The House of Favourite Newspapers

TIGO YAMZAWADIA MKIMBIAJI SHUPAVU MIAKA 93 NYUMBA

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Tigo Tanzania Simon Karikari (wa pili kulia) akikata utepe kuashiria kumkabidhi rasmi nyumba mzee Joram Mollel (93) ambaye amekuwa akishiriki mbio za Tigo Kili Half Marathon kwa miaka minne mfululizo. Kulia kwake ni mzee Mollell akifautiwa na mwanaye Elibarik Mollel pamoja na Afisa Biashara Mkuu wa Tigo Tarik Boudiaf. 
Babu Joram Molle (93)  akitoa neno la shukrani muda mfupi baada ya kukabidhiwa nyumba na Kampuni ya Tigo kutokana na ushiriki wake wa mbio za Tigo Kili Half Marathon kwa miaka minne mfululizo. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Tigo Tanzania Simon Karikari, akimkabidhi fungua za nyumba mzee Joram Mollel.
Baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni ya Tigo Tanzania wakiwa katika picha ya Pamoja.

 

 

 

KAMPUNI ya Mawasiliano ya Tigo imemkabidhi nyumba ya vyumba 17 ikiwa na samani zote za ndani Babu Joram Mollel (93), kutokana na ushiriki wake wenye mafanikio katika mbio za Tigo Kili Half Marathon kwa miaka mine mfululizo.

 

 

Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika eneo la Mushono nje kidogo ya Jiji la Arusha, ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo Simon Karikari pamona na Afisa Biashara mkuu Tarik Boudiaf.

 

Akizungumza kwenye hafla hiyo Karikari alisema, nyumba hiyo ilinunuliwa na kukarabatiwa kisha kumkabidhi Babu Mollel kama ishara ya shukrani kwa kujituma na umahiri wake katika riadha.

 

‘Babu Mollel amekuwa akishiriki mashindano ya Tigo Kili Half Marathoni kwa miaka mingi sasa. Tulipoona hali ya makazi yake si nzuri Tigo tuliona njia sahihi ni kuwezesha apate nyumba yake mwenyewe,”alisema Karikari.

 

“Katika nyumba yake hii ya hapa Mushono, Babu atakuwa anakaa katika nyumba ya kisasa, iliyo tayari na samani pamoja na vyombo vyote muhimu vya ndani. Nyumba hii pia imeunganishwa na umeme na maji. Hati ya nyumba pia ipo kwa jina lake, hivyo yeye ndiye mmiliki halali wa nyumba hii,” aliongeza Karikari.

 

Aidan Komba, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini alisema kwamba nyumba imegawanyika sehemu tatu na kuongeza kuwa Babu Mollel atakaa katika nyumba moja na mbili zilizobaki ataweza kuzipangisha na kujipatia kipato cha kuendeshea maisha yake ya kila siku.

 

“Napenda kuwashukuru sana Tigo kwa zawadi hii ya kipekee. Maneno yangu hayawezi kuelezea furaha niliyonayo. Ktendo hiki kina maana kubwa sana kwangu. Maana hivi sasa ninaweza nikasema sasa nina mahali pakuita kwangu,” alisema Babu Mollel.

 

 

Ushiriki wa Babu Mollel katika mashindano ya Kilimarathon ni wa zaidi ya miaka 15, ambapo amekuwa akiwavutia watu wengi kumshangilia wakati akishiriki mbio za marathon, pamoja na uzee wake. Katika miaka minne mfululizo iliyopita, Tigo imekuwa mlezi na mdhamini mkuu wa mbio za kilometa 21 zinayojulikana kama ‘Tigo Kili Half-Marathon’, ambayo ni nusu ya mbio kamili ya kilometa 42 za marathon ambayo hufanyika katika vilima vya Mlima Kilimanjaro, mlima mrefu kuliko wote barani Afrika.

 

“Babu Mollel ni taswira halisi ya uanamichezo, ujasiri na jitihada. Yeye ni mfano aliye hai kwamba kama binadamu tunaweza tukafanikiwa katika lolote lile ambacho tukiamua kukifanya kwa dhati, na kuondoa dhana nzima kwamba umri au changamoto zingine zozote zinaweza zikawa sababu ya kutokufanikiwa kwetu. Leo, tunamsheherekea yeye,” alieleza Karikari kuhusu mzee huyo wa miaka 93.

 

Mwaka jana, Tigo ilishirikiana na Babu Mollel katika kampeni maalum ya Tigo Kili Half-Marathon iliyoitwa ‘Tisha kama Babu’. Kampeni hiyo ilikuwa na lengo kubwa la kuhamasisha Watanzania kuweza kuishi maisha ya kujali afya zao. Wakati huo huo, Tigo pia ilisitisha rasmi namba ya mbio aliyokuwa akiitumia Babu Mollel ‘1040’ na alitambuliwa rasmi kama mwanamichezo wa heshima ‘Hall of Fame’.

Comments are closed.