakaa sana.

 

Nikasogea mpaka pembeni ya mti wa mjohoro, nikaanza kufukua kwa kutumia panga nililokuwa nimelishika. Baada ya kufukua kwa muda, hatimaye nilikutana na kitu nilichokuwa nakitafuta. Nilikitoa kisanduku kidogo cha plastiki, nikageuka na kutazama huku na kule, nilipohakikisha hakuna anayeniona, harakaharaka nilikibeba kisanduku hicho mpaka ndani.

 

Nikakiweka mezani, nikakifutafuta udongo kwa sababu kilikuwa kimekaa kwa muda mrefu ardhini na baada ya kuridhika na hali yake, hatimaye nilikifungua.

 

Bado nilikuwa nazikumbuka namba za siri nilizotumia kukifunga, macho yangu yakatua juu ya kitu kilichosababisha nitabasamu! Siyo tabasamu la furaha, la hasha! Tabasamu la kifo, tabasamu ambalo huwa linaonekana usiku wa giza totoro pekee.

 

Unaweza kujiuliza nilikuwa nimeona nini kilichosababisha nitoe tabasamu la aina hiyo? Kihulka mimi ni mpole sana na pengine upole wangu wa nje ndiyo unaosababisha wakati mwingine watu kunionea waziwazi, wakiwa hawajui ndani ya moyo wangu kumejificha kitu.

 

Ilikuwa ni bunduki ninayoipenda sana, AK47 ambayo ilikuwa imekatwa kitako na mtutu na kuifanya iwe na uwezo wa kubebeka vizuri mikononi. Jinsi nilivyoipata silaha hii hatari, ambayo kisheria haitakiwi kabisa kumilikiwa na raia, isipokuwa wanajeshi tu, ni stori ndefu sana na yenye kusisimua kwelikweli.

 

Wakati mwingine binadamu wanakuwa wepesi wa kuwalaumu wenzao kwa matokeo ya mwisho, lakini ni wachache wanaokuwa wanaujua ukweli wa nini kinachosababisha mtu fulani akafanya tukio fulani. Sikuwahi kudhani hata mara moja kwamba itafika siku nitakuwa nikiutegemea mtutu wa bunduki kufanya kile ninachokitaka.

 

Kwa kipindi kirefu ndoto zangu zilikuwa ni kusoma na kuja kuwa mtu mkubwa miashani mwangu.

 

Hata hivyo, ndoto zote hizo ziliyeyuka kutokana na matatizo niliyopitia na japokuwa baadaye niliamua kuachana na mambo hayo, siku hiyo nilijikuta nimetamani tena kufanya jambo kwa ajili ya kujitetea pamoja na kumtetea Saima wangu.

 

Hakuna kitu ambacho nilikuwa nakichukia kwenye maisha yangu kama kuonewa, shida na matatizo niliyopitia maishani mwangu vilinifanya niwe na roho ya aina yake, ambayo wakati mwingine nikikasirika utaona ni bora ukutane na mnyama mkali wa porini kuliko mimi.

 

Niliendelea kuitazama ile bunduki huku tabasamu la kifo likiwa bado limetanda kwenye uso wangu, nikainua macho na kutazama juu angani huku ile bunduki nikiwa nimeishikilia vilevile, nikaitazama tena na kujaribu kuikoki, ikakubali na kutoa mlio fulani ambao kwa kipindi kirefu ulikuwa unaashiria jambo baya na kila nilipousikia ujue kuna jambo baya lilikuwa linaenda kutokea.

Unaweza kujiuliza, nini hasa kilichotokea kwenye maisha yangu kiasi cha kufanya ndoto zangu ziyeyuke na kujikuta nikiishia kuwa mtumiaji mzuri wa bunduki za kivita wakati hata jeshini sijawahi kupitia?

 

Nikisema mtumiaji mzuri wa bunduki namaanisha hivyo, kwenye suala zima la kulenga shabaha na kufanya mashambulizi ya kushtukiza, wenyewe wanaita ‘ambush’ nilikuwa vizuri kwelikweli kiasi kwamba kipindi nilipoamua kujikita kwa asilimia mia moja kwenye kazi hiyo, licha ya umri wangu mdogo nilikuwa tegemeo.

 

Ilikuwa ikitokea ‘kazi’, basi lazima nitakuwa miongoni mwa watu wawili au watatu ambao ndiyo wanaoongoza msafara. Baada ya hapo, niligeuka huku na kule kutazama kama kuna mtu alikuwa ananitazama, nilipogundua kwamba niko peke yangu, harakaharaka nililirudisha lile sanduku palepale lilipokuwa na kulifunga vizuri, kwa kutumia ‘chepe’ nikafukia na kuparudishia kama palivyokuwa awali.

 

Kwa muda wote huo, zana yangu nilikiwa nimeivaa begani. Nilirudishia miche ya mipapai ambayo ilikuwa juu ya eneo hilo kama njia ya ‘kuwazuga’ askari wasijue chochote kilichokuwa kinaendelea kisha harakaharaka nikarudi mpaka ndani, nikachukua begi dogo lililokuwa darini na kutoka nje.

 

Begi hilo lilikuwa na vifaa maalum ambavyo kwa harakaharaka ungeweza kudhani labda ni vya ufundi wa umeme, lakini kimsingi vilikuwa ni vifaa kwa ajili ya kusafishia bunduki.

 

Harakaharaka nilianza kuifungua silaha hiyo na kwa sababu tayari nilikuwa na uzoefu wa namna ya kuifungua na kuifunga upya kwa muda mfupi, ndani ya dakika chache tu nilikuwa nimeshaifungua, nikaanza kuisafisha kwani haikuwa imetumika kwa muda mrefu kiasi.

Wakati nikiendelea na kazi hiyo, kwa mbali nilianza kusikia muungurumo kama wa gari au pikipiki kubwa ukija kwa kasi kubwa. Kengele ya hatari ikalia ndani ya kichwa changu, kwa kuwa nilikuwa nakaribia kumaliza, niliamua kuifunga hivyohivyo, harakaharaka nikairudishia na kuivaa begani.

 

Nikachukua koti langu la kazi, refu na jeusi kisha nikafunga mlango na kuzunguka nyuma ya nyumba, nikakimbia na kuyapita yale makaburi na kutokomea kwenye vichaka vilivyokuwa mita kadhaa kutoka pale nyumbani.

 

Nikaenda kupanda juu ya mti mrefu wa mkaratusi, nikawa natazama kwa mbali kuangalia muungurumo niliokuwa nausikia ulikuwa unatokea wapi kwa sababu haikuwa kawaida kwa magari kuja huko tulikokuwa tunaishi.

 

Nilichokuwa nimekihisi ndicho kilichokuwa kimetokea, niliona pikipiki mbili aina ya Honda, zile kubwa kama zinazotumika kwenye mashindano zikija kwa kasi kubwa huku wanaume wanne wenye miili mikubwa wakiwa wamepakizana wawili wawili.

 

Walikuja kwa kasi kubwa mpaka pale nyumbani kwetu, ile pikipiki ya kwanza ikasimama upande wa kulia na ile nyingine upande wa kushoto kisha wote wanne wakateremka huku wakiwa wamevaa kofia maalum za kuficha nyuso zao.

 

Japokuwa walikuwa wamejiziba nyuso zao, niliweza kuhisi moja kwa moja kwamba ni watu niliokuwa nawafahamu kwa jinsi miili yao ilivyokuwa na jinsi walivyokuwa wakitembea. Unajua kama mtu umewahi kufanya naye kazi kwa karibu, hata ikitokea akajaribu kujibadilisha, ni rahisi sana kumgundua, hivyo ndivyo ilivyotokea kwangu.

 

Nitakuja kueleza kwa kirefu baadaye ni kwa namna gani mimi na watu hawa tulifahamiana lakini chanzo cha yote, kilikuwa ni mtu mmoja tu.

Mtu ambaye awali niliamini kwamba anaweza kunisaidia kuutua mzigo mzito niliokuwa nao kichwani lakini mwisho akaishia kunibadilisha na kuwa kiumbe mwingine tofauti kabisa.

 

Basi nikiwa pale juu ya mti, niliwashuhudia watu wale wakigonga mlango kwa fujo kama walivyofanya jana yake, na walipoona kimya, walivunja mlango na kuingia ndani kibabe.

 

Nikiwa sielewi hili wala lile, nilimuona mmoja kati yao akirudi pale kwenye pikipiki, nikamuona akifungua kidumu kilichokuwa na kimiminika ndani yake ambacho kwa mbali sikuweza kugundua ni nini. Akarudi ndani kwa wenzake na kufumba na kufumbua, nilishtuka kuona moshi mwingi ukianza kutokea madirishani na pembeni ya paa.

 

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia: www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com ,  Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online. Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower)

0719401968

Leave A Reply