The House of Favourite Newspapers

 MFANYABIASHARA JELA MIAKA 30, VIBOKO 12

MBEYA: Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya imemhukumu kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela na kuchapwa viboko 12 mfanyabiashara mmoja mkazi wa Isanga jijini Mbeya, Antony Madawa baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka na kumsababishia ujauzito mwanafunzi.

 

Kwa mujibu wa Hakimu Mkazi mkoani Mbeya aliyesikiliza kesi hiyo namba 145/2018, Rashid Chaungu, mshtakiwa Madawa (58) alitenda makosa hayo, Februari, mwaka jana.

 

Hakimu Chaungu alisema mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka juu ya mtuhumiwa kumbaka mtoto wa kidato cha kwanza aliyekuwa akisoma katika Shule ya Upili- Samora, hali iliyomsababisha kupata ujauzito na kukatishwa masomo yake.

 

Alisema Jamuhuri kupitia mashahidi wake akiwemo mhanga wa tukio hilo ilithibitishwa bila kuacha shaka mfanyabiashara huyo kufanya makosa hayo hivyo kumtia hatiani kwa makosa yote mawili.

 

Awali, katika utetezi wake, mshtakiwa Madawa alikana kutenda kosa hilo huku akikosoa mwenendo wa shauri hilo kuwa baada ya tukio mhanga alichelewa kutoa taarifa kwa kuripoti tukio hilo mwezi mmoja baadaye jambo analosema haikutakiwa kuwa hivyo pia aliieleza mahakama kuwa yeye ni mwathirika, lakini binti ambaye ni mhanga hajaathirika mambo ambayo mahakama ilidai hayana mashiko katika kumtia au kutomtia hatiani mtuhumiwa.

 

Shauri hilo lilikuwa likiendeshwa na Wakili wa Serikali, Davice Msanga ambaye aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na jamii ya watu wanaotekeleza makosa kama hayo.

 

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka mshtakiwa Madawa alikuwa akishtakiwa na Jamuhuri kwa makosa mawili ya kumbaka mwanafunzi wa kidato cha kwanza kinyume na kifungu namba 130 (2) e na 131 (1) cha kanuni ya adhabu na pili ni kumsababishia ujauzito mwanafunzi huyo kinyume na kifungu namba 60 A (3) cha Sheria ya Elimu sura ya 353 na marekebisho yake kifungu namba 22 (3) cha sheria namba 2 ya mwaka 2016.

 

Akitoa hukumu hiyo, Chaungu baada ya kumtia hatiani amemhukumu mtu huyo kutumikia kifungo cha miaka 30 jela na viboko 12 kwa kosa la kwanza ikiwa ni pamoja na kumlipa fidia ya shilingi milioni mbili mhanga wa tukio hilo na kwa kosa la pili la kumsababishia ujauzito mwanafunzi huyo amemhukumu pia kutumikia kifungo cha miaka 30 jela vifungo alivyoamuru kwenda kwa pamoja.

 

Mshtakiwa Madawa alichukuliwa na Polisi tayari kwa kwenda kuanza kutumikia adhabu hiyo dhidi yake katika Gereza la Ruanda jijini Mbeya.

Stori: EZEKIEL KAMANGA, IJUMAA

Comments are closed.